Askofu Peter Munguti Makau, I.M.C. Jimbo Katoliki la Isiolo, Kenya
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko Jumamosi tarehe 4 Mei 2024 amemteua Mheshimiwa sana Padre Peter Munguti Makau, I.M.C., Mmisionari wa Shirika la Consolata kuwa Askofu mwandamizi mwenye haki ya kurithi Jimbo Katoliki la Isiolo, lililoko nchini Kenya. Hadi kuteuliwa kwake, Askofu mteule Peter Munguti Makau, I.M.C., alikuwa ni Mkuu wa Shirika la Waconsolata nchini Kenya na Uganda. Itakumbukwa kwamba, Askofu mteule Peter Munguti Makau, I.M.C., alizaliwa tarehe 6 Mei 1975 Jimbo kuu la Nairobi, Kenya. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kitawa na Kipadre, tarehe 5 Desemba 2003 akaweka nadhiri za daima na hatimaye tarehe 20 Novemba 2004 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre, Jimbo Katoliki la Machakos.
Baada ya Upadrisho alijiendeleza na masomo ya juu na hatimaye akajipatia Diploma katika Sheria za Kanisa kutoka Chuo Kikuu cha “Universidad Monteávila" huko Caracas, kilichoko nchini Venezuela. Katika maisha na utume wake, amewahi kuwa Paroko wa Parokia ya Carapita, Jimbo kuu la Caracas nchini Venezuela kuanzia mwaka 2006 hadi mwaka 2014. Baadaye akateuliwa kuwa ni Mwakilishi wa Mkuu wa Shirika la Waconsolata nchini Venezuela kwa vipindi viwili vya uongozi yaani kati yam waka 2014 hadi mwaka 2019. Kuanzia mwaka 2019 hadi kuteuliwa kwake alikua ni Mkuu wa Kanda ya Wamisionari wa Consolata Kenya na Uganda.