Julai 3,Kard.Rugambwa atavikwa Pallia takatifu katika Jimbo Kuu la Tabora!
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Katika fursa ya siku kuu ya Mtakatifu Thomas Mtume, Jimbo Kuu Katoliki la Tabora nchini Tanzania, litakuwa na maadhimisho ya kupewa Pallia takatifu kwa Askofu Mkuu, Kardinali Protase Rugambwa, mara baada ya kukabidhiwa kutoka mikononi mwa Baba Mtakatifu Francisko, tarehe 29 Juni 2024, katika Siku Kuu ya Watakatifu Petro na Paulo, katika Maadhimisho ya Misa Takatifu yaliyofanyika katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Sherehe hizo ziliwaona maelfu ya waamini kuanzia: Makardinali, Maaskofu wakuu, maaskofu, mapadre, mashemasi, watawa kike na kiume na waamini watu wa Mungu.
Ilikuwa ni mnamo tarehe 12 Januari 2015 ambapo Baba Mtakatifu Francisko alitamka kwamba, tangu wakati huo, Maaskofu wakuu watakuwa wanashiriki katika Ibada ya Misa takatifu kwa ajili ya kubariki Pallia takatifu kila mwaka ifikapo tarehe 29 Juni, Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo Mtume wa Watu lakini Pallia takatifu watavikwa na Mabalozi wa Vatican katika chi husika kadiri ya nafasi zao. Na katika muktadha huo, ambapo nchini Tanzania, tarehe 3 Julai katika Siku Kuu ya Mtakatifu Thomas Mtume, Balozi wa Vatican Nchini Tanzania, Askofu mkuu Angelo Accattino atamvika Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu katoliki, Tabora Pallia hiyo.
Lengo kuu la mabadiliko haya ni kuwawezesha watu wa Mungu kutoka katika Makanisa mahalia kushiriki kikamilifu katika maadhimisho haya adhimu katika maisha, historia na utume wa Kanisa mahalia. Pili, ni kuendelea kuimarisha mchakato wa unafsishaji wa “dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa.” Kwa njia hiyo msikose kufuatilia tukio hilo la kupewa Palia kwa Kardinali Rugambwa katika Jimbo Kuu lake.
Mara baada ya misa ilifuatia afla ya kumpongeza Kardinali Rugambwa iliyofanyika katika Chuo Kikuu cha Kipapa la Urbaniana. Wakati wa sherehe zikiliendelea Vatican ilizungumza na Askofu Mkuu Mstaafu Paulo Luzoka na mapadre kadhaa na wengine wageni waliokuwapo. Ukibonyeza hapa utasikiliza yaliyojiri:
Ikumbukwe Baba Mtakatifu Francisko tarehe 13 Aprili 2023 alimteuwa Askofu mkuu Protase Rugambwa kuwa Askofu mkuu mwandamizi mwenye haki ya kurithi Jimbo kuu la Tabora, Tanzania na tarehe 9 Julai 2023 akamteuwa kuwa ni Kardinali wa tatu kutoka nchini Tanzania na kusimikwa rasmi tarehe 30 Septemba 2023. Kardinali Protase Rugambwa, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Tabora akasimkwa rasmi tarehe 10 Novemba 2023 na hivyo kuchukua nafasi ya Askofu mkuu Mstaafu Paulo Runangaza Ruzoka wa Jimbo kuu la Tabora. Ni katika muktadha huu, Kardinali Protase Rugambwa, Dominika tarehe 18 Februari 2024, alikabidhiwa Kanisa la “Santa Maria in Montesanto”, yaani Mtakatifu Maria wa Montesano lililoko kwenye Barabara la Babuino, namba 198, jijini Roma, kuashiria kwamba, Kardinali Rugambwa anakuwa sehemu ya Wakleri wa Roma, wanaounda Baraza la Makardinali lenye jukumu la kumsaidia Khalifa wa Mtakatifu Petro katika shughuli zake za kichungaji kama Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Roma.