Ujumbe wa Vatican kwa mfungo wa Ramadhani:ulete matunda tele,matumaini&furaha
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Katika ujumbe uliotumwa na Baraza la Kipapa la Majadiliano ya kidini, wenye mada: Wakristo na Waislamu: Zima Moto wa Vita na Washa Mshumaa wa Amani, katika fursa ya Mfungo wa Mwezi Mtukukufu wa Ramadhani na sherehe zijazo za Idi. Kwa ujumbe hywa wanataka kuwa wa ukaribu na urafiki, wakifahamu umuhimu wa mwezi huu katika safari yao ya kiroho na kwa familia yao na maisha ya kijamii, ambayo pia yanakumbatia marafiki na majirani zao Wakristo. Wanayo furaha kujua kwamba Ujumbe huu wa kila mwaka wa Ramadhani ni njia muhimu ya kuimarisha na kujenga uhusiano mwema kati ya Wakristo na Waislamu, kutokana na kuenea kwake kupitia vyombo vya habari vya kiutamaduni na vya kisasa, hususan mitandao ya kijamii. Kwa sababu hiyo, itakuwa ya manufaa kuufanya Ujumbe huu ujulikane vyema kati ya jumuiya zote mbili.
Mwendelezo wa biashara ya silaha
Katika ujumbe huo kwa njia hiyo wamependa kushiriki baadhi ya mambo ya kuzingatia kuhusu mada tofauti na ile waliyochagua kushughulikia.Bado idadi inayoongezeka ya migogoro katika siku hizi, kuanzia mapigano ya kijeshi hadi mapigano ya silaha yenye nguvu tofauti zinazohusisha mataifa, mashirika ya uhalifu, magenge yenye silaha na raia, imekuwa ya kutisha sana. Papa Francisko hivi karibuni alisema kwamba "ongezeko hili la uhasama kiukweli linabadilisha vita vya tatu vya dunia vilivyogawanyika vipande vipande kuwa mgogoro wa kweli wa kimataifa.” Sababu za migogoro hii ni nyingi, zingine za muda mrefu, zingine za hivi karibuni. Pamoja na hamu ya kudumu ya mwanadamu ya kutawala, matarajio ya kisiasa ya kijiografia na masilahi ya kiuchumi, sababu kuu hakika ni kuendelea kwa uzalishaji na biashara ya silaha. Hata kama sehemu ya familia yetu ya kibinadamu inateseka sana kutokana na matokeo mabaya ya utumizi wa silaha hizo katika vita, wengine wanashangilia kwa dhihaka ya faida kubwa ya kiuchumi inayopatikana kutokana na biashara hiyo isiyo ya kiadili. Papa Francisko ameeleza hayo kuwa "ni kuchovya kipande cha mkate katika damu ya ndugu yetu."
Uharibifu wa miundombinu na maisha kuwa magumu
Wakati huo huo, tunaweza kushukuru kwamba pia tuna rasilimali nyingi za kibinadamu na za kidini kwa ajili ya kuendeleza amani. Shauku ya amani na usalama imejikita sana katika nafsi ya kila mtu mwenye mapenzi mema, kwa kuwa hakuna anayeweza kushindwa kuona athari mbaya za vita katika kupoteza maisha ya binadamu, madhara makubwa na msongamano wa mayatima na wajane. Uharibifu wa miundombinu na mali hufanya maisha kuwa magumu bila matumaini, au haiwezekani. Wakati fulani mamia ya maelfu ya watu huhamishwa katika nchi yao wenyewe au kulazimika kukimbilia nchi nyingine kama wakimbizi. Kwa hivyo, kulaaniwa na kukataliwa kwa vita kunapaswa kuwa wazi: "kila vita dhidi ya udugu, haina maana, ni giza. Katika vita, kila mtu hupoteza." Kwa mara nyingine tena, kwa maneno ya Papa Francisko asemaye: "Hakuna vita vitakatifu, ni amani iliyo takatifu tu".
Dini zote zione maisha matakatifu
Dini zote, kila moja kwa njia yake, huona maisha ya mwanadamu kuwa matakatifu na hivyo kustahili heshima na ulinzi. Mataifa ambayo yanaruhusu na kutekeleza adhabu ya kifo, kwa bahati nzuri, yanapungua kila mwaka. Hisia iliyoamshwa tena ya heshima kwa adhama hii ya msingi ya zawadi ya uhai itachangia usadikisho kwamba vita lazima vikataliwe na kuthaminiwa amani. Ingawa pamoja na tofauti zao, dini zinakubali kuwepo na jukumu muhimu la dhamiri. Kuunda dhamiri ili kuheshimu thamani kamili ya maisha ya kila mtu na haki yake ya uadilifu wa kimwili, usalama na maisha yenye heshima kutachangia kulaaniwa na kukataa vita, vita vyovyote na vita vyote!
Tumtazame Mungu wa amani na chanzo cha amani
Tunamtazama Mwenyezi kama Mungu wa amani, chanzo cha amani, ambaye kwa namna ya pekee anawapenda wale wote wanaojitolea maisha yao kwa ajili ya huduma ya amani. Kama ilivyo kwa mambo mengi, amani ni zawadi ya kimungu lakini wakati huo huo ni matunda ya juhudi za wanadamu, hasa katika kuandaa mazingira muhimu kwa kuanzishwa na kuhifadhi. Kama waamini, sisi pia ni mashahidi wa matumaini, kama tulivyokumbuka katika Ujumbe wetu wa Ramadhani 2021 a mada ya: "Wakristo na Waislamu: Mashahidi wa Matumaini".
Mfungo uwaletee matunda tele ya amani, matumaini na furaha
Matumaini yanaweza kufananishwa na mshumaa, ambao mwanga wake huangaza usalama na furaha, ambapo moto, bila kudhibitiwa, unaweza kusababisha uharibifu wa wanyama na mimea, miundombinu na kupoteza maisha ya binadamu. Kwa njia hiyo ujumbe unahitimishwa kwa kusema kuwa: "Ndugu wa Kiislamu, tuungane katika kuzima moto wa chuki, vurugu na vita, na badala yake tuwashe mshumaa wa amani, tukichota rasilimali kwa ajili ya amani iliyopo katika mila zetu nyingi za kibinadamu na kidini. Mfungo wenu na ibada zenu nyingine za uchamungu ndani ya Ramadhani na sherehe ya ‘Id al-Fitr itakayohitimishwa, iwaletee matunda tele ya amani, matumaini na furaha.