Askofu mkuu Flavio Pace, Katibu Mkuu wa Baraza la Kipapa la Uhamashaji Umoja wa Wakristo
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Askofu mkuu Flavio Pace, Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa la Uhamasishaji wa Umoja wa Wakristo alizaliwa tarehe 29 Julai 1977 huko Monza, Jimbo kuu la Milano, Italia. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kipadre tarehe 29 Septemba 2001 akapewa Daraja Takatifu ya Ushemasi na hatimaye, tarehe 8 Juni 2002 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre. Tarehe 3 Februari 2020 Baba Mtakatifu Francisko akamteuwa kuwa Katibu mkuu Msaidizi wa Baraza la Kipapa la Kuhamasisha Umoja wa Wakristo. Ilipogota tarehe 23 Februari 2024 Baba Mtakatifu Francisko akampandisha hadhi na kuwa ni Askofu mkuu na Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa la Kuhamasisha Umoja wa Wakristo Monsinyo Flavio Pace, amewekwa wakfu kuwa Askofu mkuu tarehe 4 Mei 2024, huko Jimbo kuu la Milano na Askofu mkuu Mario Enrico Delpin wa Jimbo kuu la Milano, Italia akisaidiana na Kardinali Leonardo Sandri, Mwenyekiti Mstaafu wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Makanisa ya Mashariki na Dekano wa Baraza la Makardinali pamoja na Kardinali Kurt Koch, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uhamasishaji wa Umoja wa Wakristo.
Itakumbukwa kwamba, uinjilishaji mpya unaotekelezwa na Mama Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo unajikita katika mchakato wa: Majadiliano ya kiekumene na kidini ili kujenga na kudumisha: utu, heshima, haki msingi za binadamu, ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu katika ujumla wao. Baba Mtakatifu Francisko anakazia uekumene wa: damu, maisha ya kiroho, sala na huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Ikumbukwe kwamba, uekumene wa utakatifu wa maisha unafumbatwa katika toba na wongofu wa ndani; kwa kujikana na kujivika fadhila ya unyenyekevu; moyo wa ukarimu na udugu; upole, uvumilivu na kutumikia bila ya kujibakiza. Wakristo wanakumbushwa kwamba, kadiri wanavyojitahidi kuishi maisha matakatifu mintarafu Injili, ni kwa kadiri ile ile wataweza kuhamasishana kutekeleza mchakato wa ujenzi wa umoja wa Wakristo na udugu kati yao. Uekumene wa damu unajikita katika ushuhuda wa imani kwa Kristo Yesu na Kanisa lake.
Askofu mkuu Flavio Pace, Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa la Uhamasishaji wa Umoja wa Wakristo katika maisha na utume wake anaongozwa na kauli mbiu “Fove precantes Trinitas” yaani “Himiza Utatu Katika Sala.” Askofu mkuu Mario Enrico Delpin wa Jimbo kuu la Milano, katika mahubiri yake amemwihimiza Askofu mkuu Flavio Pace kutangaza na kushuhudia ukweli kwa njia ya maisha sala, kwa sababu ulimwengu mamboleo unawahitaji watu wanaokita maisha yao katika sala, inayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Awe ni mtu wa diplomasia kwa kuheshimu na kuthamini Mapokeo ya Makanisa. Kama shuhuda wa ukweli, ajiaminishe chini ya Kristo Yesu na Roho Mtakatifu anayekuja kuwasaidia na kuwanyanyua katika umaskini na udhaifu wao wa kibinadamu. Askofu mkuu Mario Delpin amekazia pia umuhimu wa maisha ya sala ya Kanisa na tafakari ya kina ya Neno la Mungu, ili kukoleza mchakato wa majadiliano ya kiekumene kati ya Makanisa, ili kusimika imani na matumaini ya Kanisa la Kristo Yesu; Upatanisho na amani ya kweli. Kama Askofu awe makini na Sheria za Kanisa, Mapokeo, lakini zaidi ya yote awe ni mtu wa Sala, ili kukoleza umoja wa Kanisa sanjari na kuombea amani.
Kwa upande wake, Askofu mkuu Flavio Pace, Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa la Uhamasishaji wa Umoja wa Wakristo amemshukuru Mungu kwa zawadi na wito wa Daraja ya Uaskofu pamoja na wale wote waliomsaidia katika maisha na utume wake kama Padre na sasa kama Askofu, ili aendelee kuwa kati ya Kondoo wake, Mchungaji mwema anayeshirikishana maisha na Kondoo wake, anayewalinda na kuwachunga; tayari kuganga na kuponya madonda yao.