Tafuta

Kwa nini silaha za kuua zinauzwa kwa wale wanaopanga kuleta mateso yasiyoelezeka kwa watu binafsi na jamii? Kwa nini silaha za kuua zinauzwa kwa wale wanaopanga kuleta mateso yasiyoelezeka kwa watu binafsi na jamii?   (ANSA)

Vatican:wakati vita vinaendelea kuna uenezi haramu wa silaha ndogo na nyepesi

Vatican imetoa tamko katika Mkutano wa Nne wa Umoja wa Mataifa wa Kupitia Maendeleo yaliyopatikana katika Utekelezaji wa Mpango wa Hatua ya Kuzuia, Kupambana na Kutokomeza Biashara Haramu ya Silaha Ndogo Ndogo na Nyepesi katika Nyanja zake zote,Jijii New York,Marekani tarehe 19 Juni 2024.

Na Angella Rwezaula- Vatican.

Mwakilishi wa Kudumu wa Vatican katika Umoja wa Mataifa Jijini New York,  Marekani, tarehe 19 Juni 2024, Monsinyo Robert Murphy alitoa tamko la Vatican katika ufunguzi wa Mkutano wa "Nne wa Mapitio (RevCon4) wa Mpango wa Utekelezaji wa Umoja wa Mataifa (PoA) kuhusu Silaha Ndogo Ndogo na Silaha Nyepesi na Chombo cha Kimataifa cha Kufuatilia (ITI).  Awali alisema Vatican inatoa  shukrani na msaada kwa uongozi wao katika mchakato wa mazungumzo. Ni matumaini ya Vatican kwamba: “tutaweza kufikia makubaliano na kushirikiana katika kutafuta kuendeleza upokonyaji silaha na kupatikana kwa amani ya haki.

Wakati vita vinaendelea duniani,matumizi ya silaha ndogo yanaenea

Mwakilishi wa Kudumu wa Vatican aliendelea hasa kubainisha kwamba kwa hakika, wakati ulimwengu unapopitia "vita vya tatu vya dunia vilivyogawanyika vipande vipande," kuenea haramu na matumizi mabaya ya silaha ndogo ndogo na nyepesi kunawakilisha mojawapo ya matishio makubwa zaidi ya usalama katika ngazi ya kitaifa, kikanda na kimataifa. Kila mwaka, makumi ya maelfu ya watu huuawa au kujeruhiwa katika mizozo ambayo hupiganwa hasa kwa "silaha hizi za maangamizi kwa mwendo wa polepole" na katika maeneo yenye uhalifu nje ya maeneo ya migogoro, mara nyingi mikononi mwa makundi yenye silaha na magaidi. Kuongezeka kwa silaha ndogo ndogo na nyepesi kuna matokeo mabaya kwa watu binafsi na jamii, na kuchangia kukosekana kwa utulivu na kuzuia maendeleo yao.

Cha kusikitisha leo hii uwekezaji wa silaha na mapato mengi

Kwa njia hiyo Mwakilishi wa Vatican alisisitiza kuwa cha kusikitisha, leo hii, uwekezaji katika utengenezaji wa silaha ndio unaoleta mapato mengi." Kwa kuwa mwelekeo huu wa kutisha unajumuisha pia silaha ndogo ndogo na silaha nyepesi, Mwakilishi wa Vatican aliomba Mwenyekiti amruhusu  kukumbusha maneno ya Papa Francisko: “Kwa nini silaha za kuua zinauzwa kwa wale wanaopanga kuleta mateso yasiyoelezeka kwa watu binafsi na jamii?  Cha kusikitisha, jibu, kama sisi sote tunavyojua, ni kwa pesa tu: pesa ambazo zimelowa damu, mara nyingi damu isiyo na hatia.” Hata hivyo, uzalishaji na usambazaji wa silaha ndogo ndogo na nyepesi haupaswi kuzingatiwa katika masuala ya kiuchumi tu; pia ni suala la mahangaiko makubwa ya kimaadili na kibinadamu ambayo yanahitaji uangalizi wetu wa haraka na hatua.

Kuna haja ya kutanguliza ulinzi wa maisha ya binadamu

Kwa njia hiyo ujumbe wa Vatican  umejihusisha kikamilifu katika mazungumzo ya RevCon4, ukitanguliza ulinzi wa maisha ya binadamu na kulinda utu wa binadamu, hasa kwa wale walio katika mazingira magumu zaidi. Kuhusiana na hilo Mwakilishi wa kudumu alipenda kumulika mambo mawili ambayo ni muhimu sana kwa ujumbe wake: Kwanza, watoto wanaendelea kuathiriwa kwa njia isiyo sawa na migogoro ya silaha. Silaha ndogo ndogo na nyepesi hutumiwa kwa kawaida kufanya ukiukaji mkubwa dhidi ya watoto, ikiwa ni pamoja na kuajiri, utekaji nyara na vurugu, pia katika muktadha wa mashambulizi dhidi ya shule na hospitali. Kwa hivyo, ujumbe wa Vatican unaamini kuwa maandishi ya RevCon yanapaswa kujumuisha masharti thabiti zaidi kuhusu ulinzi wa mtoto.

Tupambane na biashara haramu ya silaha hizo:wanawake na watoto ni waathirika

Pili, Mwakilishi wa Vatican alisisitiza kuwa: "katika kupambana na athari za biashara haramu ya silaha hizo, Vatican inapenda kusisitiza umuhimu wa kuzingatia mbinu inayoweza kushughulikia ipasavyo mahitaji halisi ya wanawake na watoto wanaoangukia kwenye ukatili huo. Tunaamini kuwa hili linaweza kupatikana kwa kuepuka kutoelewana kwa hali zinazoweza kuhatarisha ulinzi halisi wa waathrika hao,” alihitimisha, Mwakilishi wa Kudumu wa Vatican katika Umoja wa Mataifa.

Tamko la Vatican Kuhusu matumizi ya silaha ndogo ndogo na madhara yake
20 June 2024, 18:06