Askofu Mkuu Ante Jozić, Balozi wa Vatican Nchini Georgia Na Armenia
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko amemteua Askofu mkuu Ante Jozić, kuwa Balozi mpya wa Vatican nchini Georgia na Armenia. Kabla ya uteuzi huu Askofu mkuu Ante Jozić, alikuwa ni Balozi wa Vatican nchini Belarus. Itakumbukwa kwamba, Askofu mkuu Ante Jozić alizaliwa tarehe 16 Januari 1967 huko Trilj, nchini Croatia. Baada ya masomo na majiundo yake ya kikasisi, tarehe 28 Juni 1992 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre kwa ajili ya Jimbo kuu Katoliki la Split-Makarska. Askofu mkuu Ante Jozić, alijiendeleza zaidi katika masomo ya Sheria, Kanuni na Taratibu za Kanisa na kujipatia Shahada ya Uzamivu katika Sheria za Kanisa. Tarehe 1 Julai 1999 akaanza utume wa kidiplomasia mjini Vatican.
Katika kipindi chote hiki, amewahi kufanya utume wake kwenye Ofisi za Ubalozi wa Vatican huko: India, Urusi na Ufilippini. Kwa miaka 10 akiwa Hong Kong, alipewa kazi maalum ya kustadi uhusiano kati ya China na Vatican kama sehemu ya mchakato wa ujenzi wa mahusiano ya kidiplomasia kati ya nchi hizi mbili kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya pande hizi mbili. Tarehe 2 Februari 2019, Baba Mtakatifu Francisko akamteuwa kuwa Balozi wa Vatican nchini Pwani ya Pembe. Tarehe 7 Aprili 2019 akiwa nchini Croatia akapata ajali mbaya ya gari na kulazwa hospitalini huko nchini Croatia.
Baada ya matibabu ya kina, tarehe 20 Juni 2019 akaruhusiwa kurejea nyumbani kwao. Tarehe 22 Januari 2020 akakutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko mjini Vatican. Tarehe 21 Mei 2020, Baba Mtakatifu Francisko akamteuwa kuwa ni Balozi wa Vatican nchini Belarus na kuwekwa wakfu tarehe 16 Septemba 2020 na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican akisaidiana na Askofu mkuu Marin Barisic wa Jimbo kuu Katoliki la Split-Makarska. Hii ni nchi ambayo ilianzisha uhusiano wa kidiplomasia na Vatican hapo tarehe 11 Novemba 1992.