Wanataaluma wamekusanyika mjini Vatican kwa Mkutano wa Kimataifa wa Hisia!
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Wakurugenzi wengi kutoka vyuo vikuu vinavyoongoza duniani, wasomi mashuhuri, watu mashuhuri wa kiutamaduni na vijana wenye ushawishi wamekusanyika mjini Vatican kwa ajili ya kongamano la kimataifa la siku tatu, tarehe 21hadi 23 Mei 2024. Tukio hilo limeandaliwa na Shirika la Kipapa la Scholas Occurrentes, pamoja na Benki ya Maendeleo ya Amerika ya Kusini (CAF), katika mfumo wa Chuo Kikuu cha Hisia (Universidad del Sentido).
Chuo kikuu hiki chenye makao yake makuu mjini Vatican, kinachofadhiliwa na Papa Francisko na kusimamiwa na Jumuiya ya Kimataifa ya Kielimu ya Scholas Occurrentes, kilianzishwa kwa lengo la kushughulikia masuala muhimu ambayo yamechochewa na msukosuko wa maana wa ulimwengu mamboleo, kama vile athari za teknolojia, mazingira na afya ya akili. Mkutano wa Kimataifa wa Hisia unakuja baada ya ushirikiano kati ya Scholas na CAF, ambao umejumuisha mipango mashuhuri ya kielimu, pamoja na uzinduzi wa Shule ya kwanza ya Laudato Sí mnamo Mei 2022. Mpango huo ulishuhudia wawakilishi vijana 50 kutoka nchi mbalimbali za Amerika ya Kusini na Carribein wakikusanyika ili kujadili masuala muhimu ya kimazingira na kijamii.
Zaidi ya hayo, mnamo Mei 2023, Scholas na CAF walipanga Kongamano la kwanza la Ulimwengu la "Miji ya Kielimu-Eco-Elimu," ambalo liliwaleta pamoja baadhi ya mameya 50 kutoka Amerika ya Kusini na Ulaya, ili kukuza na kueneza maendeleo endelevu katika mbinu zote za elimu zinazoendelezwa na harakati ya elimu na uzoefu unaofanywa na vijana katika jumuiya zao kwa kuzingatia wazo la Papa Francisko la “ikolojia fungamani” lililopendekezwa katika Waraka wa Laudato si.’” Matokeo ya maendeleo ya mipango hii ya awali yatajadiliwa wakati wa mkutano wa siku tatu. Kikao cha mwisho cha mkutano huo kitafanyika Alhamisi mchana, tarehe 23 Mei, katika Ukumbi wa Sinodi ya Kale, ambapo washiriki watawasilisha matokeo na mapendekezo yao kwa Baba Mtakatifu Francisko.