Askofu mkuu Luís Miguel Muñoz Cárdaba Awasilisha Hati za Utambulisho Msumbiji
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko amemteua Askofu mkuu Luís Miguel Muñoz Cárdaba kuwa Balozi mpya wa Vatican nchini Msumbiji. Kabla ya uteuzi huu, Askofu mkuu Luís Miguel Muñoz Cárdaba alikuwa ni Balozi wa Vatican nchini Sudan na Eritrea. Itakumbukwa kwamba, Askofu mkuu Luís Miguel Muñoz Cárdaba alizaliwa tarehe 25 Agosti 1965 huko Vallelado, nchini Hispania. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, tarehe 28 Juni 1992 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre. Alijiendeleza na hatimaye, kubahatika kupata Shahada ya Uzamili katika masomo ya taalimungu, Sheria za Kanisa pamoja na Sheria na Taratibu za Uendeshaji wa Kesi Mahakamani, “Giurisprudenza.” Askofu mkuu Luís Miguel Muñoz Cárdaba alianza kutoa huduma za Kidiplomasia mjini Vatican hapo tarehe 1 Aprili 2001. Tangu wakati huo akatumwa kwenye Balozi za Vatican nchini Ugiriki, Mexico, Ubelgiji, Italia, Australia, Ufaransa na Uturuki. Na ilipofika tarehe 31 Machi 2020 Baba Mtakatifu Francisko akamteuwa kuwa Balozi wa Sudan na Eritrea na kumpandisha hadhi na kuwa ni Askofu mkuu na hatimaye, kuwekwa wakfu kuwa Askofu mkuu na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican tarehe 25 Julai 2020. Na hatimaye, 23 Januari 2024 Baba Mtakatifu Francisko akamteuwa Askofu mkuu Luís Miguel Muñoz Cárdaba kuwa ni Balozi mpya wa Vatican nchini Msumbiji. Ni katika muktadha wa uteuzi huu, hivi karibuni Askofu mkuu Luís Miguel Muñoz Cárdaba, amewasilisha hati zake za utambulisho kwa Rais Filipe Jacinto Nyusi wa Msumbiji, ambaye amemshukuru na kumpongeza Baba Mtakatifu Francisko kama sehemu ya kumbukizi ya miaka mitano ya hija yake ya kitume nchini Msumbiji.
Kauli mbiu iliyoongoza hija ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Msumbiji ni: matumaini, amani na upatanisho. Baba Mtakatifu katika hotuba yake alionesha uwepo wake wa karibu, upendo na mshikamano na familia ya Mungu nchini Msumbiji kutokana na majanga asilia. Alikazia umuhimu wa kujenga amani na upatanisho wa kidugu; mchakato wa maendeleo endelevu sanjari na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote! Baba Mtakatifu aliwashukuru watu wa Mungu nchini Msumbiji kwa mapokezi na ukarimu waliomwonesha wakati wa hija yake nchini Msumbiji. Aliwapongeza kwa utajiri wa tamaduni, uoto wa asili, furaha na matumaini ya watu wa Mungu nchini Msumbiji. Aliwashukuru wadau wote waliojisadaka bila kujibakiza ili kupyaisha tena mchakato wa amani na upatanisho nchini Msumbiji. Baba Mtakatifu aliipongeza na kuishukuru Jumuiya ya Kimataifa ambayo kwa miaka ya hivi karibuni imesimama kidete ili kuhakikisha kwamba mchakato wa amani na upatanisho wa kitaifa, licha ya matatizo na changamoto zake, unarejea tena na matokeo yake ni kutiwa saini kwa Mkataba wa Amani huko Serra da Gorongosa kati ya Chama cha FRELIMO na RENAMO. Mkataba huu unafutilia mbali uhasama kati ya ndugu wamoja nchini Msumbiji na kwamba, Mkataba huu utaimarisha zaidi Mkataba wa Amani uliotiwa saini mjini Roma kunako mwaka 1992. Matunda ya mchakato huu yameanza kuonekana kwa kutambuana kama ndugu, wenye dhamana na wajibu wa kuendeleza ustawi wa nchi ya Msumbiji.
Ujasiri unaleta amani ya kweli, unatafuta na kudumisha ustawi na maendeleo ya wengi. Wananchi wa Msumbiji wameteseka sana na madhara ya vita na kinzani za kijamii, lakini hawakutaka kukubali kutawalia na chuki, uhasama na mtindo wa kutaka kulipizana kisasi na kwamba, vita haikuwa na usemi wa mwisho katika mustakabali wa wananchi wa Msumbiji. Vita imeharibu sana makazi ya watu, imewatumbukiza wananchi katika baa la njaa, ujinga na maradhi. Vita imewakosesha watu nyumba za sala na ibada; imepelekea watu kukosa fursa za ajira na kwamba, kuna umati mkubwa wa wananchi wa Msumbiji walilazimika kuikimbia nchi yao ili kutafuta: usalama na hifadhi ya maisha yao. Huu ni wakati wa kukumbatia amani na kuachana kabisa na falsafa ya mtutu wa bunduki. Baba Mtakatifu aliendelea kufafanua kwamba, mchakato wa kutafuta amani ya kudumu ni endelevu na unajikita katika ukweli na uwazi; ujasiri na unyenyekevu pasi na baadhi ya watu kutaka kujikweza. Ni mchakato unaofumbatwa katika ushupavu ili kukuza na kudumisha amani na upatanisho, kwani vita inaleta maafa kwa watu na mali zao. Amani ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu inayowawajibisha hasa wale ambao wamepewa dhamana ya uongozi ili kuhakikisha kwamba wanalinda: utu na heshima ya ndugu zao ili hata wao pia wajisikie kuwa ni sehemu muhimu sana ya mchakato wa maendeleo kwa mustakabali wa nchi yao.
Ili kudumisha amani ya kweli, kuna haja ya kujenga mazingira ya haki na usawa ili kuondokana na vurugu na migongano inayoweza kupelekea jamii kulipuka kwa vita na misigano ya kijamii. Kukosekana kwa usawa kutawafanya wale waliotengwa kujibu “mapigo” kwa ghasia. Kupatikana kwa amani nchini Msumbiji kumepelekea maboresho makubwa katika sekta ya elimu na afya na kwamba, kuna haja ya kuendelea kuwekeza katika maendeleo fungamani ya binadamu na asiwepo hata mtu mmoja atakaye achwa nyuma katika maendeleo. Baba Mtakatifu alisema, vijana wapewe kipaumbele cha kwanza kwani wao wanaunda sehemu kubwa ya familia ya Mungu nchini Msumbiji. Changamoto mamboleo, ziwabidiishe kutumia vipaji vyao vya ubunifu, hawa ni mbegu iliyopandikizwa tayari, wakipewa fursa, watachangia mchakato wa ukuaji wa jamii unaotakiwa na wengi. Ikumbukwe kwamba, utamaduni wa amani ni mchakato endelevu unaopaswa kuwashirikisha hata vijana wa kizazi kipya; kwa kujenga na kudumisha utamaduni wa watu kukutana; kwa kuheshimiana na kuthaminiana kama ndugu wamoja. Kumbe, utulivu ni hitaji muhimu, ili kuweza kufikia malengo yaliyobainishwa, nguvu msingi za maisha na mawazo yanayofyekelea mbali ile tabia ya kudhaniana vibaya. Utajiri mkubwa nchini Msumbiji unapaswa kuwa ni huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, kwa kuhakikisha kwamba, wanapata elimu makini, makazi bora zaidi pamoja na fursa za ajira. Sanjari na haya, wakulima wawe na mashamba kwa ajili ya shughuli za kilimo. Huu ni msingi wa matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi na silaha madhubuti ya amani ya kudumu!
Ni katika muktadha huu, Msumbiji inapaswa pia kusimama kidete kulinda na kutunza mazingira nyumba yote, kama njia ya kulinda uhai. Ardhi iwe ni kwa ajili ya mafao ya wengi na kwamba, amani ya kudumu inafumbatwa katika mchakato wa maendeleo fungamani ya binadamu. Mwishoni mwa hotuba yake, Baba Mtakatifu aliwaambia viongozi wa Serikali, wanadiplomasia pamoja na wawakilishi wa vyama vya kiraia nchini Msumbiji kwamba, wao wote ni wasanii katika ujenzi wa haki na upatanisho wa kidugu nchini Msumbiji; kwa kulinda haki na amani kwa ajili ya watoto wao. Muda huu anapenda pia kuutumia kwa ajili ya kujenga na kudumisha umoja na mshikamano na Maaskofu Katoliki kwani Kanisa limekuwa ni msaada mkubwa katika mchakato wa kutafuta amani, upatanisho na matumaini. Askofu mkuu Luís Miguel Muñoz Cárdaba na Rais Filipe Jacinto Nyusi wa Msumbiji katika mazungumzo yao, wameridhishwa na uhusiano mzuri kati ya Vatican na Msumbiji na kwamba, uhusiano huu unaendelea kuimarishwa kwa uwepo wa Mabalozi wa Vatican nchini Msumbiji. Kwa upande wake, Askofu mkuu Luís Miguel Muñoz Cárdaba ameridhishwa na mchango wa Kanisa katika ustawi, maendeleo na ustawi wa watu wa Mungu nchini Msumbiji. Changamoto kubwa kwa wamisionari kupata na kupyaisha tena nyaraka za kuishi na kufanya utume wao nchini Msumbiji.