Tafuta

Ujumbe wa Sikukuu ya Vesak Wakristo na Wabudha wanahimizwa kufanya kazi kwa pamoja ili kulinda na kudumisha amani. Ujumbe wa Sikukuu ya Vesak Wakristo na Wabudha wanahimizwa kufanya kazi kwa pamoja ili kulinda na kudumisha amani. 

Ujumbe wa Sikukuu ya Vesak Kwa Mwaka 2024: Amani na Upatanisho

Ujumbe kutoka Baraza la Kipapa la Majadiliano ya Kidini kama sehemu ya Maadhimisho ya Sikukuu ya Vesak kwa mwaka 2024 unahimiza pamoja na mambo mengine, kuhakikisha kwamba, dini hizi mbili zinajenga na kudumisha amani ili kuachana kabisa na vita, kama alivyokaza kusema Mtakatifu Paulo VI, wakati akilihutubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataita. Viongozi mbalimbali wa kidini na kisiasa wameendelea kulaani vita sehemu mbalimbali za Dunia, lakini vita bado ...

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Adui mkubwa wa mchakato wa majadiliano ya kidini ni woga na wasiwasi usiokuwa na msingi, mambo yanayochangia watu wa dini mbalimbali kushindwa kufahamiana na hatimaye kuishi kwa amani, umoja na udugu wa kibinadamu kwa kutambua kwamba, wote wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu na hivyo tofauti zao za kidini si sababu msingi ya malumbano na kinzani zisizo na tija wala mashiko kwa watu. Katika mchakato wa majadiliano ya kidini, Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kuhimiza umuhimu wa waamini wa dini mbalimbali kufahamiana na kushirikiana. Majadiliano ya kidini na waamini wa dini mbalimbali ni sehemu ya vinasaba vya Kanisa Katoliki ili kujenga na kudumisha amani, upendo na mshikamano kati ya watu na wala si kwa bahati mbaya kwamba, Kanisa katika sera, mikakati na vipaumbele vyake katika mchakato wa uinjilishaji linaendelea kukazia majadiliano ya kidini na waamini wa dini mbalimbali duniani.

Vesak: Ni Siku ya kuzaliwa kwa Budha, Upako na kifo chake
Vesak: Ni Siku ya kuzaliwa kwa Budha, Upako na kifo chake

Sikukuu ya "Vesak", ni siku ya mwezi uliokamilika na huadhimishwa mwezi wa Mei. Ni siku takatifu zaidi kwa mamilioni ya Wabudha ulimwenguni kote.  Na ilikuwa ni katika Siku ya Vesak milenia mbili na nusu zilizopita, mwaka wa 623 Kabla ya Kristo (KK), ambapo Gautama Budha alizaliwa. Ni katika siku hii Budha pia alipata upako na ni katika maadhimisho ya Sikukuu hii, Gautama Budha alipofariki dunia, akiwa na umri wa miaka 80 tangu alipozaliwa. Kumbe hii ni fursa ya kuwa karibu na watu wanaoteseka, ili kuwapatia faraja, amani na furaha kwa njia ya huduma inayojikita katika huruma. Ni katika muktadha wa Sikukuu ya Vesak kwa mwaka 2024, “Wakristo na Wabudha wanahimizwa kufanya kazi kwa pamoja kwa amani kwa njia ya upatanisho na ustahimilivu, mambo msingi yanayofumbatwa katika Mapokeo ya dini hizi mbili.

Wabudha na Wakristo washirikiane kudumisha amani duniani
Wabudha na Wakristo washirikiane kudumisha amani duniani

Hii ni sehemu ya ujumbe kutoka Baraza la Kipapa la Majadiliano ya Kidini kama sehemu ya Maadhimisho ya Sikukuu ya Vesak kwa mwaka 2024. Huu ni ujumbe unahimiza pamoja na mambo mengine, kuhakikisha kwamba, dini hizi mbili zinajenga na kudumisha amani ili kuachana kabisa na vita, kama alivyokazia kusema Mtakatifu Paulo VI, wakati akilihutubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa tarehe 4 Oktoba 1965. Viongozi mbalimbali wa kidini na kisiasa wameendelea kulaani vita sehemu mbalimbali za Dunia, lakini laana na matamko yao “hayajaweza kufua dafu”; vita, kinzani na migogoro mbalimbali inaendelea kupamba moto. Kumbe, kuna haja ya kufanya tafakari ya kina kuhusu umuhimu wa kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha amani sehemu mbalimbali za dunia, kila mtu akitekeleza dhamana na wajibu wake. Huu ni mwaliko kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuondokana na chuki pamoja na tabia ya kutaka kulipiza kisasi, mambo yanayowazamisha watu wa Mataifa katika vita.

Wakristo na Wabudha wasimame kidete kujenga msingi ya amani
Wakristo na Wabudha wasimame kidete kujenga msingi ya amani

Kumbe, waamini na watu wenye mapenzi mema wajizatiti zaidi katika mchakato wa upatanisho na ustahimivu, mambo yanayohitaji kwa waamini kufahamu vyema misingi ya imani yao. Amani na ustahimivu ni mambo msingi katika kukuza na kudumisha amani, usawa na haki katika masuala ya kisiasa, kiuchumi na kitamaduni. Msamaha na upatanisho ni chanda na pete, kwa sababu ni mfano hai kwa waamini kujikita katika sheria, kuondoa kufuru na hivyo kuendelea kujikita katika kujenga na kudumisha ukweli. Huu ni mwaliko kwa waamini wa dini hizi mbili kutolea shuhuda mchakato wa upatanisho na ustahimilivu, ili msamaha uweze kurejesha, kuganga na kuponya majeraha ya utengano wa mahusiano na mafungamano ya kijamii na hatimaye, amani na utulivu viweze kurejea tena, na hivyo kukuza matumaini kwa leo na kesho iliyo bora zaidi, tayari kukabiliana na changamoto mamboleo kwa ari na mwamko mkubwa zaidi.

Ondoeni chuki na uhasama ili kujenga haki na amani
Ondoeni chuki na uhasama ili kujenga haki na amani

Upatanisho na ustahimilivu ni nyenzo muhimu katika kupambana na uvunjifu wa amani; mambo msingi katika kutafuta na kudumisha upendo na jirani zao. Huu ni mwaliko kwa waamini wa dini hizi mbili kukataa kishawishi cha kutumbukia katika chuki na hasira na badala yake wawe ni vyombo na wajenzi wa upatanisho. Mwenyeheri Maha Ghosanda ni shuhuda wa mauaji ya kimbari yaliyofanyika huko Cambodia, changamoto na mwaliko wa kungo’a ndago za chuki nyoyoni mwao. Baba Mtakatifu Francisko anasema: “Upatanisho na malipizi vinawakirimia waamini maisha mapya na hivyo kuwaweka huru na kuwaondoa katika woga. Huu ni mwaliko kwa waamini kuhakikisha kwamba, wanaondoa hisia za uadui miongoni mwao, na kuanza kujikita katika toba na wongofu wa ndani, kwa kukubali yaliyopita na kutofunika yajayo mbeleni mwao kwa majuto, matatizo na mipango yao. Waamini na watu wote wenye mapenzi mema wameitwa kutunza amana na utajiri huu unaobubujika kutoka katika Mapokeo ya dini hizi mbili, ili kuwaunganisha waamini wengine na hivyo kuanza kutembea pamoja kwa ajili ya kujenga amani duniani.

VESAK 2024
07 May 2024, 15:34