Tafuta

Jumuiya ya Watanzania Wakatoliki Italia, Jumamosi, tarehe 25 Mei 2024 wamekutana na kuadhimisha Ibada ya Misa takatifu kwa ajili ya kumshukuru Mungu kwa kuhitimisha Mwaka wa Masomo 2023-2024. Jumuiya ya Watanzania Wakatoliki Italia, Jumamosi, tarehe 25 Mei 2024 wamekutana na kuadhimisha Ibada ya Misa takatifu kwa ajili ya kumshukuru Mungu kwa kuhitimisha Mwaka wa Masomo 2023-2024.  

Mapadre Na Watawa Ni Mashuhuda wa Ufunuo wa Upendo na Huruma ya Mungu Kwa Watu Wake!

Jumuiya ya Watanzania Wakatoliki Italia, Jumamosi, tarehe 25 Mei 2024 imekutana na kuadhimisha Ibada ya Misa takatifu kwa ajili ya kumshukuru Mungu, Ilikuwa ni nafasi ya kuagana na wanafunzi waliohitimu masomo yao, na fursa ya kuwachagua viongozi wapya wa Umoja watakaoiongoza Jumuiya ya Watanzania Wakatoliki Italia kwa mwaka 2024-2025. Imekuwa pia ni nafasi ya kuwapongeza wale watakaopewa Madaraja mbalimbali katika kipindi hiki cha mwaka 2024.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Jumuiya ya Watanzania Wakatoliki Italia, Jumamosi, tarehe 25 Mei 2024 wamekutana na kuadhimisha Ibada ya Misa takatifu kwa ajili ya kumshukuru Mungu kwa kuhitimisha Mwaka wa Masomo 2023-2024. Ilikuwa ni nafasi ya kuagana na wanafunzi waliohitimu masomo yao, na sasa wanarejea nchini Tanzania kuendelea na maisha pamoja na utume kwa watu wa Mungu nchini Tanzania. Imekuwa ni nafsi ya kuwachagua viongozi wapya wa Umoja watakaoiongoza Jumuiya ya Watanzania Wakatoliki Italia kwa mwaka 2024-2025. Imekuwa pia ni nafasi ya kuwapongeza wale watakaopewa Madaraja mbalimbali katika kipindi hiki cha mwaka 2024 na hatimaye, kumshukuru Mungu kwa Jubilei ya Miaka 25 ya Daraja Takatifu ya Upadre: Kwa Padre Paulo Kaigarula, Mkarmeli wa kwanza Mtanzania kupewa Daraja Takatifu ya Upadre pamoja na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. Mmisionari wa Shirika la Damu Azizi ya Yesu. Ilikuwa ni Siku maalum ya kuwakumbuka na kuwaombea viongozi wa Tanzania pamoja na wale wote waliotangulia mbele ya haki wakiwa na tumaini la maisha na ufufuko wa wafu! Tukio hili limehudhuriwa na Balozi wa Tanzania nchini Ujerumani, Mhe. Hassan Iddi Mwamweta ambaye pia ni Balozi wa Tanzania mjini Vatican pamoja na Mheshimiwa Mahmoud Thabit Kombo, Balozi wa Tanzania nchini Italia pamoja na wafanyakazi wa Ubalozi wa Tanzania nchini Italia. Viongozi waliochaguliwa ni: Padre Joseph Herman Luwela, Mwenyekiti, Padre Victor Basilius, Katibu, Sr. Salome Sheshe, Mhazini, Pd. Revocatus Mwemezi: Liturujia pamoja na Padre Simeone Kiiza Mkutubi. Katika mahubiri yake, Padre Richard Mjigwa, aliwakumbusha watu wa Mungu kwamba, Mapadre na Watawa ni Mashuhuda wa ufunuo wa huruma ya Mungu. Wanaitwa na kutumwa kujenga na kuimarisha mahusiano na mafungamano ya kijamii, kwa kujenga utamaduni wa kusikiliza kama sehemu ya mchakato wa ujenzi wa Kanisa la Kisinodi.

Watanzania Wakatoliki Italia baada ya Misa ya Shukrani Kwa Mwaka 2023/24
Watanzania Wakatoliki Italia baada ya Misa ya Shukrani Kwa Mwaka 2023/24

Baba Mtakatifu Francisko kwa njia ya maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro amekuwa ni changamoto kubwa ya kuangalia tena mchakato wa malezi na majiundo ya maisha, wito na utume wa kipadre na maisha ya kuwekwa wakfu ndani ya Kanisa, kwa kuendelea kusoma alama za nyakati, changamoto iliyotolewa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican. Hii inatokana na ukweli kwamba, mapadre na watawa si watu wa mshahara, bali ni wachungaji wa familia ya Mungu, wanaopaswa kwa namna ya pekee, kuwa ni watu wasikivu, wenye huruma na upendo kama ilivyokuwa kwa Kristo Yesu katika maisha na utume wake. Yesu aliwaonea watu huruma, akawasikiliza kwa makini, akawaganga na kuwaponya, akawasamehe dhambi zao na kuwapatia tena furaha ya kuendelea kuishi kwa imani na matumaini, kwani walikuwa wameonja na kukutana na Uso wa upendo na huruma ya Mungu katika safari ya maisha yao! Kumbe, majiundo na malezi makini ya kipadre na kitawa ni kiini cha maisha na utume wa Baba Mtakatifu Francisko kwa wakati huu, ili kweli Kanisa liweze kuwapata Mapadre na Watawa wema, watakatifu na wachapakazi wanaoweza kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya Kristo Yesu na Kanisa lake. Maaskofu na wakuu wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume wanawajibika sana katika malezi na majiundo ya majandokasisi, watawa pamoja na wakleri wao kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Kanisa la Kristo! Hapa mkazo ni kuwa na muungano kamili na endelevu wa majiundo na malezi ya Kipadre: kiutu, kiroho, kiakili na katika shughuli za kichungaji. Malezi ya kiutu yanamtaka jandokasisi au mlelelewa kuwa na ukomavu na uwiano mzuri kati ya maisha ya kiroho na kiutu; mahusiano kati ya watu yanayojikita katika heshima na nidhamu. Bila ya kuwa na jicho la kichungaji, matatizo na changamoto zinazoweza kujitokeza katika maisha ya majandokasisi na walelewa, yanaweza kuwa ni mzigo mkubwa kwa siku za baadaye kwa mapadre na watawa wenyewe na kwa ajili ya familia ya Mungu inayowazunguka.

Wafanyakazi wa Ubalozi wa Vatican nchini Italia
Wafanyakazi wa Ubalozi wa Vatican nchini Italia

Kumbe, majiundo ya falsafa, taalimungu na shughuli za kichungaji yameboreshwa kwa kuongezewa tena majiundo ya kitume, utambulisho wa wito na utume wa kipadre na kitawa ili kuweza kuwa na mwelekeo mkamilifu wa Yesu Kristo mchungaji mwema. Padre mwema na mtawa mwema, mtakatifu na mchapakazi hapatikani kwa kufaulu vyema masomo na mitihani yake, bali anahitaji kuwa na ukomavu wa kiutu, maisha ya kiroho na shughuli za kichungaji. Awe makini na lugha anayoitumia katika maisha na utume wake bila kusahau mbinu msingi za malezi na majiundo. Mambo makuu mawili yamepewa kipaumbele cha kwanza: “Utu” yaani, Majandokasisi na walelewa wanapaswa kusindikizwa ili waweze kuwa na ukomavu katika utu wa binadamu, ili kweli waweze kupenda na kupendwa katika hali ya ukomavu; watu huru kutoka katika sakafu ya maisha yao; watu wanaoweza kujenga na kudumisha mahusiano ya kijamii; watu wenye amani na utulivu wa ndani; wanaoweza kutoa na kupokea na kumwilisha Mashauri ya Kiinjili katika maisha yao bila shuruti, unafiki wala kutafuta njia ya mkato. “Tasaufi” ni neno la pili, linalopewa kipaumbele cha pekee katika malezi na majiundo ya kipadre na maisha ya wakfu kwa kufunda dhamiri nyofu mintarafu maisha na wito wa Kipadre na Kitawa. Ikumbukwe kwamba, Padre au Mtawa si mfanyakazi wa mshahara wala mfanyabiashara anayelitumia Kanisa kwa ajili ya mafao yake binafsi. Padre na Mtawa ni mfuasi wa Kristo Yesu anayejisadaka kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake, kwa kujenga na kudumisha uhusiano wa pekee na Kristo kwa njia ya Neno, Sakramenti, Matendo ya huruma: kiroho na kimwili pamoja na sadaka binafsi, kielelezo cha Kristo mchungaji mwema. Mapadre wanapaswa kuboresha maisha yao ya kiroho yanayofumbatwa katika tunu msingi za Kiinjili kwa kujisikia kuwa na Kanisa kwa ajili ya Kanisa kama alivyokuwa Kristo Yesu.

Viongozi wa Jumuiya ya Watanzania Wakatoliki Wanaoishi Italia
Viongozi wa Jumuiya ya Watanzania Wakatoliki Wanaoishi Italia

Mapadre na Watawa wanapaswa kuwa ni watu wa “Huduma” yaani “Wasamaria wema”, watu wenye huruma, upendo na msamaha. Hawa ni watu wanaopaswa kujenga na kudumisha utamaduni wa kusikiliza kwa makini, kwani katika maisha na utume wao, watakutana na watu wenye kiu ya kusikilizwa; watu wanaweza kuanzisha na kudumisha mchakato wa majadiliano katika ukweli na uwazi pasi ya kuwa na jazba au kutaka kulipiza kisasi. Ikumbukwe kwamba, ndani ya familia ya Mungu kuna watu ambao wamejeruhiwa vibaya wanapaswa kugangwa na kuponywa na huruma na upendo wa Mungu kwa njia ya Sakramenti za Kanisa, ushauri makini na ushuhuda wenye mvuto na mashiko. Majandokasisi na Walelewa wanapaswa kuondokana na tabia ya kujifungia katika ubinafsi wao, tayari kujielekeza katika mwono mpana utakaowapatia mang’amuzi ya kina katika maisha na utume wao kwa siku za baadaye, kama Mapadrena Watawa. Baadhi ya Mapadre na Watawa wanaishi na kufanya kazi katika mazingira magumu na hatarishi, kumbe wanahitaji kusindikizwa kwa njia ya sala na sadaka ili kamwe wasikate tamaa, hata pale wanapoteleza na kuanguka katika udhaifu wa kibinadamu wawe na ujasiri wa kusimama tena na kusonga mbele kwa imani na matumaini. Kanisa pia limebahatika kuwa na umati mkubwa wa Mapadre wema, watakatifu na wachapakazi wanaoendelea kujisadaka kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake bila hata ya kujibakiza, wote hawa wanapaswa kuungwa mkono ili waendelee kusonga mbele kwani mapambano bado kabisa yanaendelea hapa duniani, hadi kitakapoeleweka. Mapadre wajenge na kudumisha utamaduni wa maisha matakatifu katika utume wao wa Kipadre, kwa kuendelea kuboresha maisha yao ya kiroho kwa njia ya nyenzo ambazo zimewekwa na Mama Kanisa; waendelee kuwajibika barabara katika shughuli za kichungaji kwa kushirikiana na watu wa Mungu waliokabidhiwa kwao. Mapadrena Watawa wawe makini na kuendelea kukesha daima katika sala, tafakari ya Neno la Mungu, Sakramenti na matendo ya huruma, na kamwe wasidhani kwamba wamekwisha kufika, bali wako safarini na bado kuna vishawishi na changamoto nyingi katika maisha na utume wa Kipadre na Kitawa!

Mapadre na Watawa waliopongezwa kwa hatua mbalimbali katika maisha
Mapadre na Watawa waliopongezwa kwa hatua mbalimbali katika maisha

Baba Mtakatifu anasema, maisha ya kijumuiya ni toba ya hali ya juu kabisa kama anavyokaza kusema Mtakatifu John Berchmans kwa lugha ya Kilatini kwamba, “Mea maxima poenitentia, vita communis.” Si rahisi sana kwani huu ni uhalisia wa maisha ya watu unaogusa matatizo, fursa na changamoto mbalimbali za maisha. Kuna wivu usiokuwa na mvuto wala mashiko; kuna tabia ya watu wa kutaka kujimwambafai, kuna mashindano ambayo watu wanataka kujikuza na kujiona bora zaidi kuliko wanajumuiya wengine; hali ya kutoelewana, kinzani na misigano ya kibinadamu. Yote haya yanaendelea kujengeka taratibu katika nyoyo za watu, kiasi hata cha mapadre na watawa kushindwa hata kusalimiana kama ndugu katika Kristo Yesu. Maisha ya kidugu katika jumuiya yanafumbatwa kwa namna ya pekee katika sala, kwa kuombeana, kusaidiana na kutegemezana kwa hali na mali kwani, hakuna maisha pasi na mikwaruzano, kama haya yanaweza kutokea katika familia na maisha ya watu wa ndoa, sembuse watawa wanaokutanishwa kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo na Daraja takatifu, ili kujisadaka kwa ajili ya Mungu na jirani? Baba Mtakatifu anakaza kusema, kukosa na kukoseana ni jambo la kawaida katika maisha ya pamoja, kusamehe na kusahau ni kuanza hija ya utakatifu wa maisha, pasi na kubaki na kinyongo moyoni. Mapadre na Watawa wajifunze kusema na kushuhudia ukweli wa mambo bila woga, kielelezo makini cha ukomavu na uhuru kamili! Masengenyo na unafiki ni sumu mbaya inayopekenyua hata kuua maisha ya kijumuiya. Watawa wawe na ujasiri wa kushirikishana shida, mang’amuzi, uzuri na changamoto wanazokumbana nazo katika nadhiri zao, yaani: ufukara, useja na utii, kama kielelezo cha ushuhuda wao kwa Kristo Yesu na kwa ajili ya ujenzi wa Ufalme wa Mungu! Watawa wawe ni nidhamu ya kuheshimu utu na heshima ya ndugu zao katika utawa na kamwe wasimpatie Shetani nafasi ya kuchafua utu na heshima ya ndugu zao katika Kristo Yesu!

Watanzania Mahubiri
27 May 2024, 14:51