Balaa la Njaa, Umaskini Na Deni Kubwa ni Hatari Kwa Maendeleo
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Binadamu Ifikapo mwaka 2030 ni mchakato wa Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba, inajizatiti katika kutokomeza umaskini, baa la njaa na magonjwa duniani. Watu wanapaswa kupatiwa elimu bora, kwa kuhakikisha usawa wa kijinsia pamoja na uwezeshaji wa wanawake na wasichana wote. Jumuiya ya Kimataifa inataka kuhakikisha kwamba, kunakuwepo na upatikanaji wa maji safi na salama; nishati mbadala kwa gharama nafuu pamoja na uwepo wa mipango bora ya miji na makazi ya watu, ili kudumisha usalama na upatikanaji wa maendeleo fungamani ya binadamu. Jumuiya ya Kimataifa haina budi kujifunga kibwebwe kulinda mazingira nyumba ya wote pamoja na kudumisha amani duniani! Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Binadamu kufikia Mwaka 2030 yalipaswa kugharimiwa na Taasisi mbalimbali za fedha Kimataifa pamoja na kufuta madeni makubwa yanayoendelea kukwamisha mchakato wa maendeleo fungamani ya binadamu kwa Nchi changa zaidi duniani!
Changamoto kubwa iliyoko mbele ya Jumuiya ya Kimataifa ni kilio cha Dunia Mama kutokana na uharibifu mkubwa wa mazingira pamoja na kusikiliza kilio cha maskini duniani, ambao kimsingi ndiyo waathirika wakuu wa mabadiliko ya tabianchi. Amana na utajiri kutoka kwa watu mbalimbali duniani, visaidie kukoleza maisha: kiroho na kimwili. Waamini wa dini mbalimbali duniani, wanaweza kushiriki kikamilifu katika kujibu kilio cha maskini duniani; watu wanaohitaji chakula bora, maji safi na salama, huduma makini ya afya na elimu pamoja na makazi bora zaidi ya kuishi. Muda unazidi kuyoyoma kwa kasi, kumbe, Jumuiya ya Kimataifa haina budi kutekeleza kwa haraka sera na mikakati ya Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Binadamu ifikapo mwaka 2030. Umoja na mshikamano wa dhati ni mambo msingi katika utekelezaji wa malengo haya kwa vitendo. Watu kutoka katika makundi na medani mbalimbali za maisha wanapaswa kushirikishwa katika utekelezaji wake. Kipindi kirefu cha watu kuwekwa karantini, kuporomoka kwa vitega uchumi na uzalishaji; ukosefu wa fursa za ajira na mambo mengine kama haya, yanaendelea kuchangia kuporomoka kwa ukuaji wa uchumi kitaifa na kimataifa.
Ni hakika kwamba, watu wengi kutoka katika Nchi zinazoendelea duniani, wanaendelea kuathirika sana. Huu ni wakati wa kusimama kidete kulinda maisha ya watu, kwa kuangalia uwezekano wa kufuta madeni makubwa kutoka katika Nchi zinazoendelea duniani, madeni ambayo kwa sasa yamekuwa ni mzigo mzito usioweza kubebeka hata kidogo. Nchi changa zenye madeni makubwa, HIPC, pamoja na Mpango Mkakati wa Nafuu ya Deni la Nje, MDRI, ni ushuhuda kwamba, Jumuiya ya Kimataifa inaweza kutenda kwa dhati pale inapotakiwa. Huu ni wakati wa kuongeza juhudi kama hizi, kwa kuhakikisha kwamba, madeni ya nje ambayo yamekuwa ni mzigo mzito, yanapunguzwa na kama si kufutwa kabisa, ili kutoa nafuu katika sera na mipango ya Nchi Zinazoendelea duniani. Ni katika muktadha huu, Askofu mkuu Gabriele Giordano Caccia, Mwakilishi wa Kudumu wa Vatican kwenye Makao makuu ya Umoja wa Mataifa, Jijini New York, Marekani anasema, umaskini, baa la njaa na deni kubwa la nje ni hatari sana kwa ustawi, maendeleo na mafanikio katika Nchi changa duniani na kwamba, hivi ni vikwazo vikuu katika kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Binadamu ifikapo mwaka 2030.
Askofu mkuu Gabriele Giordano Caccia alikuwa akichangia kwenye Jukwaa la Uchumi na Siasa na kwamba athari zake zimejipenyeza hata katika mfumio wa fedha Kimataifa. Badala ya kuwekeza kwenye vitega uchumi, sera na mikakati ya maendeleo, sehemu kubwa ya mapato ya Nchi changa duniani inatumika kwa ajili ya kulipia deni la nje, ambalo linaendelea kuongezeka kiasi cha kugumisha maisha ya watu wengi katika Nchi changa duniani. Matokeo yake ni mipasuko ya kijamii na kisiasa inayoendelea kujionesha sehemu mbalimbali za dunia. Leo hii, balaa njaa na utapiamlo wa kutisha, athari za myumbo wa uchumi kitaifa na Kimataifa, athari za mabadiliko ya tabianchi, vita, machafuko wa kisiasa ni mambo ambayo yanaendelea kukwamisha juhudi za kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Binadamu Ifikapo mwaka 2030. Kanisa Katoliki kwa kupitia taasisi zake mbalimbali litaendelea kupambana na baa la umaskini na njaa, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu katika ujumla wake.