Papa akutana na Bi Zuzana Caputová, Rais wa Jamhuri ya Slovakia
Na Angella Rwezaula- Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko Jumamosi tarehe Mosi Juni 2024 amempokea kwa Mkutano Mheshimiwa Zuzana Caputová, Rais wa Jamhuri ya Slovakia, ambaye baadaye alikutana na Kardinali Pietro Parolin, Katibu wa Vatican, akifuatana na na Monsinyo Miroslaw Wachowski, Katibu msaidizi wa Vatican kwa ajili ya Mahusiano na Mataifa na Mashirika ya Kimataifa. Ni katika taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Vyombo vya habari vya Vatican.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo imesema: “Wakati wa mkutano mzuri katika Sekretarieti ya Nchi, “walizungumza juu ya matarajio ya nchi kwa kuzingatia tukio la kusikitisha la kushambuliwa kwa Waziri Mkuu, mabadiliko ya hivi karibuni ya urais na mbinu ya uchaguzi wa Ulaya, wakielezea matumaini kwamba wataimarisha amani na utulivu wa Nchi.”Na zaidi “Mazungumzo yalipoendelea, umakini mkubwa ulitolewa kwa vita huko Ukraine.”
Kubadilishana kwa zawadi
Papa Francisko alimpatia Bi.Zuzana Caputová sanamu ya shaba inayoonesha ua likizaliwa, yenye maandishi: “Amani ni ua dhaifu.” Kwa upande wake, rais alitoa mashine ya kuandika maandishi ya typebraille kwa Papa. Ni kifaa kilichotengenezwa katika nchi ya Ulaya, ambacho kinaruhusu vipofu kuandika kwa mfumo wa Braille kwa haraka zaidi. Rais wa Jamhuri ya Slovakia pia alimpatia Papa divai kutoka mkoa mdogo wa Carpathian na waridi tatu za chuma, ikiwa ni kumbukumbu ya vijana watatu waliofariki katika ajali wakati wakielekea kwenye mkutano wa jimbo.
Waziri Mkuu Fico kuruhusiwa kutoka hospitali
Tarehe 31 Mei 2024 Waziri Mkuu wa Slovakia, Robert Fico, aliruhusiwa kutoka hospitali alikolazwa baada ya shambulio la tarehe 15 Mei 2024. Miriam Lapunikova, mkurugenzi wa hospitali katika mji wa kati wa Banska Bystrica, alitangaza kuwa Fico, “mgonjwa mwenye nidhamu,” amesafirishwa hadi nyumbani kwake Bratislava ambako ataendelea na matibabu yake. Waziri Mkuu huyo alikuwa amejeruhiwa tumboni na mtu aliyempiga risasi alipokuwa akiwasalimia wafuasi wake katika mji wa Handlova, kaskazini-mashariki mwa mji mkuu.