Hati Kuhusu "Askofu wa Roma. Ukuu wa Sinodi, Majadiliano ya Kiekumene; Waraka wa Ut Unum Sint
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baraza la Kipapa la Kuhamasisha Umoja wa Wakristo, tarehe 13 Juni 2024 limechapisha Hati kuhusu: "Askofu wa Roma. Ukuu na Sinodi katika Majadiliano ya Kiekumene na Katika Majibu ya Waraka wa Ut unum sint." Mtakatifu Yohane Paulo II tarehe 25 Mei 1995 alichapisha Waraka wake wa Kitume “Ut unum sint” yaani “Ili Wawe Wamoja: Dhamana ya Kiekumene.” Huu ni mwendelezo wa majadiliano ya kiekumene yaliyoanzishwa na Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican na ni njia ya Kanisa inayojikita katika upyaisho wa maisha na wongofu wa ndani. Ni Waraka wa Kitume uliochapishwa kama kumbukumbu ya miaka 30 baada ya Maadhimisho ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican. Mtakatifu Yohane Paulo II akakazia tena umuhimu wa kuendeleza mchakato wa majadiliano ya kiekumene miongoni mwa Wakristo wa Makanisa na Madhehebu mbalimbali, ili kujenga fumbo la Mwili wa Kristo yaani Kanisa ambalo limejeruhiwa kutokana na utengano miongoni mwa Wakristo na kwamba, majadiliano ya kiekumene ni sehemu ya maisha na vinasaba vya Kanisa Katoliki! Hati kuhusu: "Askofu wa Roma. Ukuu na Sinodi katika Majadiliano ya Kiekumene na Katika Majibu ya Waraka wa Ut unum sint” imegawanyika katika sehemu kuu nne: Utangulizi; Maswali msingi ya kitaalimungu; Usimamizi wa huduma ya umoja katika Kanisa lililounganishwa tena; Baadhi ya ushauri au Maombi yaliyoelekezwa kwa Kanisa Katoliki; Muhtasari; Kuelekea zoezi la Ukulu katika karne ya 21. Pendekezo kutoka kwa mkutano wa mkuu wa Baraza la Kipapa la Kuhamasisha Umoja wa Wakristo unaozingatia Waraka wa “Askofu wa Roma”; na hatimaye ni vyanzo vya hati hii. Kama sehemu ya kumbukizi ya Miaka 25 ya Waraka wa Kitume “Ut unum sint” yaani “Ili Wawe Wamoja: Dhamana ya Kiekumene” imekuwa ni fursa ya kuendeleza majadiliano ya kiekumene, kwa kutofautisha asili na utekelezaji wa ukulu wa Mtakatifu Petro.
Kumekuwepo na maendeleo kwa kiasi fulani kwa Baba Mtakatifu Francisko kuitisha Sinodi ya XVI ya Maaskofu kuanzia mwaka 2021 hadi mwaka 2024 na mchango wa Baraza hili katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene mintarafu mchakato wa ujenzi wa Kanisa la Kisinodi. Hati hii ni muhtasari wa maadhimisho ya majadiliano ya kiekumene na ujenzi wa Kanisa la Kisinodi, iliyoridhiwa na Baba Mtakatifu Francisko, kama changamoto na hamasa ya kuendeleza utafiti wa kitaalimungu, ili hatimaye, kutoa mapendekezo kama sehemu ya utekelezaji wa utume wa umoja unaotekelezwa na Askofu wa Roma na unaotambuliwa na wote. Kumbe kuna haja ya kutafuta njia za utekelezaji wa ukulu wa Mtakatifu Petro mintarafu umoja na huduma ya upendo, inayohitaji wongofu wa kichungaji sanjari na ujenzi wa Kanisa la Kisinodi linalosimikwa katika nguvu ya Roho Mtakatifu na kulifanya lisilokosea “In Credendo” kwa sababu Mwenyezi Mungu huwajalia waamini wote silika ya imani “Sensus fidei.” Unaowasaidia kupambanua kile kilicho kweli cha Mungu. Huu ni mwaliko wa kufanya upembuzi yakinifu kuhusu ukulu wa Mtakatifu Petro. Maswali msingi ya kitaalimungu kama jibu msingi la Waraka wa Kitume “Ut unum sint” yaani “Ili Wawe Wamoja: Dhamana ya Kiekumene” ni yale yaliyotolewa na Makanisa pamoja na Madhehebu mbalimbali ya Kikristo; makongamano ya kiekumene pamoja na semina mbalimbali. Mwendelezo wa majadiliano ya kitaalimungu ili kutoa utambulisho wa ukulu wa Mtakatifu Petro kama kielelezo cha umoja na huduma. Kwa hakika, kumekuwepo na uelewa chanya wa dhamana na utume wa Khalifa wa Mtakatifu Petro, kama kielelezo cha umoja wa Kanisa pamoja na kutambua udugu wa Kikristo. Kumbe, tafakari ya kitaalimungu inapaswa kujikita katika mafundisho makuu ya Kanisa pamoja na mang’amuzi ya waamini wa Makanisa haya, kwa kujenga na kudumisha umoja na mshikamano katika uhalisia wa maisha kama ambavyo inaendelea kujionesha hata kwa wakati huu.
Usimamizi wa huduma ya umoja katika Kanisa lililounganishwa tena. Sehemu hii inachota amana na utajiri wake kutoka katika Maandiko Matakatifu: Mt 16:17-19 Yn 21:15. Kumekuwepo na mwelekeo mpya wa uelewa juu ya Ukulu wa Mtakatifu Petro mintarafu Maandiko Matakatifu, Mafundisho ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican na kwamba, Mtakatifu Petro hakuwa peke yake aliyetekeleza dhamana ya umoja na huduma kwa Kanisa la mwanzo. Kumbe, dhamana ya Askofu inachukua uzito mkubwa zaidi kama huduma ya upendo. Utume wa Mtakatifu Petro kadiri ya Mapokeo na Mafundisho ya Mababa wa Kanisa ni matokeo ya maendeleo ya kihistoria, kumbe, kuna haja ya kuangalia sheria ya Mungu “Iure divino” na Sheria ya binadamu “Iure humano” katika utekelezaji wa ukulu wa Mtakatifu Petro mintarafu mahitaji ya Kanisa na mwelekeo wake wa kihistoria. Mtaguso Mkuu wa Kwanza wa Vatican ulikabiliana na changamoto zake lakini kuna haja ya kutofautisha nia na maelezo; nyaraka na tafsiri zake; Mafundisho Sadikifu ya Kanisa, lakini Injili zipewe kipaumbele cha kwanza pamoja na kuhimiza urika wa Maaskofu wanapotekeleza dhamana ya kuongoza, kufundisha na kuwatakatifuza watu wa Mungu. Usimamizi wa huduma ya umoja katika Kanisa lililounganishwa tena, swali la msingi hapa, Je, Ukulu wa Mtakatifu Petro ni muhimu kwa Kanisa zima? Umuhimu wa Makanisa mahalia umetiliwa mkazo katika majadiliano ya kiekumene na kwamba, ujenzi wa Kanisa la Kisinodi na Ukulu wa Mtakatifu Petro ni mambo msingi katika ujenzi wa umoja wa Kanisa na kwamba, kuna haja ya kuwa na utume kwa ajili ya umoja wa Kanisa katika ngazi ya kiulimwengu ili kukuza na kudumisha Maandiko Matakatifu na Mapokeo ya Kanisa.
Ukuu wa Mtakatifu Petro ni heshima inayotolewa kwa Askofu wa Roma kama inavyojieleza kwenye Mitaguso mbalimbali. Kuna haja ya kuwa na kanuni msingi zitakazowezesha utekelezaji wa Ukulu wa Mtakatifu Petro, kwa kujibu kikamilifu changamoto katika ulimwengu mamboleo yaani: Utofauti, Urika na Kanuni ya Auni. Kuna mwingiliano kati ya ukulu wa Mtakatfu Petro na Ujenzi wa Kanisa la Kisinodi katika maisha na utume wa Kanisa. Baadhi ya ushauri au Maombi yaliyoelekezwa kwa Kanisa Katoliki: Kuna haja ya kufanya mageuzi makubwa ndani ya Kanisa Katoliki ili kweli Ukulu wa Mtakatifu Petro uweze kukubalika na wengi, kwa kufanya tafsiri ya kina ya Mtaguso Mkuu wa Kwanza wa Vatican; kuwepo na utofauti kati ya utekelezaji wa ukulu wa Askofu wa Roma na kwamba, mkazo zaidi uwe ni katika mchakato wa ujenzi wa Kanisa la Kisinodi ndani na nje unaotekelezwa katika ari na moyo wa uvumilifu na majadiliano ya kidugu. Huu ni mwaliko wa kufanya kazi na kusali kwa pamoja kama ilivyotokea wakati wa hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Sudan ya Kusini kunako mwaka 2023; sanjari na mkesha wa sala ya kiekumene kama sehemu ya ufunguzi wa maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu mwezi Oktoba 2023. Muhtasari; Waraka wa Kitume “Ut unum sint” yaani “Ili Wawe Wamoja: Dhamana ya Kiekumene” umeendelea kufanyiwa kazi na Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wake kwa kujikita katika ujenzi wa Kanisa la Kisinodi. Kumekuwepo na mwelekeo mpya wa kitaalimungu kwa kukazia Askofu wa Roma kama kielelezo cha huduma; Ukulu wa Mtakatifu Petro unapaswa kuangaliwa kama “Sheria ya Kimungu “De iure divino na Sheria ya Kibinadamu “de iure humano.” Mafundisho ya Mtaguso Mkuu wa Kwanza wa Vatican ni kikwazo cha umoja wa Kanisa.
Umoja wa Wakristo unasimikwa katika ukweli na upendo. Kutokosea kwa ukuu wa Injili, Kutokosea kwa Kanisa zima na Urika wa Maaskofu ni mambo ambayo bado yanapaswa kufanyiwa kazi. Umisionari wa Kanisa na Ulimwengu wa utandawazi ni kati ya changamoto zinazomsibu Khalifa wa Mtakatifu Petro wakati wa kutekeleza wajibu wake. Mapendekezo muhimu ni kusoma tena Nyaraka za Mtaguso Mkuu wa kwanza wa Vatican na kuzifasiri tena upya mintarafu tamaduni na majadiliano ya kiekumene kwa sasa pamoja na kupyaisha utume wa Khalifa wa Mtakatifu Petro kwa kukazia ujenzi wa Kanisa la Kisinodi, mchakato unaowashirikisha watu watakatifu wa Mungu. Kuna ushauri wa viongozi wa Kanisa kukutana mara kwa mara ili kujenga na kudumisha umoja wa Kanisa, kwa kutenda na kushuhudia umoja wa Kanisa. Kuelekea zoezi la Ukulu katika karne ya 21. Kumekuwepo na majadiliano mapana ya kiekumene kuhusu asili, maisha na utume wa Kanisa; mambo ambayo yamechangia kwa kiasi kikubwa majadiliano ya kiekumene kwa kukazia kuhusu: Ushiriki mkamilifu wa watu watakatifu wa Mungu katika maisha na utume wa Kanisa; Urika wa Maaskofu pamoja na ujenzi wa Kanisa la Kisinodi. Kumbe, kuna haja ya kusonga mbele katika majadiliano ya kitaalimungu, ili yaweze kukamilishana; Ufafanuzi wa misamihati inayotumika pamoja na ufahamu wa “dhana” ya Kanisa la kiulimwengu. Mkazo ni majadiliano katika ukweli na uwazi; majadiliano ya upendo na maisha mintarafu sala za pamoja, ushuhuda wa shughuli za kichungaji pamoja na kukuza udugu wa kibinadamu. Tofauti lazima iwepo kati ya utume unaotekelezwa na Papa kama mkuu wa Kanisa Katoliki na Papa kama kiongozi wa Mkanisa yote. Katiba mpya ya Kitume: “Predicate evangelium” yaani “Hubirini Injili” Juu ya Sekretarieti kuu “Curia Romana” na Huduma Yake Kwa Kanisa na Kwa Ulimwengu” imepyaisha dhamana na utume wa Sekretarieti kuu ya Vatican na ni sehemu muhimu sana ya ujenzi wa Kanisa la Kisinodi katika mchakato wa ujenzi wa umoja wa Kanisa. Katika Kristo Yesu Kanisa ni kama Sakramenti, ishara na chombo cha kuwaunganisha watu kiundani na Mungu na kuleta umoja kati ya wanadamu wote. Kanisa ni Taifa jipya la Mungu; tabia ya kieskatolojia ya Kanisa linalosafiri na umoja wa Kanisa lililo mbinguni. Rej. LG 1, 9, 48. Ikumbukwe kwamba, umoja wa Kanisa ni zawadi kutoka kwa Roho Mtakatifu.