Rais Josè Maria Pereira Neves Akutana na Papa Francisko Mjini Vatican
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa tarehe 14 Juni 2024 alikutana na kuzungumza na Rais José Maria Pereira Neves wa Cape Verde ambaye baadaye alibahatika kukutana na kuzungumza na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican aliyekuwa ameambatana na Askofu mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu mkuu wa Mambo ya Nchi za Nje, Ushirikiano na Mashirika ya Kimataifa.
Katika mazungumzo yao ya faragha, viongozi hawa wawili wamepongeza uhusiano mwema uliopo kati ya Vatican na Cape Verde na baadaye, wamejielekeza zaidi katika masuala ya kijamii, kiuchumi na Kikanisa mintarafu maridhiano ya Mkataba kati ya Vatican na Cape Verde uliotiwa saini kunako mwaka 2014. Baadaye katika mazungumzo yao, viongozi hawa wamejikita zaidi katika hali ya Kimataifa mintarafu: Ulinzi na usalama; vita, kinzani na mipasuko ya kijamii sehemu mbalimbali za dunia; wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji; mifumo mbalimbali ya utumwa mamboleo na biashara ya binadamu na viungo vyake.