Tafuta

. Mhe. Mahmoud Thabit Kombo, Balozi wa Tanzania nchini Italia, amewataka watanzania kuchangamkia fursa za masomo zinazotolewa na Taasisi mbalimbali nchini Italia. . Mhe. Mahmoud Thabit Kombo, Balozi wa Tanzania nchini Italia, amewataka watanzania kuchangamkia fursa za masomo zinazotolewa na Taasisi mbalimbali nchini Italia. 

Balozi Mahmoud Thabiti Kombo: Changamkieni Fursa za Masomo Nchini Italia

Balozi Mahmoud Thabiti Kombo anatambua kwamba, kama Mapadre wanayo dhamana ya kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu. Lakini uongozi wa maisha ya kiroho una mchango mkubwa katika kukoleza: ustawi, maendeleo na mafao ya wengi katika masuala ya uchumi, haki, amani na utulivu wa nchi. Serikali inatambua na kuthamini mchango wa Kanisa Katoliki katika maendeleo ya watanzania katika sekta ya elimu, afya na ustawi wa jamii.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Jumuiya ya Watanzania Wakatoliki Italia, Jumamosi, tarehe 25 Mei 2024 wamekutana na kuadhimisha Ibada ya Misa takatifu kwa ajili ya kumshukuru Mungu kwa kuhitimisha Mwaka wa Masomo 2023-2024. Ilikuwa ni nafasi ya kuagana na wanafunzi waliohitimu masomo yao, na sasa wanarejea nchini Tanzania kuendelea na maisha pamoja na utume kwa watu wa Mungu nchini Tanzania. Imekuwa ni nafsi ya kuwachagua viongozi wapya wa Umoja watakaoiongoza Jumuiya ya Watanzania Wakatoliki Italia kwa mwaka 2024-2025. Imekuwa pia ni nafasi ya kuwapongeza wale watakaopewa Madaraja mbalimbali katika kipindi hiki cha mwaka 2024 na hatimaye, kumshukuru Mungu kwa Jubilei ya Miaka 25 ya Daraja Takatifu ya Upadre: Kwa Padre Paulo Kaigarula, Mkarmeli wa kwanza Mtanzania kupewa Daraja Takatifu ya Upadre pamoja na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. Mmisionari wa Shirika la Damu Azizi ya Yesu. Ilikuwa ni Siku maalum ya kuwakumbuka na kuwaombea viongozi wa Tanzania pamoja na wale wote waliotangulia mbele ya haki wakiwa na tumaini la maisha na ufufuko wa wafu! Tukio hili limehudhuriwa na Balozi wa Tanzania nchini Ujerumani, Mhe. Hassan Iddi Mwamweta ambaye pia ni Balozi wa Tanzania mjini Vatican pamoja na Mheshimiwa Mahmoud Thabit Kombo, Balozi wa Tanzania nchini Italia pamoja na wafanyakazi wa Ubalozi wa Tanzania nchini Italia. Katika mahubiri yake, Padre Richard Mjigwa, C.PP.S., aliwakumbusha watu wa Mungu kwamba, Mapadre na Watawa ni Mashuhuda wa ufunuo wa huruma ya Mungu. Wanaitwa na kutumwa kujenga na kuimarisha mahusiano na mafungamano ya kijamii, kwa kujenga utamaduni wa kusikiliza kama sehemu ya mchakato wa ujenzi wa Kanisa la Kisinodi.

Balozi Kombo na Balozi Hassan wakiwa na mapadre na wafanyakazi wa Ubalozi
Balozi Kombo na Balozi Hassan wakiwa na mapadre na wafanyakazi wa Ubalozi

Mhe. Hassan Iddi Mwamweta ambaye pia ni Balozi wa Tanzania mjini Vatican mwenye makazi yake mjini Berlin nchini Ujerumani, akizungumza na Jumuiya ya Watanzania Wakatoliki Italia, amesema, anatarajia kuwasilisha hati zake za utambulisho kwa Baba Mtakatifu Francisko tarehe 8 Juni 2024. Amesema, amani na utulivu ni vinasaba na utambulisho wa Tanzania sehemu mbalimbali za dunia. Hii ni tunu adhimu inayopaswa kulindwa na kutunzwa kama mboni ya jicho! Amewaalika watanzania kuombea uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka 2024 na uchaguzi Mkuu wa Rais na Wabunge mwaka 2025. Amesema, kanuni na taratibu zinazoongoza utendaji wa kazi katika Ubalozi wa Tanzania mjini Vatican ni kusikiliza, kujadiliana na kwamba, wao ni daraja kati ya watanzania, Serikali na Vatican katika ujumla wake. Wanaongozwa na dhana ya kusikiliza na kuwahudumia watanzania. Kumbe, watanzania wenye mawazo na ushauri wajisikie kuwa huru kuwasiliana na Ubalozi.

Balozi Mahmoud Thabit Kombo: Wekezeni kwenye elimu
Balozi Mahmoud Thabit Kombo: Wekezeni kwenye elimu

Kwa upande wake Mhe. Mahmoud Thabit Kombo, Balozi wa Tanzania nchini Italia, amewataka watanzania kuchangamkia fursa za masomo zinazotolewa na Taasisi mbalimbali nchini Italia, ili kuwaandaa viongozi watakaojisadaka kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watanzania. Anatambua kwamba, kama Mapadre wanayo dhamana ya kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu. Lakini uongozi wa maisha ya kiroho una mchango mkubwa katika kukoleza: ustawi, maendeleo na mafao ya wengi katika masuala ya uchumi, haki, amani na utulivu wa nchi. Serikali inatambua na kuthamini mchango wa Kanisa Katoliki katika maendeleo ya watanzania katika sekta ya elimu, afya na ustawi wa jamii. Ili kuweza kufikia hapa kuna haja ya kupambana na “ukweli mchungu” unaokita mizizi yake katika uchoyo na uroho, mambo yanayosababisha athari za mabadiliko ya tabianchi na watu kushindwa kuwashirikisha wengine kuchangia fursa za masomo nchini Italia.

Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania alipokutana na Papa Francisko.
Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania alipokutana na Papa Francisko.

Tangu mwanzo wa mchakato wa uinjilishaji nchini Tanzania, Kanisa limekuwa mstari wa mbele katika kuchangia ustawi, maendeleo na mafao ya wengi hususan katika nyanja za elimu, afya, maendeleo na ustawi wa jamii, bila kusahau huduma ya maisha ya kiroho kwa watu wa Mungu nchini Tanzania na katika mchakato wa kudumisha amani ulimwenguni. Takwimu zinaonesha kwamba, Kanisa Katoliki nchini Tanzania hadi kufikia mwaka 2024 linamiliki na kuendesha shule za awali 240, shule za msingi 147, shule za sekondari 244, vyuo vya ufundi, vyuo vikuu 5; taasisi za elimu ya juu 5 na vituo vya vyuo vikuu 2 ambavyo viko chini ya Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agostino, SAUT. Vyuo vyote hivi vina jumla ya wanafunzi 31, 000 pamoja na taasisi za afya ni 473, lengo likiwa ni kumhudumia mtu mzima: kiroho na kimwili.

Balozi Kombo
29 May 2024, 16:49