Ask.Mkuu Caccia:Bara la Afrika lina utajiri wa rasilimali watu,asili&urithi wa utamaduni
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Mwakilishi wa Kudumu wa Vatican katika Umoja wa Mataifa alitoa tamko katika Baraza la Usalama kuhusu hatua za kuimarisha jukumu la mataifa ya Afrika katika kushughulikia changamoto za usalama na maendeleo duniani mjini New York, Marekani, Alhamisi tarehe 23 Mei 2024. Askofu Mkuu Gabriele Cacca akianza alisekuwa “Bara la Afrika limejaliwa utajiri wa rasilimali watu na asili, pamoja na urithi wa kiutamaduni. Hata hivyo, linakabiliwa na changamoto nyingi, ikiwa ni pamoja na migogoro, ugaidi, athari za mabadiliko ya tabianchi, na mapambano yanayoendelea ya maendeleo ya kiuchumi na kutokomeza umaskini. Changamoto hizi zimesababisha kukosekana kwa utulivu na kuzorotesha maendeleo katika nchi nyingi za Afrika, na kusababisha mateso mengi kwa wengi. Katika muktadha huu, Ujumbe wake ulitaka kusisitiza mambo mawili muhimu kuhusu “uimarishaji wa nafasi ya Mataifa ya Afrika katika kushughulikia changamoto zao za usalama na maendeleo.”
Umuhimu wa kutambua maendeleo makubwa yaliyofanywa na mataifa ya Afrika
Kwanza, ni muhimu kutambua maendeleo makubwa yaliyofanywa na Mataifa ya Afrika katika kuimarisha ushirikiano wao ili kukabiliana na baadhi ya changamoto kubwa zaidi za bara. Kwa mfano, Ujumbe wake ulikaribisha kazi ya kutekeleza mpango wa Umoja wa Afrika wa “Kunyamazisha Bunduki” kwa 2030, ambao unaweza kuwa muhimu katika kukomesha kuenea kwa vurugu kupitia biashara haramu ya silaha na makundi ya kigaidi na yenye silaha, ambayo yanapata faida za kifedha kwa gharama ya walio hatarini zaidi.
Kuna nia mbaya ya baadhi ya nchi kunyonya maliasili na watu barani Afrika
Pili, Askofu Mkuu Caccia alibanisha kuwa “nia mbaya ya baadhi ya Nchi kunyonya maliasili na watu wa bara la Afrika inahusu sana. Wimbi jipya la ukoloni linashuhudiwa hivi sasa, ambalo haliheshimu utu wa asili wa binadamu wote, linadhoofisha manufaa ya wote na kutishia juhudi za kutokomeza umaskini. Kwa hiyo ni muhimu sana kwamba jumuiya ya kimataifa ichukue hatua kwa pamoja ili kuhakikisha kwamba wanaume, wanawake na watoto kote barani Afrika wanakuwa “wakala wenye heshima wa hatima yao wenyewe”. Ni muhimu kwamba juhudi zifanywe kuunga mkono, badala ya kulazimisha, na kuipatia Afrika uhuru wa kufuata sera za maendeleo fungamani ya binadamu. Askofu Mkuu Caccia aidha aliomba aruhusiwe kuhitimisha kwa maneno ya kutia moyo kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko, “Afrika, tabasamu na matumaini ya dunia, ihesabiwe zaidi! Na izungumzwe mara nyingi zaidi, na iwe na uzito na heshima kubwa miongoni mwa mataifa!