Tafuta

Mhe. Hassan Iddi Mwamweta amesema, amani na utulivu ni vinasaba na utambulisho wa Tanzania sehemu mbalimbali za dunia. Mhe. Hassan Iddi Mwamweta amesema, amani na utulivu ni vinasaba na utambulisho wa Tanzania sehemu mbalimbali za dunia.  

Balozi Hassan I. Mwamweta: Amani Na Utulivu Ni Vinasaba na Utambulisho wa Tanzania!

Mhe. Hassan Iddi Mwamweta, Balozi wa Tanzania mjini Vatican amesema, amani na utulivu ni vinasaba na utambulisho wa Tanzania sehemu mbalimbali za dunia. Hii ni tunu adhimu inayopaswa kulindwa na kutunzwa kama mboni ya jicho! Amewaalika watanzania kuombea uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka 2024 na uchaguzi Mkuu wa Rais na Wabunge mwaka 2025. Kanuni msingi ni kusikiliza kwa makini, kujadiliana na kwamba, wao ni daraja na kiungo muhimu sana!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Jumuiya ya Watanzania Wakatoliki Italia, Jumamosi, tarehe 25 Mei 2024 wamekutana na kuadhimisha Ibada ya Misa takatifu kwa ajili ya kumshukuru Mungu kwa kuhitimisha Mwaka wa Masomo 2023-2024. Ilikuwa ni nafasi ya kuagana na wanafunzi waliohitimu masomo yao, na sasa wanarejea nchini Tanzania kuendelea na maisha pamoja na utume kwa watu wa Mungu nchini Tanzania. Imekuwa ni nafsi ya kuwachagua viongozi wapya wa Umoja watakaoiongoza Jumuiya ya Watanzania Wakatoliki Italia kwa mwaka 2024-2025. Imekuwa pia ni nafasi ya kuwapongeza wale watakaopewa Madaraja mbalimbali katika kipindi hiki cha mwaka 2024 na hatimaye, kumshukuru Mungu kwa Jubilei ya Miaka 25 ya Daraja Takatifu ya Upadre: Kwa Padre Paulo Kaigarula, Mkarmeli wa kwanza Mtanzania kupewa Daraja Takatifu ya Upadre pamoja na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. Mmisionari wa Shirika la Damu Azizi ya Yesu. Ilikuwa ni Siku maalum ya kuwakumbuka na kuwaombea viongozi wa Tanzania pamoja na wale wote waliotangulia mbele ya haki wakiwa na tumaini la maisha na ufufuko wa wafu! Tukio hili limehudhuriwa na Balozi wa Tanzania nchini Ujerumani, Mhe. Hassan Iddi Mwamweta ambaye pia ni Balozi wa Tanzania mjini Vatican pamoja na Mheshimiwa Mahmoud Thabit Kombo, Balozi wa Tanzania nchini Italia pamoja na wafanyakazi wa Ubalozi wa Tanzania nchini Italia. Katika mahubiri yake, Padre Richard Mjigwa, C.PP.S., aliwakumbusha watu wa Mungu kwamba, Mapadre na Watawa ni Mashuhuda wa ufunuo wa huruma ya Mungu. Wanaitwa na kutumwa kujenga na kuimarisha mahusiano na mafungamano ya kijamii, kwa kujenga utamaduni wa kusikiliza kama sehemu ya mchakato wa ujenzi wa Kanisa la Kisinodi.

Balozi Hassan Iddi Mwamweta akiwa na Jumuiya ya Watanzania Wakatoliki Italia
Balozi Hassan Iddi Mwamweta akiwa na Jumuiya ya Watanzania Wakatoliki Italia

Mhe. Hassan Iddi Mwamweta ambaye pia ni Balozi wa Tanzania mjini Vatican mwenye makazi yake mjini Berlin nchini Ujerumani, akizungumza na Jumuiya ya Watanzania Wakatoliki Italia, amesema, anatarajia kuwasilisha hati zake za utambulisho kwa Baba Mtakatifu Francisko tarehe 8 Juni 2024. Amesema, amani na utulivu ni vinasaba na utambulisho wa Tanzania sehemu mbalimbali za dunia. Hii ni tunu adhimu inayopaswa kulindwa na kutunzwa kama mboni ya jicho! Amewaalika watanzania kuombea uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka 2024 na uchaguzi Mkuu wa Rais na Wabunge mwaka 2025. Amesema, kanuni na taratibu zinazoongoza utendaji wa kazi katika Ubalozi wa Tanzania mjini Vatican ni kusikiliza, kujadiliana na kwamba, wao ni daraja kati ya watanzania, Serikali na Vatican katika ujumla wake. Wanaongozwa na dhana ya kusikiliza na kuwahudumia watanzania. Kumbe, watanzania wenye mawazo na ushauri wajisikie kuwa huru kuwasiliana na Ubalozi.

Balozi Hassan Iddi Mwamweta akisalimiana na Padre R. Mjigwa, C.PP.S.
Balozi Hassan Iddi Mwamweta akisalimiana na Padre R. Mjigwa, C.PP.S.

Mhe. Hassan Iddi Mwamweta amewataka watanzania kujenga na kudumisha utamaduni wa: kupendana, kuheshimiana, kusaidiana, kushirikiana na kushauriana kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watanzania wengi. Faraja inapatikana kwa kuaminiana na kusikilizana na kwamba, hii ni furs makini ya pande zote mbili kujifunza. Watanzania wajenge pia utamaduni wa kuheshimu mila, desturi na tamaduni njema; uzalendo; kuipenda na kuithamini nchi yao; kuheshimu na kufuata sheria, kanuni na taratibu za nchi mwenyeji. Ameishukuru na kuipongeza Jumuiya ya Watanzania Wakatoliki Italia kwa hafla ya kuagana, uchaguzi uliofanyika katika misingi ya haki, ukweli na uwazi; na kwa furaha iliyooneshwa kwa wale wanaomaliza muda wao wa uongozi na wale ambao kwa sasa wameshika hatamu za uongozi.

Jumuiya ya Watanzania Wakatoliki Italia 25 Mei 2024
Jumuiya ya Watanzania Wakatoliki Italia 25 Mei 2024

Watanzania kamwe wasielemewe na ubinafsi pamoja na uchoyo! Kwa hakika taasisi za kidini zinahitaji pia kukuza na kudumisha demokrasia ya uongozi kwa sababu kila kiongozi ana mawazo, maono na uwezo wa kuongoza ni hutofautiana. Amesema, uongozi bora unasimikwa katika fadhila ya unyenyekevu, ili kurekebisha: Matatizo, changamoto na fursa mbalimbali, yote haya yanahitaji ujenzi wa moyo wa ushirikiano na mafungamano ya kijamii. Ubalozi unaandaa tukio kubwa ili kuwapatia watanzania wanaoishi diaspora kuwa kupata huduma muhimu kwa kipindi kifupi sana yaani: Hati za kusafiria, Pasi, Vitambulisho vya NIDA. Mwishoni amemshukuru Mheshimiwa Mahmoud Thabit Kombo, Balozi wa Tanzania nchini Italia pamoja na wafanyakazi wa Ubalozi wa Tanzania nchini Italia kwa kutoa huduma muhimu kwa watanzania.

Balozi Hasan Mwamweta
28 May 2024, 16:53