Ask.Caccia:lazima kuimarisha ushirikiano mzuri unaovuka mipaka na itikadi
Na Angella Rwezaula- Vatican.
Katika Tamko la Mwakilishi wa Kudumu wa Vatican katika Umoja wa Mataifa, wakati wa Hotuba yake katika Jukwaa la kisiasa la Ngazi za juu kuhusu “Maendeleo endelevu,” lililofanyika tarehe 17 Julai 2024, huko Marekani, Askofu Mkuu Gabriele Caccia akianza alianza kusema kuwa: “Katika hotuba yake kwa Baraza Kuu la 2015, Papa Francisko aliita kupitishwa kwa Ajenda ya 2030, “ishara muhimu ya matumaini.” Ajenda hii inajumuisha matarajio ya pamoja ya ulimwengu ambamo utu wa asili, uliopewa na Mwenyezi Mungu kwa kila mtu, binadamu anaimarishwa, kupitia lengo kuu la kutokomeza umaskini na njaa katika aina na vipimo vyake vyote.
Ahadi ya Mataifa kutelekeza SDGS ifikapo 2030
Ahadi ya Mataifa kutekeleza Ajenda hii na kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) ifikapo mwaka 2030 ilithibitishwa tena katika Mkutano wa SDG uliofanyika mnamo 2023. Mkutano ujao wa kilele wa “Wakati Ujao” unatoa fursa ya kutafakari juu ya hatua iliyofikiwa kuelekea kufikiwa kwa SDGs na kurekebisha juhudi kwa kuzingatia changamoto mpya. Ingawa hatua kubwa zimepigwa, bado kuna mengi ya kutekelezwa. “Ni muhimu kwamba juhudi ziimarishwe na umakini uelekezwe katika jinsi ya kufikia maendeleo fungamani ya binadamu kwa wote.” Alisema Askofu Mkuu Caccia
Mikutano ijayo itumike kuthibitisha kanuni za msingi
Mwakilishi wa Kudumu wa Vatican alibanisha kuwa “ni uzembe kudhani kwamba hali ya sasa inaruhusu hali ya kuridhika au mwelekeo wa kupotoka kutoka kwa ahadi ambazo zimefanywa. Mkutano wa kilele wa siku za usoni lazima utumike kama wakati muhimu wa kuthibitisha kanuni za kimsingi zinazounga mkono juhudi za pamoja za jumuiya ya kimataifa: kukuza utu wa binadamu, kutafuta manufaa ya wote, na usimamizi wa sayari yetu. Haya yanapaswa kuongoza matendo na sera zetu kwa nia ya kufikia jamii endelevu zaidi, yenye haki na amani.”
Tutapata suluhisho ikiwa tutatenda pamoja
Papa Francisko ameonya mara kwa mara kwamba: “wakati wa kutafuta suluhisho za kimataifa unazidi kuyoyoma. Tunaweza kupata masuluhisho yanayofaa ikiwa tu tutatenda pamoja na kukubaliana.” Askofu Mkuu Caccia alisema: “Maneno haya yanasikika kwa kina katika muktadha wa mkutano wa leo na hasa kwa kuzingatia changamoto kubwa na zinazoendelea tunazokabiliana nazo, ikiwa ni pamoja na umaskini, ambayo ni changamoto kubwa kuliko zote, njaa, mabadiliko ya Tabianchi na migogoro. Ili kukabiliana na changamoto hizi, ni muhimu kutekeleza hatua za ushirikiano na za pamoja, kuimarisha ushirikiano wa kimataifa, kuimarisha ushirikiano wa pande nyingi, na ushirikiano mzuri unaovuka mipaka na itikadi.
Mikutano ya wakati ujao haifai kutayarisha upya ajenda ya 2030
Askofu Mkuu Caccia vile vile alisema kuwa “Mkutano Mkuu kuhusu “Wakati Ujao” haufai kutayarisha upya Ajenda ya 2030. Badala yake, ni lazima itumike kuthibitisha upya mfumo elekezi wa dhamira ya pamoja iliyowekwa katika Ajenda ya 2030, yaani kwa watu, sayari, ustawi, amani na ushirikiano. Uendelezaji wa Ajenda lazima uharakishwe kwa moyo wa mshikamano na kwa azimio la kuleta mustakabali endelevu na wenye mafanikio kwa wote,”Alihitimisha.