Vipaumbele Vya Wanawake Wakatoliki: Tunu Msingi za Familia na Utunzaji wa Mazingira
Mama Evaline Malisa Ntenga, - Vatican
Mama Evaline Malisa Ntenga, Rais wa Shirikisho la Umoja wa Wanawake Wakatoliki Kanda ya Afrika ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake Wakatoliki Tanzania, WAWATA, anapenda kushirikisha yale yaliyojiri katika mkutano wa WUCWO uliofanyika kuanzia tarehe 26 Mei hadi tarehe Mosi, Juni 2024 kwa ufupi anazungumzia kuhusu: Dhamiri ya Umoja wa Wanawake Wakatoliki Duniani, Vipaumbele 2023-2027; Mikutano ya kikatiba katika kipindi cha mwaka 2023/24; Mikutano ya Kanda ya Afrika; Tarehe 13 MEI 2024, ilikuwa ni Siku ya Umoja wa Wananwake Wakatoliki Duniani; Mkutano wa Kanda ya Afrika 27 Julai hadi tarehe Mosi, Agosti 2025, Kampala Uganda: Warsha ya WWO mwezi Julai 2024 nchini Tanzania. Vipaumbele vya Bara la Afrika: Tunu msingi za familia sanjari na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Dhamira ya WUCWO: Umoja wa Wanawake Wakatoliki Duniani, WUCWO, “Unión Mundial de las Organizaciones Femeninas Católicas, UMOFC” (WUCWO) ulianzishwa mnamo mwaka 1910 na sasa unawakilisha karibu mashirika 100 ya wanawake Wakatoliki ulimwenguni, wanaofanya kazi katika nchi karibu 80 katika mabara yote ikiwa na hesabu inayokadiriwa kuwa ni wanachama milioni nane (8). Lengo la WUCWO ni kukuza uwepo, ushiriki na uwajibikaji wa wanawake wa Katoliki katika jamii na Kanisa, ili kuwawezesha kutimiza dhamira yao ya uinjilishaji na kufanya kazi kwa maendeleo ya binadamu, haswa katika kuongeza fursa za elimu, kupunguza umaskini na kuendeleza haki za binadamu kuanzia na haki msingi ya kuishi. WUCWO inaunganisha wanawake Wakatoliki ulimwenguni kuwapa sauti kwenye jukwaa la kimataifa. Tangu kuanzishwa kwake, WUCWO imekuwa na hadhi ya kuwa na uwakilishi wa kudumu katika Baraza la Uchumi na Jamii la Umoja wa Mataifa (ECOSOC – Economic & Social Council), Baraza la Haki za Binadamu (Geneva), Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo (FAO), na ni Afisa mshirika wa UNESCO (Paris).
WUCWO inatafiti maswala muhimu ambayo yanaathiri maisha ya wanawake kimataifa na inakuza hadhi ya kila mwanadamu. WUCWO inaratibu shughuli za mashirika ya wanawake Wakatoliki ulimwenguni, ikiwa ni kiungo muhimu kati yao na mtandao wa mashirika ya kimataifa na jamii za Imani mbalimbali. Kupitia wao, WUCWO husaidia kufundisha wale ambao hawana rasilimali au fursa, kuwapatia wahanga wa unyanyasaji na umaskini njia ya kujikimu kwao na watoto wao na inasaidia kuwawezesha kutimiza kazi yao ya uinjilishaji na kufanya kazi kwa maendeleo ya binadamu. WUCWO ni sauti ya wanawake wote ulimwenguni inayotumiwa kufikisha ujumbe wenye kuleta manufaa kwa kila alieumbwa na Mungu. Sisi kama WAWATA kuwa mwanachama wa WUCWO tunapata hiyo fursa ya kuwafikia wengine ama wengine kutufikia sisi kwa nama ya kutangaza Habari za Kristo Yesu mfufuka. VIPAUMBELE 2023-2027: WUCWO itaimarisha, kuendeleza na kupanua Mradi wa Uangalizi wa Masuala ya Unyanyasaji kupitia mradi wa WWO. WUCWO itatetea Uhuru wa kidini: msingi wa njia ya udugu na amani (Frateli tutti 279). Wito wa Toba na Wongofu wa kiikolojia. Utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Tuitikie kwa Imani na kwa ari mpya, safari ya furaha ya upendo ndani ya familia – Umama na Ubaba kadiri ya Wosia wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko “Amoris laetitia” yaani “Furaha ya Upendo ndani ya familia.” Kufanya kazi na Mashirika ya Kimataifa kuboresha sera zinazohusu wakimbizi na Sera za Uhamiaji. Kutoa elimu ili kuwezesha wanawake kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa kazi za Kanisa kama sehemu ya ujenzi wa Kanisa la Kisinodi. Vipaumbele hivi vyote vinatakelezwa kadiri ya Mpangokazi wa WAWATA Taifa katika majimbo yote kuendana na vipaumbele vya eneo mahalia.
MIKUTANO YA KIKATIBA: Katika kipindi cha mwaka 2023/24 WUCWO imefanya mikutano miwili ya kikatiba ambayo mjumbe wa bodi alihudhuria: Septemba 2023 – kwa njia ya mtandao 25 – 28. Huu ni mkutano wa kwanza kwa bodi mpya ya 2023 – 2027. Mkutano huu ulikuwa muhimu kama hatua ya kwanza ya kufamamiana wajumbe waliochaguliwa 2023, kuunda kamati muhimu, maandalizi ya mkutano wa Bodi wa ana kwa ana, kupokea ripoti ya kikundi cha uangalizi wa masuala ya Wanawake Ulimwenguni -WWO, kuanza Shule ya ujenzi wa Kanisa la Kisinodi “School of Synodality.” Mei 2024 – Umefanyika mkutano wa kawaida wa Bodi - Roma Italia 26 Mei hadi 02 Juni. Agenda muhimu: Mkutano na Kardinali Kevin Joseph Farrell, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha. Kardinali Farrell alianza kwa kusema, ‘Hakuna Parokia inaweza kusimama bila WANAWAKE’. Kanisa linatambua wajibu mkubwa wanawake wanafanya kote ulimwenguni. Ni wazi kuwa Paroko yoyote anayeshindwa kufanya kazi na wanawake Parokia yake haiwezi kufikia Malengo. Aliwapongeza WUCWO na mashirika yake kwa kazi kubwa inayofanyika kwenye vipaumbele muhimu vya Baba Mtakatifu Francisko: Hususan katika mchakato wa ujenzi wa Kanisa la Kisinodi, Utunzaji Bora wa Mazingira nyumba ya wote “Laudato si” na Malezi ya Familia na kusisitiza umuhimu wa kuendelea na miradi hiyo yote. Aliongeza, Shule ya ujenzi wa Kanisa la Kisinodi iwe endelevu kwani mwisho wa Maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu mwezi Oktoba 2024 ni mwanzo wa safari ya kutembea kwa pamoja kama Kanisa la Kristo. Kardinali alisisitiza umuhimu wa Wanawake kuhusika kwa karibu katika majiundo ya wanandoa. Kuna kilio kila kona ya dunia yetu leo kwa sababu ya ukosefu wa maandalizi sahihi ya wanandoa kunakopelekea ndoa nyingi kuvunjika zikiwa bado changa na kuwaacha watoto wakiishi kama yatima.
Pamoja na pongezi, Kardinali Farrell aliwaasa Wanawake kote ulimwenguni kuwa na umoja baina yao na kuwa na ushirika pamoja na kushikamana na Kanisa. Maeneo mengi, mashirika ya Wanawake yameshindwa kufikia maalengo kwa sababu ya kukosekana kwa upendo wa kweli baina yao na wakati mwingine ubinafsi na kushindwa kutambua wote wameitwa na Mungu kwa lengo moja tu la kuutangaza ufalme wa Mungu kwa kuanza na wale waliosukumizwa pembezonimwa jamii na wanaoonewa. Tukisoma kitabu cha Mwanzo 1: 26 ‘26 Ndipo Mungu akasema, “Tufanye mtu kwa mfano wetu, kwa sura yetu, wakatawale juu ya samaki wa baharini na ndege wa angani, juu ya mifugo, juu ya dunia yote, na juu ya viumbe wote watambaao juu ya nchi.” 27 Kwa hiyo Mungu akamuumba mtu kwa mfano wake mwenyewe, kwa mfano wa Mungu alimuumba; mwanaume na mwanamke aliwaumba.’ Wakati mwingine tumeshindwa kutimiza malengo kwa sababu ya kuwepo kwa mashindano baina ya wanawake na wanaume. Mungu amemuumba mwanamke kwa sura na mfano wake, vivyo hivyo mwanaume. Mungu amempa mwanamke upendeleo kushiriki na namna ya kipekee kazi ya uumbaji na kuhusika na malezi ya familia kwa ujumla (Watoto anaopewa na Mungu kama zawadi, na yeyote anaekuwa malangoni). Mungu amemuumba mwanamke/mwanaume kukamilishana (complementary for each other). Kumbe kila mmoja ana jukumu, na ili Fumbo la Mwili wa Kristo yaani Kanisa ukamilike, kila mmoja ana wajibu. Warsha ya Sinodi na kupokea taarifa ya kikundi cha uchunguzi wa masuala ya Wanawake Ulimwenguni - WWO na mpango wa kuendelea na mradi Afrika. Wakati wa mkutano, WUCWO iliwezesha warsha na wadau wake, kujadili maendeleo yaliyofikiwa katika Mradi wa WWO, na pia Shule ya Ujenzi wa Kanisa la Kisinodi. Zaidi ya wajumbe 100 wakiwepo wawakilishi wa Bodi ya WUCWO walikutana pamoja katika ofisi za Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha huko San Calisto Roma. Warsha hii ilifanyika mubashara kupitia mitandao yote ya kijamii ya WUCWO na wadau wengi walishiriki kwa njia ya mitandao. Inatia moyo kusikia 60 ya Wanawake takriban 600 walioshiriki dodoso lililoandaliwa na WUCWO kuhusu ushiriki wa Wanawake katika Sinodi wanakiri kushirikishwa katika hatua za awali.
Katika kipindi cha mwaka 2023-2024, WUCWO iliandaa mazungumzo, midahalo na mijadala mbalimbali ili kutoa elimu kuhusu muhtasari ya awali wa Sinodi ya ya XVI ya Maaskofu (Synthesis report), iliandaa mafunzo kwa wawakilishi kutoka nchi zote wanachama juu ya namna bora ya kusikilizana na kutafakari katika Roho kwa lengo la kutembea pamoja Kisinodi. Zaidi ya Wanawake 400 kutoka nchi wanachana walishiriki mdahalo wa Sinodi na kusimulia ushiriki wao katika Sinodi, changamoto walizokutana nazo na nini maoni yao kuhusu ushirikishwaji wa wanawake katika Parokia zetu. Taarifa ya midahalo yote itawakilishwa kwa Sekretarieti kuu ya Sinodi kabla ya kilele cha Maadhimisho ya Sinodi hapo Oktoba 2024. Kuwapokea Wajumbe wa Mashirika mapya: Tunamshukuru Mungu, WUCWO inaendelea kukua. Mashirikia 3 yaliomba na yamepokelewa wakati wa mkutano, na shirika moja kuomba kuwa mwanachama kamili. Mashirkia haya yatathibitishwa kwenye mkutano mkuu (GA) 2027. Mashirika yaliyopokelewa: Catholic Women’s League (Jamaica) kama mwanachama kamili. ASE – Accion Social Empresarial (Hispania) kama mwanachama mshiriki. D.VA – Associazione Donne in Vaticano “Wanawake wanaofanya kazi mjini Vatican kama wanachama washiriki. Katholische Frauenbewegung Österreichs K.F.B.O. (Austria), wameomba kuwa mwanachama kamili baada ya kuwa mwanachama mshirika kwa muda mrefu. Kupokea wajumbe wapya wa Bodi kutoka mashirika rafiki – AMSIF, TCAS, Shirikisho la Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki Kimataifa, Caritas Internationalis. Kupiga kura na kuridhia nchi mwenyeji wa Mkutano Mkuu (GA) 2027.
MIKUTANO YA KANDA YA AFRIKA. Kanda ya Afrika ilifanya mikutano 2 na mikutano 3 ya Kamati ya Maandalizi ya Mkutano wa Kanda ya Afrika “Regional conference.” Vipaumbele kwa kanda ya Afrika ni vile vilivyoridhiwa na Mkutano wa Assisi, Italia. Kwa kauli moja, Kanda ya Afrika iliomba kuweka mkazo katika malezi ya familia/majiundo ya wanandoa. Kazi ya kusilikiza vilio vya mwanamke wa Kiafrika kupitia dodoso iliendelea toka mwezi Julai 2023 lengo kuu likiwa ni kuendelea kukuza mtandao wa wanaharakati wa kupiga vita aina zote za: dhuluma, unyanyasaji na biashara haramu ya binadamu na viungo vyake. Maeneo mengi mradi huu ilisua sua kwa sababu mbalimbali, hasa kukosekana kwa fedha. Hata hivyo WUCWO inatoa Shukrani za dhati kwa kila alieguswa na kushiriki kazi hii muhimu. Huu ni mradi wa kudumu. WWO inategemea kufanya Warsha ya pili nchini Tanzania mwezi Julai, Uganda mwezi Septemba na baadae Malawi na Zambia. Lengo ni kuhakikisha mradi huu unatekelezwa na kufikia lengo la kuwa sauti ya wasio na sauti. SIKU YA WUCWO 13 MEI 2024: Umoja wa Wananwake Wakatoliki Duniani (WUCWO) huadhimisha /kusherehekea siku hii kwa namna ya kipekee ikiwa ni Siku kuu ya Somo wetu Mama Bikira Maria, 13 Mei kila mwaka. Kwa Tanzania, kwa sababu za kimazingira hasa tukizingatia mwezi Mei ni kipindi cha Masika na wengi wanakuwa mashambani, Sikukuu ya Mama Bikira Maria huadhimishwa Kijimbo mwezi Septemba. Mwongozo wa Liturujia maalum na tafakari kwa mwaka huu imeandaliwa na Kanda ya Afrika Ikiwa na kichwa: “Kanisa la Sinodi katika mwanga wa Laudato si.” Tafakari ya Kanisa la Sinodi katika mwanga wa Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote” unatukumbusha mahusiano yetu na Mungu, wanadamu wengine na viumbe vyote vya Mungu. Viongozi wa kanda na majimbo wanaombwa kufanya maandalizi mapema ili kuwezesha WAWATA wengi kushiriki. WUCWO imeyaomba mashiriki yote kushiiki katika kampeni ya kutafuta fedha kwa ajili ya kuwezesha miradi mbalimbali inayofanywa na umoja huu.
MKUTANO WA KANDA YA AFRIKA 27 JULAI – 01 AUG 2025, KAMPALA UGANDA: Mkutano wa Kanda ya Afrika utafanyika Mjini Kampala, nchini Uganda kuanzia tarehe 27 Julai 2025 hadi tarehe 1 Agosti 2025. Maandalizi yalianza Januari 2024 baaada ya kuridhiwa na Baraza la Maaskofu Katoliki la Uganda. Mkutano huu hufanyika kila baada ya miaka miwili, mmoja ukifanyika sambamba na Mkutano mkuu (GA). Kauli mbiu ya Mkutano wa Kanda ya Afrika Jijini Kampala utakuwa na maudhui ya kipaumbele cha WUCWO kuhusu familia. Tuitikie kwa Imani na kwa ari mpya, safari ya furaha ya upendo ndani ya familia – Umama na Ubaba kadiri ya Wosia wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko: “Amoris laetitia” yaani “Furaha ya Upendo ndani ya familia.” Kwa moyo wa unyenyekevu, napenda kutumia fursa hii kuwaalika Wanawake Wakatoliki wote kuungana nami na mashirika ya WUCWO kujiandaa kushiriki kwa lengo la kuendelea kujifunza na kufanya hija kule Uganda. Tuendelee kuuombea mkutano huu na kuwaombea Wanawake wote wa Afrika ili tuwe kweli wajenzi wa amani ya Ulimwengu. Kwa namna ya pekee Rais wa WUCWO Mama Monica Santamarina atashiriki mkutano huu. Karibuni nyote. WARSHA YA WWO, JULAI 2024 – TANZANIA: Kwa mara nyingine, kikundi cha uangalizi wa masuala ya Wanawake Ulimwenguni WWO kinatarajia kufanya Warsha ya pili nchini Tanzania katikati ya mwezi Julai 2024. Kwa namna ya pekee, Jimbo kuu la Dar es Salaam wanaombwa kujiandaa kupokea ugeni kama walivyofanya mwaka 2023. Ratiba kamili itafuata. UTEKELEZAJI WA VIPAUMBELE VYWA WUCWO: Wajumbe wa Bodi walipitia kwa upya vipaumbele vya kamati na makundi mbalimbali na kuandaa mpango wa utekelezaji. Kati ya vipaumbele vinavyopewa uzito zaidi ni pamoja na Familia, Ikolojia, Shule ya Ujenzi wa Kanisa la Kisinodi; Wakimbizi na Wahamiaji. Baada ya kuandaa mpango kazi, wajumbe walipata nafasi ya kufanya hija katika Kanisa kuu la Mtakatifu Yohane wa Laterano wakimshukuru Mungu na kujikabidhisha kwa Mwenyezi Mungu ili waweze kutekeleza utume wao kama wabatizwa.
Imewasilishwa na: Mama Evaline Malisa Ntenga. Juni, 2024.