Mtakatifu Gaspari Del Bufalo: Miaka 70 Tangu Atangazwe Kuwa Mtakatifu
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Gaspare Melchiorre Baldassarre del Bufalo “Gaspari, Melkiori na Bartazari del Bufalo” alizaliwa tarehe 6 Januari 1786 mjini Roma. Akafariki dunia tarehe 28 Desemba 1837 mjini Roma na kuzikwa kwenye Kanisa la “Santa Maria in Trivio, Roma. Papa Pio X akamtangaza kuwa ni Mwenyeheri mwaka 1904. Na tarehe 12 Juni 1954, miaka 70 iliyopita Papa Pio XII akamtangaza kuwa ni Mtakatifu, matendo makuu ya Mungu. Mtakatifu Gaspari del Bufalo ni mfano bora wa uinjilishaji wa kina unaojikita katika ushuhuda na utakatifu wa maisha. Mtakatifu Gaspari ni mtume hodari wa Damu Azizi ya Yesu, chemchemi ya huruma, upendo na ukombozi wa mwanadamu. Katika maisha na utume wake, alibahatika kusimama kidete na kwa ujasiri mkubwa, akapambana na madhulumu dhidi ya Kanisa wakati wake, huku akiwa amejiaminisha na kujikabidhi chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa. Mtakatifu Gaspari del Bufalo alikuwa ni mhubiri maarufu wa Neno la Mungu lililoacha chapa ya kudumu katika maisha ya wale wote waliolisikiliza. Mtakatifu Gaspari del Bufalo alijisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu, akawa na ujasiri wa kuweza kusikiliza na kujibu kilio cha maskini na wale wote waliokuwa wametengwa na jamii kutokana na kukengeuka na hatimaye, kutopea katika dhambi. Kwa watu wote hawa, Gaspari akajipambua kwao kuwa ni ndugu, rafiki na mlinzi mwaminifu katika hija ya maisha! Mtakatifu Gaspari del Bufalo ni alama na kielelezo cha sadaka ya maisha yaliyomiminwa katika tamaduni za watu mbalimbali duniani, ili kusikiliza na kujibu kilio cha “Damu ya Kristo” inayoendelea kumwagika sehemu mbalimbali za dunia kutokana na umaskini, magonjwa, dhuluma na nyanyaso.
Kristo Yesu katika mahubiri yake alitaka kuwahubiria maskini Habari Njema, kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao na vipofu kupata kuona tena, kuwaacha huru waliosetwa na kutangaza mwaka wa Bwana uliokubalika. Waamini wanapaswa kuwa kweli ni wajumbe, vyombo na mashuhuda wa Injili ya matumaini, upendo na mshikamano wa dhati kwa wale waliopondeka na kuvunjika moyo, kiasi cha kukata tamaa kutokana na sababu mbalimbali za maisha. Injili ya Kristo Mfufuka iwe ni chemchemi ya furaha, imani na faraja. Isaidie kuamsha dhamiri, ili kujikita katika toba na wongofu wa ndani. Kimsingi; imani, matumaini na mapendo ni tunu msingi za Kiinjili zinazopaswa kumwilishwa katika uhalisia wa hija ya maisha ya waamini. Mtakatifu Gaspari del Bufalo kwa kuanzisha Shirika la Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu, C.PP.S. alikuwa ni kielelezo makini cha kujibu kilio cha “Damu Azizi ya Kristo”, kinachoendelea kusikika sehemu mbalimbali za dunia kutokana na umaskini, magonjwa, njaa na upweke hasi unaowanyemelea watu wengi kwa sasa. Mtakatifu Gaspari akafanikiwa kuyamimina maisha yake katika tamaduni mbalimbali duniani, leo hii Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu wako mstari wa mbele katika kusikiliza na kujibu kilio cha damu ya watu wateule na watakatifu wa Mungu. Huu ni utakatifu unaojikita katika sala na Neno la Mungu linalomwilishwa katika uhalisia wa maisha. Leo hii kuna watu wanaoteseka kutokana na sababu mbali mbali; watu wanao ogelea katika upweke hasi; wote hawa wanahitaji mtu wa kusikiliza na kujibu kilio chao. Damu Azizi ya Kristo, iwe ni chemchemi ya: imani, faraja na matumaini kwa wale wote wanaoteseka sehemu mbalimbali za dunia!
Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu wawe ni vyombo na mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Gaspari katika maisha na utume wake. Baba Mtakatifu Francisko analitaka Kanisa kuwa kama Hospitali katika uwanja wa vita, ili kuwaganga na kuwaponya wale waliovunjika na kupondeka moyo, watu wanaoelemewa na mizigo ya maisha. Kimsingi, Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu wawe ni chemchemi ya matumaini kwa wale waliokata tamaa. Watambue kwamba, wameitwa na kutumwa sehemu mbalimbali za dunia ili kutangaza na kushuhudia huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake. Maisha ya Mtakatifu Gaspari ni kielelezo cha maisha yaliyosimikwa katika huruma na upendo wa Mungu unaojionesha kwa namna ya pekee, kwa Kristo Yesu kumwaga Damu yake Azizi kwa ajili ya kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Maadhimisho ya Kumbukizi ya Miaka 70 tangu Gaspari del Bufalo kutangazwa na Mama Kanisa kuwa ni Mtakatifu ni muda wa kumshukuru Mungu kwa zawadi ya utakatifu na ujasiri wa Padre Gaspari del Bufalo. Ikumbukwe kwamba, utakatifu wa maisha ni wito kwa kila mwamini; wito unaopaswa kumwilishwa katika uhalisia wa maisha ya kila mtu. Mtakatifu Gaspari anawahimiza wamisionari wake kuwa ni chemchemi ya utakatifu kama ushuhuda na utambulisho wao, changamoto inayopaswa kuvaliwa njuga, kila siku ya maisha!