Ziara ya Papa Francisko katika Manispaa ya Roma Juni 10 Juni!
Osservatore Romano
Ofisi ya Waandishi wa Habari ya Vatican Jumantano tarehe 5 Juni 2024 ilichapishwa ratiba iliyotayarishwa na Nyumba ya Kipapa kuhusu ziara ambayo Baba Mtakatifu atafanya kwenye Manispaa ya Jiji la Roma mnamo Jumatatu tarehe 10 Juni 2024. Hii ilikuwa imetangazwa mwezi mmoja uliopita, na ziara hiyo itakayochukua takribani muda wa saa mbili. Baba Mtakatifu Francisko atawasili saa tatu asubuhi kwa gari kwenye kilima cha Roma, ambapo atakaribishwa na meya wa Jiji la Roma, Bwana Roberto Gualtieri. Mazungumzo ya faragha kati ya hao wawili yatafanyika katika Ikulu ya Seneti kwenye ofisi ya meya.
Kisha akipita kwenye Ukumbi, Askofu wa Roma atasalimia wajumbe wa Sekretarieti ya Meya. Kisha katika Ukumbi wa Bendera atasaini “Kitabu cha Dhahabu cha Manispaa”. Baadaye, kutafanyika kikao na Madiwani na viongozi wengine walioalikwa katika Ukumbi wa Giulio Cesare, ambapo atatoa pia hotuba yake, ikifuatiwa na ubadilishanaji wa zawadi.
Hatimaye, Baba Mtakatifu Francisko na Meya wa mji wataangalia kutoka Balconi ya Jumba la Seneti ili kuwasalimu wananchi wa Roma watakaokuwa wamekusanyika katika Uwanja wa ikulu ya Manispaa ya Roma. Mara baada ya kurejea katika Ukumbi wa Giulio Cesare, Papa na Gualtieri watasimama mbele ya ubao wa kuadhimisha ziara hiyo. Baadaye, wakivuka Ukumbi wa “Laudato si',” wataelekea Ukumbi wa Protomoteca kwa mkutano mfupi na wafanyakazi wa manispaa. Kwa karibu saa 5.00 kupitia mlango wa Vignola, Baba Mtakatifu anatarajia kuondoka kurejea mjini Vatican.