Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S Jubilei ya Miaka 25 ya Daraja Takatifu ya Upadre 2024
Na Padre Philemon Anthony Chacha, SDB., - Vatican.
Mapadre wanapaswa kuwa ni mfano na kielelezo cha Kristo Yesu Mchungaji mwema, kwani wanapaswa kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya Kristo Yesu na Kanisa lake; sadaka inayojionesha katika mchakato wa maisha na utume wa Kipadre, kwa kujikita katika huduma makini kwa Familia ya Mungu wanayoihudumia. Waamini wanatambua na kuthamini sadaka ya maisha ya Mapadre wanaojitosa bila ya kujibakiza; wahudumu wa Mafumbo ya Kanisa wanaotekeleza dhamana na wito wao katika hali ya unyenyekevu pasi na makuu. Mara nyingi hawa ni viongozi wanaoonesha dira na njia ya kufuatwa wala si watu wanaotoa amri na kuendelea “kuponda maisha.” Mapadre wanaojisadaka barabara ni mfano mwema katika maisha ya kiroho na wengi wanaweza kuwatambua Mapadre wa namna hii kuwa kweli ni “Watu wa Mungu” ambao hawajamezwa na malimwengu na kutopea huko huko! Jumamosi tarehe 27 aprili 2024 katika Chuo Kikuu cha Mtakatifu Paolo, Roma nchini Italia zilitawala shwange na nderemo kwa watanzania waishio nchini humo. Hii ilikuwa ni kusheherekea Jubilei ya miaka 25 ya Daraja Takatifu ya Upadre ya Padre Richard, Mjigwa C.PP.S., wa Shirika la Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu. Padre Richard Mjigwa maarufu kama “Mtoto wa Mkulima: Falsafa ya Ufagio ni Unyenyekevu” alizaliwa tarehe 28 Novemba 1964, Makoko, Parokia ya Nyamiongo Jimbo Katoliki la Musoma. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kipadre na Kitawa, tarehe 17 Aprili 1999, Askofu Msaidizi Cesare Nosiglia wa Jimbo Katoliki la Roma, akampatia Daraja Takatifu ya Upadre kwenye Parolia ya “Corpo e Sangue di Gesù” Jimbo kuu la Roma.
Sherehe za kumpongeza Baba Richard hapa Roma zilianza na Ibada ya Misa Takatifu ya kumshukuru Mungu kwa zawadi ya Jubilei ya miaka 25, huku Padre Richard mwenyewe akiwa ndiye mwadhimishaji Mkuu wa Misa. Pembeni mwake alikuwepo Padre Paulo Kaigarula aliyezaliwa tarehe 18 Februari1970. Aliweka nadhiri za muda 10 Septemba 1995 na za daima tarehe 9 Desemba 1998. Alipewa Daraja Takatifu ya Upadre tarehe 12 Septemba 1999 nchini Italia. Huyu ndiye Mkarmeli wa kwanza mtanzania, ambaye na yeye anasherehekea Jubilei ya Miaka 25 ya Upadre. Alikuwepo pia Padre Felix Mushobozi, C.PP.S., Katibu mkuu wa Shirika la Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu kanda ya Tanzania. Padre Emmanuel Tumaini, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Watanzania Wakatoliki Italia, JWWI, na Padre Tumaini Ngonyani Litereku, maarufu kama “Baba Lite.” ambaye alikuwa Mhubiri katika Ibada hii ya Misa Takatifu. Pamoja nao walikuwepo mapadre wengi, Shemasi, Watawa, Waseminari, wageni kutoka Tanzania ambao walikuwepo hapa Roma kwa ajili ya kufanya Hija, Sigfried Filipo Nnembuka, mwakilishi wa Balozi wa Tanzania nchini Italia, ndugu pamoja na maafisa wengine wa Ubalozi.
Katika mahubiri yake Padre Tumaini Ngonyani Litereku alikazia umuhimu wa kuwa na moyo wa shukrani, furaha na unyenyekevu na kwamba, Padre awe ni sababu ya furaha ya watu wa Mungu, kama ilivyokuwa kwa Kristo Yesu, Mtumishi wa furaha. Unyenyekevu ni siri ya mafanikio katika maisha; ni kuyakubali makuu ya Mungu, tayari kuyatumia kunogesha furaha ya watu wa Mungu. Padre Lite alianza kwa kusema kuwa katika sherehe ambazo aliwahi kufurahi sana, basi moja wapo ni hii, ambayo ni kubwa ikifuata ile ya upadre wake. Padre Litereku alisisitiza katika neno Furaha, akijiliuza Furaha ile ya kweli inatoka wapi? Aliendelea kwa kusema mfano wa Furaha ni Yesu Kristo ambae pia ni Mtumishi wa furaha yetu. Huku akiendelea kutafuta chimbuko la furaha hii, aliweza kuunganisha na Injili aliyoichagua, ikiwa ni ile ya Yesu kuwaponywa wakoma kumi (Lk 17,11-19). Wakoma hawa walitengwa kwa jinsi walivyokuwa na hivyo kukosa ile furaha kwasababu walijiona kama watu ambao hawatambuliki, lakini walikuwa na matumaini kuwa siku moja watapata ile furaha ya kuponywa ule ugonjwa wao. Hivyo kukutana kwao na Yesu sala yao ilikuwa “Bwana utuonee Huruma” kwa sala hiyo ni ishara wazi kuwa walikuwa wanaomba kuponywa. Lakini Yesu anawaabia waende wakajionyeshe kwa makuhani. Lakini walipokuwa njiani mmoja wao aliposikia ameponywa anageuka kwa moyo wa shukrani na furaha anageuka kumshukuru Mungu.
Padre Tumaini anaendelea kwa kusema: “Yesu Kristo Mtumishi wa furaha yetu anapotutendea makuu anatuonesha kwanza yeye mwenyewe jinsi alivyo: hana kikomo, anajishusha, anawagusa, anawaponya na baadaye anawatuma, enenda imani yako imekuponya”. Kumbe, Yesu Kristo anategemea unyeyekevu kutoka kwetu kama ilivyo falasafa ya ufagio ya Baba Mjigwa. Hivyo tukitakaswa na kuwezeshwa katika maisha yetu, na kama tunahitaji kuwa na mafanikio zaidi, ni lazima kuwa na unyenyekevu. Unyenyekevu kwa maana ya kukubali makuu ya Mungu ambayo ametujalia na kuyatumikia kwa furaha. Kumbe, tunaitwa hata sisi kwenda kutangaza na kuwa sababu ya hii furaha kwa wenzetu. Padre Litereku alimalizia kwa kumpongeza sana Padre Mjigwa pamoja na kuahidi kumwombea na kumshukuru Mungu kwa zawadi hii ya Wito wa Upadre. Amemsihi aendelee kuwa na moyo wa furaha siku zote, aendelee kuwa na moyo wa sala, moyo wa shukrani na unyenyekevu, ili daima furaha yake izidi kuwa kubwa zaidi na kuenea kwa watu wengi zaidi, hasa wale wanaomsikiliza katika vipindi mbalimbali vya Radio Vaticani, Idhaa ya Kiswahili.
Naye Padre Richard Mjigwa, C.PP.S., katika kusheherekea Jubilei hii anasema: “Miaka 25 ya Daraja Takatifu ya Upadre ni Zawadi, ni Dhamana, ni Utume na wajibu ambao Mwenyezi Mungu amenikabidhi kuutenda na kuhushuhudia kwa watu wa Mataifa”. Itakumbukwa kuwa katika miaka hii 25, Padre Richard Mjigwa amewahi kuwa Paroko Usu kwa miaka 3 Parokia ya Mtongani, Kunduchi Jimbokuu la Dar es Salaam; Muasisi na Mhariri Mkuu Radio Mwangaza FM, Dodoma; Mkuu wa Chuo cha Ufundi cha Mtakatifu Gaspari, Kunduchi, Jimbo Kuu la Dar es Salaam; Mwandishi na Mtangazaji wa Radio Vatican, Roma, nchini Italia Hakika Padre Mjigwa katika miaka hii amepitia changamoto nyingi, yeye mwenyewe anasema kati ya changamoto hizo ni kutetereka kwa afya ambako aligundulika kuwa alikuwa na tatizo katika utumbo mnene na hivyo ilipelekea kufanyiwa operesheni ya dharura mwaka 2011 na aliweza kupona huku madaktari wakiwa wanashangaa kwa sababu ni tatizo kubwa lililokuwa linapelekea kifo. Baba Mjigwa alipoulizwa nini ushauri anaoweza kutoa hasa katika siku hii muhimu katika maisha na utume wake alisema: “pale unapoitwa jitoe kwa akili yako, kwa moyo wako wote na ujue ni hapo hapo tu Mwenyezi Mungu amekupangia na kama atakuhamisha umshukuru”. Aliongezea “katika maisha na utume wa wito wa aina yeyote ile jitahidi kuwekeza kwa watu, jitahidi kujenga mahusiano na mafungamano mema na watu na hao watakusaidia katika maisha na utume wako, na kamwe hutatindikiwa na lolote.” Tunaposherehekea na kumpongeza Padre Richard Mjigwa, C.PP.S., tunaalikwa kila mmoja wetu kumwombea ili aweze kuwa mwaminifu na mwadilifu katika wito, maisha na utume wake.