Askofu Msaidizi Godfrey J. Mwasekaga & Jubilei ya Miaka 125 Uinjilishaji Jimbo kuu la Mbeya
Na Celina Munde, -Jimbo Katoliki la Mbeya,
Askofu ana wajibu na dhamana ya kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu kwa kutambua kwamba, Kristo Yesu ndiye mchungaji mkuu anayeunda na kuliongoza Kanisa; Kristo Yesu ndiye nguzo na mhimili mkuu wa Kanisa lake. Kumbe, ni wajibu wa Maaskofu kuhakikisha kwamba, wanatekeleza dhamana na wajibu wao kadiri ya mipango ya Kristo mchungaji mwema. Maaskofu wanapaswa kuwa ni wachungaji wema, Sakramenti ya wokovu na kielelezo cha ukaribu wa Mungu kwa waja wake. Uwepo wa karibu wa Mungu ni chemchemi ya utume wa Askofu kama unavyofunuliwa katika Fumbo la Umwilisho, kielelezo makini cha ukaribu wa Mungu kwa waja wake. Ili kuonja ukaribu wa Mungu kuna umuhimu wa kupata mang’amuzi ya wema, huruma na upendo kwa waja wake. Maaskofu wajenge utamaduni wa kusali na kutafakari mbele ya Kristo Yesu, ili kuwawezesha kuishi kati ya watu wa Mungu. Katika shida, magumu na changamoto za maisha na utume wa Kiaskofu, Baba Mtakatifu Francisko anawataka Maaskofu kukimbilia katika sala na tafakari, ili kujenga tena: imani na matumaini mapya, kwa kumtegemea na kuendelea kujiaminisha kwa Kristo Yesu. Ukaribu wa Mungu unajionesha kati ya watu wake kwa njia ya utambulisho wa Maaskofu, wanaojisadaka bila ya kujibakiza kama sadaka safi inayotolewa Altareni. Maaskofu ni mkate unaomegwa kwa ajili ya maisha ya ulimwengu. Kristo Yesu anataka kuwa kati pamoja na watu wake kwa njia ya Maaskofu. Ukaribu wa Mungu unajionesha katika Neno na maadhimisho ya Mafumbo mbalimbali ya Kanisa. Lakini zaidi, kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko, kwa kupenda bila kujibakiza pamoja na kuendelea kujizamisha katika huruma na upendo wa Mungu.
Ibada ya kuwekwa wakfu kwa Askofu msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Mbeya Mshashamu Godfrey Jackson Mwasekaga na Jubilei ya Miaka 125 ya Uinjilishaji jimbo kuu la Mbeya, iliyofanyika katika uwanja wa Sokoine jijini Mbeya imeongozwa na Kardinali Polycap Pengo Askofu Mkuu Mstaafu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam Dominika tarehe 26 Mei 2024. Askofu mkuu Gervas John Mwasikwabhila Nyaisonga wa Jimbo kuu la Mbeya, ambaye pia ni Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, TEC., ameiomba Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mambo sita ikiwemo: Ujenzi wa barabara ya kiwango cha lami kutoka Mbeya itakayounganisha Mikoa ya Tabora na Singida, Ili kurahisisha mchakato wa maendeleo endelevu katika Mikoa hiyo. Wito huo ameutoa wakati wa adhimisho la Misa takatifu ya kumweka wakfu Askofu Msaidizi Godfrey Jackson Mwasekaga, Sherehe iliyoenda sanjari na Maadhimisho ya Jubilee ya miaka 125 ya Uinjilishaji Jimboni Mbeya iliyofanyika tarehe 26 Mei,2024. Kwa kuwa Kanisa linatambua juhudi mbalimbali za Serikali ya Tanzania katika kutatua: matatizo na changamoto za wananchi ikiwemo maji, umeme, kujenga vituo vya afya, na kwamba wanafurahia sana pia suala la serikali kuendelea kupinga vitendo vya ndoa za jinsia moja vinavyoharibu mila, desturi njama na utamaduni wa mtanzania.
Askofu mkuu Nyaisonga ameyataja maeneo ambayo ni changamoto ili serikali iwasaidie, miongoni mwake ni kujenga barabara kwa kiwango cha lami, kuunganisha Mikoa ya Tabora na Singida, kujenga madaraja mkoa wa Songwe ilikusaidia wananchi wanaopata taabu kuvuka hasa Mkurwe na maeneo mengine ambako huvuka kwa mashaka sana kwa kuhofia kuliwa na mamba, kwani maeneo hayo tangu Mwezi Februari, 1979 hakujawahi kufanyiwa ukarabati kutokana na uharibifu wa mvua, uharakishwaji wa mradi wa umeme, Mkurwe na kupatiwa nafasi ya kusikilizwa watakapo omba kusaidiwa katika kutatua changamoto za Afya na Elimu kwa kuwa Kanisa hutoa huduma ya elimu na wala sio biashara ikiwezekana kuondoa vikwazo Ili hatimaye, Kanisa pia lifikie hatua ya kutoa elimu bure. Alisema Kanisa linapata uhalali na maendeleo katika kuwahudumia watu. Askofu mkuu Nyaisonga amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt., Samia Suluhu Hassan, kwa kazi nzuri ya Uongozi wake na kumtuma mwakilishi katika tukio la Jubilee ya miaka 125 ya Uinjilishaji Jimboni Mbeya pamoja na kuwekwa wakfu kwa Askofu Msaidizi wa Jimbo kuu la Mbeya. Alisema Kanisa Katoliki Mbeya limeendelea kuimarika katika imani kutokana na michango mbalimbali inayotolewa na waamini wakatoliki na wasio wakatoliki ikiwemo Serikali katika kutatua: matatizo na changamoto mbalimbali wanazokumbana nazo kama sehemu ya Uinjilishaji wa kina, unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili.
Wakati huo huo, Askofu mkuu Angelo Accattino, Balozi wa Vatican nchini Tanzania amewasilisha salam, pongezi na matashi mema kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko kwa Askofu msaidizi Godfrey Jackson Mwasekaga, kwa kuingia pia katika urika wa Maaskofu kwenye Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania. Lakini amemtaka kuendelea kutekeleza majukumu yake ya utume kwa kushirikiana na Askofu wake mkuu na waamini kwa lengo la kuwafundisha, kuwatakatifunza, kuwaongoza pamoja na kuhubiri injili kwa watu wote wa Mataifa. Aidha ameishukuru serikali kwa ushirikiano na Kanisa Katoliki kila mara na kwamba, hiyo ni ishara nzuri kwa Taifa la Tanzania amewapongeza pia watu wa Mungu Jimbo kuu la Mbeya na kuwataka waendelee na moyo wa upendo na mshikamano huku wakiendelea kufanya kazi kwa bidii, juhudi na maarifa Ili kulijenga Taifa, wao binafsi na Kanisa kwa ujumla ikiwemo kudumisha Amani, umoja na mshikamano miongoni mwa watu wa dini mbalimbali.
Naye Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema, Serikali itaendelea kuthamini, kutambua na kuheshimu mchango wa madhehebu ya dini katika kuchochea maendeleo katika sekta mbalimbali nchini Tanzania. Amesema kuwa Serikali imekuwa ikishirikiana na Sekta binafsi zikiwemo Taasisi za dini katika kutoa huduma kwa wananchi na kuleta maendeleo ya Taifa kwa kuwa maendeleo ya nchi hayawezi kuimarika bila ushirikiano na ushirikishwaji wa kila mtu. Amesema hayo Dominika tarehe Mei 26, 2024 alipomwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye ibada ya kuwekwa wakfu kwa Askofu msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Mbeya Mshashamu Godfrey Jackson Mwasekaga na Jubilei ya Miaka 125 ya Uinjilishaji jimbo kuu la Mbeya, iliyofanyika katika uwanja wa Sokoine jijini Mbeya. Ibada hiyo imeongozwa na Mwadhama Kardinali Polycap Pengo Askofu Mkuu Mstaafu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam. “Ni ukweli usiopingika uwepo wa Taasisi za Dini unasaidia katika kuchangia juhudi za Serikali katika kutoa huduma mbalimbali kama vile elimu, afya, kilimo, maji na fedha, huduma ambazo Serikali peke yake isingeweza kuzifikisha kwa wananchi mara moja.” Aidha, Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inalipongeza Kanisa Katoliki kwa hatua mbalimbali zinazochukuliwa katika kuunga mkono juhudi za Serikali kwenye kuimarisha utoaji na upatikanaji wa huduma bora za jamii kwa Watanzania.
“Hapa Mbeya na Mkoani Songwe ninafahamu kuwa Jimbo Kuu Katoliki la Mbeya linashirikiana na Serikali katika kutoa huduma afya katika maeneo 15 ya kutolea huduma ikiwemo Hospitali mbili za Igogwe iliyoko Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe na Mwambani iliyoko Halmashauri ya Wilaya ya Songwe, Vituo vya Afya vitatu (viwili Mkoa wa Mbeya na kimoja Mkoa wa Songwe); Zahanati 10 (7 zipo Mkoa wa Mbeya na 3 Mkoa wa Songwe)” Pia, amewakikishia viongozi wa dini kuwa Serikali iko tayari kushirikiana na madhehebu yote ya dini pamoja na wadau wote katika kuhakikisha huduma bora za afya na elimu nchini Tanzania zinapatikana. Kadhalika Waziri Mkuu ametoa wito kwa viongozi wa dini waendelee kuweka msisitizo katika masuala ya kuwekeza katika vijana na kukemea vitendo vyote hatarishi kwa vijana mfano matumizi ya dawa za kulevya, wizi, ubakaji na kadhalika. Amesema Serikali inatambua na kuthamini kazi na majukumu makubwa ya viongozi wa madhehebu ya dini ya kuwaongoza watu kiroho kwa kuwapa mafundisho, kutoa ushauri na kuwajenga kiimani.