Askofu Mkuu Julien Kaboré Balozi Mpya wa Vatican Nchini Ghana
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko tarehe 29 Juni 2024 amemteuwa Monsinyo Julien Kaboré kuwa Balozi mpya wa Vatican nchini Ghana na wakati huo huo kumpandisha hadhi na kuwa ni Askofu mkuu. Itakumbukwa kwamba, Askofu mkuu Mteule Julien Kaboré alizaliwa tarehe 18 Juni 1968 huko Zorgho, nchini Burkina Faso. Baada ya malezi na majiundo yake ya Kipadre, tarehe 8 Julai 1995 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre kwa ajili ya Jimbo Katoliki la Koupèla, lililoko nchini Burkina Faso.
Tarehe Mosi, Julai 2004 alianza utume wake katika diplomasia ya Vatican na hivyo kubahatika kutekeleza utume wake katika ngazi mbalimbali nchini: Kenya, Papua New Guinea, Visiwa vya Solomon; Costa Rica, Korea na Mongolia, Croatia, Trinidad na Tobago, Ufilippin na hatimaye, Ireland. Katika maadhimisho ya Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo Miamba wa imani, tarehe 29 Juni 2024, Baba Mtakatifu Francisko akamteuwa kuwa Balozi mpya wa Vatican nchini Ghana na kumpandisha hadhi kuwa ni Askofu mkuu.