Tafuta

Askofu Krzysztof Josef Nykiel, Hakimu mkuu wa Idara ya Toba ya Kitume amewekwa wakfu tarehe 22 Juni 2024 Askofu Krzysztof Josef Nykiel, Hakimu mkuu wa Idara ya Toba ya Kitume amewekwa wakfu tarehe 22 Juni 2024 

Askofu Krzysztof Josef Nykiel, Hakimu Mkuu, Idara ya Toba ya Kitume

Askofu Krzysztof Josef Nykiel, Hakimu mkuu wa Idara ya Toba ya Kitume aliyeteuliwa na Baba Mtakatifu Francisko Mei Mosi, 2024 kuwa Askofu na kuwekwa wakfu tarehe 22 Juni 2024 na Kardinali Mauro Piacenza, Mhudumu mkuu mstaafu wa Toba ya Kitume anamshukuru Mungu kwa zawadi ya wito. Kauli mbiu yake ya kiaskofu ni “Patris Corde” yaani “Kwa Moyo wa Kibaba.” Alizaliwa Mwaka 1964, Daraja ya Upadre Mwaka 1990 na Uaskofu tarehe 22 Juni 2024. Huruma!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, huruma ya Mungu ndiyo mahangaiko ya upendo wake kwa binadamu dhaifu na mdhambi. Mwenyezi Mungu anajisikia kuwajibika, kwa maana ya kwamba, anatamani kuwaona watu wake wakiwa na afya njema, furaha na amani tele nyoyoni mwao. Hii ni njia ambayo upendo wa huruma ya Wakristo unavyopaswa pia kujimwilisha. Huruma ndiyo msingi thabiti wa uhai wa Kanisa. Kazi zake zote za kichungaji zinapaswa kufungamanishwa katika upole linalouonesha kwa waamini; hakuna chochote katika mahubiri na ushuhuda wake kwa ulimwengu kinachoweza kukosa huruma. Umahiri wa Kanisa unaonekana kwa namna linavyoonesha huruma na upendo. Huruma ya Mungu inafungua malango ya moyo ili kuonesha upendo na ukarimu kwa watu wanaoishi katika upweke na kusukumizwa pembezoni mwa jamii, ili kweli waweze kujisikia ndugu na watoto wapendwa wa Baba wa milele kama ilivyokuwa kwa Mwana mpotevu, shilingi na kondoo aliyepotea. Huruma ya Mungu inawawezesha watu kutambua na kuguswa na mahitaji msingi ya jirani zao hasa wale wanaohitaji kuonjeshwa faraja na upendo. Kimsingi, huruma ya Mungu inawawezesha waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kuwa ni vyombo na mashuhuda wa haki, amani na upatanisho.

Huruma ya Mungu ni tunda la Kipasaka, mateso, kifo na ufufuko
Huruma ya Mungu ni tunda la Kipasaka, mateso, kifo na ufufuko

Ikumbukwe kwamba, huruma ya Mungu ni kiini cha imani, maisha na utume wa Kanisa; ushuhuda makini wa: Mateso, Kifo na Ufufuko wa Kristo Yesu. Bikira Maria, Mama wa huruma ya Mungu awasaidie waamini: kuamini na kuyaishi yote haya kama mashuhuda wa Injili ya huruma, furaha na mapendo. Mama Kanisa anaendelea kutoa kipaumbele cha pekee katika Sakramenti ya Upatanisho kama mahali muafaka pa kuonja: msamaha wa dhambi, huruma na upendo wa Mungu, tayari kusimama tena na kuendelea na safari ya imani, matumaini na mapendo kwa Mungu na jirani! Baba Mtakatifu Francisko anawakumbusha Mapadre waungamishaji kwamba, wao ni vyombo na mashuhuda wa upatanisho, huruma na upendo wa Mungu na kamwe si wamiliki wa dhamiri za waamini. Wajenge utamaduni na sanaa ya kusikiliza kwa makini, ili wawasaidie waamini wao kufanya mang’amuzi ya kina kuhusu maisha na wito wao ndani ya Kanisa na jamii katika ujumla wake! Ikumbukwe kwamba, huruma ya Mungu inapaswa kuendelea kumwilishwa katika maisha ya watu sehemu mbali mbali za dunia kama alama ya mwendelezo wa Mwaka wa Huruma ya Mungu.

Kardinali Mauro Piacenza
Kardinali Mauro Piacenza

Ni katika muktadha wa huruma ya Mungu kwa waja wake, Monsinyo Krzysztof Josef Nykiel, Hakimu mkuu wa Idara ya Toba ya Kitume aliyeteuliwa na Baba Mtakatifu Francisko Mei Mosi, 2024 kuwa Askofu na kuwekwa wakfu tarehe 22 Juni 2024 na Kardinali Mauro Piacenza, Mhudumu mkuu mstaafu wa Toba ya Kitume anamshukuru Mungu kwa zawadi ya wito. Kauli mbiu yake ya kiaskofu ni “Patris Corde” yaani “Kwa Moyo wa Kibaba.” Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kitume “Patris Corde” yaani “Kwa Moyo wa Kibaba”: alitangaza “Mwaka wa Mtakatifu Yosefu, Kumbukumbu ya Miaka 150 Tangu Mtakatifu Yosefu alipotangazwa Kuwa Msimamizi wa Kanisa la kiulimwengu.” Ibada hii imeadhimishwa kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Katika mahubiri yake, Kardinali Mauro Piacenza amesema, Daraja Takatifu ya Uaskofu inapata chanzo chake kutoka katika Sakramenti ya Ubatizo, zawadi inayomwezesha mwamini kuwa ni Mkristo, mwaliko kwa waamini kujiamisha katika huruma na upendo wa Mungu; tayari kuwa ni vyombo na mashuhuda wa huruma na msamaha wa Mungu kwa waja wake.

Huruma ya Mungu ni chemchemi ya furaha, imani, matumaini na mapendo
Huruma ya Mungu ni chemchemi ya furaha, imani, matumaini na mapendo

Askofu Krzysztof Josef Nykiel, Hakimu mkuu wa Idara ya Toba ya Kitume amemshukuru Mungu na watu wote wa Mungu waliohudhuria kwa wingi katika Ibada ya kuwekwa kwake wakfu kuwa Askofu, kielelezo cha huruma na upendo wa Mungu katika maisha yake na kama kielelezo cha utimilifu wa Daraja Takatifu ya Upadre. Anamshukuru Baba Mtakatifu Francisko kwa kumwezesha kujiunga na urika wa Maaskofu wa Kanisa Katoliki. Itakumbukwa kwamba, Askofu Krzysztof Josef Nykiel, Hakimu mkuu wa Idara ya Toba ya Kitume alizaliwa tarehe 28 Februari 1964 huko Osjakòw nchini Poland. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, tarehe 9 Juni 1990 akapewa daraja takatifu ya Upadre kwa ajili ya Jimbo Katoliki la Lodz. Mwaka 2001 akajipatia Shahada ya Uzamivu kwenye Sheria za Kanisa kutoka Chuo Kikuu cha Kipapa cha Gregorian. Tarehe 26 Juni 2012 Baba Mtakatifu Benedikto XVI akamteuwa kuwa Hakimu mkuu wa Idara ya Toba ya Kitume. Mei Mosi 2024 Baba Mtakatifu Francisko akamteuwa kuwa Askofu na hatimaye, kuwekwa wakfu kama Askofu tarehe 22 Juni 2024 kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican.

Daraja ya Uaskofu

 

23 June 2024, 15:46