Tamko la Vatican katika Mkutano wa Ngazi za Juu kuhusu Ukraine
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Kuanzia tarehe 15-16 Juni 2024, Vatican kwa kukubali mwaliko wa pamoja wa Rais wa Shirikisho la Uswiss, Viola Amherd, na Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelenskyy, walishiriki kama waangalizi katika Mkutano wa Ngazi ya Juu wa Amani huko Ukraine, uliofanyika nchini Uswisi. Mkutano huo uliwakilishwa na Katibu wa Vatican, Kardinali Pietro Parolin, akiandamana na Balozi wa Vatican nchini Uswisi, Askofu Mkuu Martin Krebs, na Monsinyo Paul Butnaru, afisa wa Kitengo cha Mahusiano na Mataifa na Mashirika ya Kimataifa ya Sekretarieti ya Vatican. Sambamba na hali mahususi ya Vatican na nafasi yake kama Mwakilishi wa Kudumu kufuatilia mazoea ya kutotia saini ya matamko ya pamoja, Wajumbe wa Vatican walijizuia kusaini Ujumbe wa mwisho, huku wakionesha kuunga mkono hitimisho la Mkutano huo, kulingana na kile alichotangaza katika hotuba ambayo Kardinali Parolin alitoa wakati wa kikao cha mwisho.
Katika Mkutano huo, Kardinali alitoa hotuba yake akianza kukaribishwa kuitishwa kwa Mkutano huu wa Ngazi ya Juu kuhusu Amani Ukraine, ulioandaliwa kwa pamoja na Uswiss na Ukraine. Ni tukio la umuhimu wa kimataifa, lililotayarishwa kwa uangalifu na Ukraine, ambayo, wakati ikifanya jitihada kubwa za kujilinda kutokana na uchokozi, pia imefanya kazi mfululizo katika nyanja ya kidiplomasia, yenye shauku ya kufikia amani ya haki na ya kudumu. Katika hali ya vita na matokeo yake ya kusikitisha, ni muhimu kamwe kutokata tamaa, bali kuendelea kutafuta njia za kumaliza mzozo huo kwa nia njema, uaminifu na ubunifu. Huu ndio ujumbe ambao Papa Francisko anawasilisha, hasa kwa watawala wa mataifa, pamoja na wito wake unaoendelea wa amani nchini Ukraine.
Ni muhimu kusisitiza kwamba njia pekee inayoweza kupata amani ya kweli, utulivu na haki ni mazungumzo kati ya pande zote zinazohusika. Vatican inaeleza matumaini yake kwamba juhudi za kidiplomasia zinazoendelezwa hivi sasa na Ukraine na kuungwa mkono na nchi nyingi zitaboreshwa, ili kupata matokeo yanayostahili wahanga na ambayo dunia nzima inayatarajia. Kwa mujibu wa asili yake, Vatican inashiriki kama Mtazamaji, ikizingatia hasa heshima ya sheria za kimataifa na masuala ya kibinadamu. Kuhusiana na kipengele cha kwanza, inataka kuthibitisha uhalali wa kanuni ya msingi ya kuheshimu uhuru wa kila nchi na kwa uadilifu wa eneo lake. Vatican inaonesha wasiwasi mkubwa juu ya matokeo mabaya ya kibinadamu na imejitolea hasa kuwezesha urejeshwaji wa watoto makwao na kuhimiza kuachiliwa kwa wafungwa, hasa askari na raia waliojeruhiwa vibaya.
Kuunganishwa kwa watoto na familia zao au walezi wa kisheria lazima iwe jambo kuu kwa wahusika wote, na unyonyaji wowote wa hali yao haukubaliki. Kwa hivyo ni muhimu kwamba kila mikondo inayopatikana iimarishwe ili kuwezesha mchakato huu. Kwa kuongezea, Vatican inashiriki kama mwangalizi katika kazi ya Muungano wa Kimataifa wa kuwarejesha makwao watoto wa Kiukreni kutoka Urusi. Zaidi ya hayo, inadumisha mawasiliano ya moja kwa moja na mamlaka za Ukraine na Urusi kwa lengo la kuimarisha ufanisi wa utaratibu wa dharura ulioundwa kufuatia na ziara ya Kadinali Matteo Zuppi huko Kyiv na Moscow, kwa nia ya kusuluhisha kesi madhubuti. Kuhusiana na wafungwa, raia na wanajeshi, kuna wasiwasi mkubwa juu ya ripoti za mara kwa mara za kutofuata Mikataba ya Geneva. Hasa kuhusu Mkataba wa Nne, ambao unawahusu moja kwa moja raia, na ugumu wa kuunda, pamoja na Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu, Tume ya Pamoja ya Matibabu ambayo inaweza kutathmini hali ya wafungwa wa vita wanaohitaji huduma ya haraka ya matibabu.
Licha ya changamoto zote, Vatican bado imejitolea kudumisha mawasiliano ya mara kwa mara na mamlaka ya Kiukraine na Urussi, na inasalia tayari kusaidia katika utekelezaji wa mipango ya upatanishi ambayo inakubalika kwa pande zote na kunufaisha wale ambao wameathirika. Wakati huo huo, Baraza takatifu linahimiza nchi na wanachama wengine wa jumuiya ya kimataifa kuchunguza njia za kutoa msaada na kuwezesha upatanishi, iwe wa kibinadamu au wa kisiasa. Kwa njia hiyo Kardinali alisisitiza kuwa Vatican inaamini kwamba kwa kuunga mkono juhudi hizi, “tunaweza kusaidia kupata mwafaka na kuhakikisha utekelezaji wa mipangoi hii kwa wakati. Kwa niaba ya Papa Francisko, napenda kuthibitisha ukaribu wake wa kibinafsi kwa watu wa Ukraine wanaoteswa na kujitolea kwake kwa amani bila kuyumbayumba.”