Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko Dominika tarehe 28 Aprili 2024 anatarajia kufanya hija ya kichungaji mjini Venezia. Baba Mtakatifu Francisko Dominika tarehe 28 Aprili 2024 anatarajia kufanya hija ya kichungaji mjini Venezia.  

Hija ya Kichungaji ya Papa Francisko Mjini Venezia: Ratiba Elekekezi

Baba Mtakatifu Francisko Dominika tarehe 28 Aprili 2024 anatarajia kufanya hija ya kichungaji mjini Venezia. Baba Mtakatifu mara baada ya kuwasili mjini Venezia atatembelea Gereza la Wanawake la Giudecca, Pili atatembelea Banda la Maonesho kutoka Vatican, kisha atakutana na kuzungumza na vijana wa kizazi kipya na baadaye ataadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Uwanja wa “San Marco” mjini Venezia. Kipaumbele cha kwanza ni wafungwa, vijana na waamini.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kunako mwaka 1972 Mtakatifu Paulo VI alitembelea mji wa Venezia na baadaye mwaka 1988 akafuata Mtakatifu Yohane Paulo II na Baba Mtakatifu Benedikto XVI akatembelea Venezia mwaka 2011. Baba Mtakatifu Francisko Dominika tarehe 28 Aprili 2024 anatarajia kufanya hija ya kichungaji mjini Venezia. Baba Mtakatifu mara baada ya kuwasili mjini Venezia atatembelea Gereza la Wanawake la Giudecca, Pili atatembelea Banda la Maonesho kutoka Vatican, kisha atakutana na kuzungumza na vijana wa kizazi kipya na baadaye ataadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Uwanja wa “San Marco” mjini Venezia. Hija hii ya kichungaji ya Baba Mtakatifu Francisko mjini Venezia inanogeshwa na kauli mbiu “Kukaa kwa umoja katika upendo wa Kristo.” Hii ni sehemu ya maadhimisho ya Sikukuu ya Mtakatifu Marko, Mwinjili inayoadhimishwa na Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 25 Aprili. Huyu ni mtoto wa Maria wa Yerusalemu, mahali ambapo Mtakatifu Petro Mtume alipata hifadhi baada ya kufunguliwa kutoka gerezani: “Na alipokuwa akifikiri haya akafika nyumbani kwa Mariamu, mamaye Yohana, ambaye jina lake la pili ni Marko; na watu wengi walikuwa wamekutana humo wakiomba.” Mdo 12:12.

Maonesho ya sanaa
Maonesho ya sanaa

Mwinjili Marko alikuwa ni binamu yake Mtakatifu Barnaba, Mtume. Katika hija ya maisha yake ya kimisionari, alifuatana sana na Paulo, Mwalimu na Mtume wa Mataifa katika safari yake ya kwanza ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa Mataifa. Historia inaonesha kwamba, baadaye alifuatana na Mtume Paulo katika safari yake hadi Roma. Alikuwa ni mwanafunzi mpendwa sana wa Mtakatifu Petro, Mtume. Akajibidiisha kuandika mafundisho ya Mtakatifu Petro katika Injili yake. Rej. Mdo 12:25; 15:37-38. Mwinjili Marko alipendwa sana na Mtakatifu Petro kiasi cha kumwita “Marko mwanangu.” 1Pt 5:13. Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Katekesi yake, Jumatano tarehe 24 Aprili 2024 amesema, Mwinjili Marko amefafanua kwa kina, mapana na uthabiti wa Fumbo la Nafsi ya Yesu wa Nazareti, changamoto na mwaliko kwa waamini kuhakikisha kwamba, wanavutwa na Kristo, ili kuweza kushirikiana kwa ari na uaminifu mkubwa katika mchakato wa ujenzi wa Ufalme wa Mungu unaosimikwa katika: kweli na uzima. Huu ni ufalme wa utakatifu na neema; ni ufalme wa haki, mapendo na amani. Kimsingi Injili ya Marko ni muhtasari wa Mafundisho makuu ya Petro, Mtume!

Viongozi wa Serikali na Kanisa wako tayari kumpokea Papa Francisko
Viongozi wa Serikali na Kanisa wako tayari kumpokea Papa Francisko

Baba Mtakatifu Francisko atakapowasili mjini Venezia atatembelea Gereza la Wanawake la Giudecca na hapo atakutana na wafungwa na kuzungumza na mfungwa mmoja mmoja. Baadaye atatembelea Banda la Maonesho kutoka Vatican yanayonogeshwa na kauli mbiu “Kwa macho Yangu.” Maonesho haya yanafanyika kwa ushirikiano kati ya Baraza la Kipapa la Utamaduni na Elimu pamoja Idara ya Utawala wa Magereza sanjari na Wizara ya Sheria. Baadaye Baba Mtakatifu atakutana na kuzungumza na wasanii. Baba Mtakatifu Francisko akiwa kwenye Kanisa kuu “Basilica delle Salute” atakutana na kuzungumza na vijana wa kizazi kipya kutoka Venezia pamoja na majimbo ya Veneto. Baba ataadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Uwanja wa “San Marco” na baadaye ataongoza Sala ya Malkia wa Mbingu. Baada ya maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu, Baba Mtakatifu atakwenda kutembelea Kanisa kuu la Mtakatifu Marco ili kutoa heshima kwa masalia ya Mtakatifu Marko na baada ya hapo, ataagana na wenyeji wake na kuanza safari ya kurejea tena mjini Vatican.

Papa Venezia
26 April 2024, 14:43