Tafuta

2024.07.04 Mkutano Mkuu wa CXVII wa Baraza la Maaskofu nchini Colombia. 2024.07.04 Mkutano Mkuu wa CXVII wa Baraza la Maaskofu nchini Colombia.  (foto © Agenzia Fides)

Colombia,Kard.Tagle:Utume wa Kikristo ni ukweli unaobadilika!

Katika maadhimisho ya kumbukizi ya miaka 100 ya Kongamano la kwanza la Kimisionari Kitaifa (1924 -2024)nchini Colombia,Kardinali Tagle alisema:“Huu ni wakati wa kumshukuru Mungu wetu mwenye rehema,kusikia upyaisho wa wito wa utume katika wakati wetu na kujibu kwa ukarimu,ujasiri na ubunifu.”

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Kardinali Luis Antonio G. Tagle, Mkuu wa Baraza la Kipapa la Kitengo cha  Uinjilishaji wa Kwanza na Makanisa mapya maalum alishiriki ufunguzi wa Kongamano la XIII la Kitaifa la Kimisionari lililoandaliwa na Mashirika ya Kimisionari ya Kipapa (PMS) na katika Mkutano Mkuu wa Baraza la Maaskofu nchini  Colombia (Cec) uliohitimishwa Jumatatu tarehe 8 Julai 2024 huko Bogotà. Akitoa hotuba yake Kardinali Tagle aliakisi umuhimu wa tukio hilo la kuadhimisha Miaka 100 ya Kongamano la kwanza la kimisionari kitaifa duniani, lililofanyika nchini Colombia mnamo mwaka 1924.  Kwa kuunganishwa na kauli mbiu ya Kongamano hilo: “Mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalemu, katika Uyahudi wote na Samaria na hata mwisho wa dunia” (Mdo 1:8), Kardinali Tagle kwa kuongozwa naye  mada ya ‘Mitume wa Watu katika Kanisa mahalia’ alilenga hasa ufuasi wa kimisionari, akisisitiza kwamba utume wa Kikristo ni ukweli wenye nguvu unaomaanisha harakati na kutoka kuelekea watu na mahali popote pale.

Maadhimisho ya miaka 100 ya Kongamano la Kimisionari nchini Colombia
Maadhimisho ya miaka 100 ya Kongamano la Kimisionari nchini Colombia

"Kwenda kwa Yesu, kukaa na Yesu na kwenda kwa wengine kushirikisha Yesu. Ni harakati inayoendelea. Hii inafanya Ukristo kuwa wa nguvu na wa kusisimua. Ni kubaki daima na daima kusonga mbele,” aliwambia Kardinali Tagle washiriki zaidi ya 1,000 waliokusanyika katika  Chuo cha Kipapa cha  Javeriana katika mji  mkuu huko Bogota. “Katika tamaduni nyingi, maisha mara nyingi huoneshwa kama hija. Kila mtu hutembea, huanguka, huinuka, hukimbia, hutambaa, hugeuka kulia au kushoto, au huzunguka ili kufikia lengo. Wengine hukata tamaa na kuacha kusonga mbele. Lakini hakuna mtu anayekwenda Hija peke yake.” Alisisitiza Kardinali Tagle katika hotuba yake kuanzia na wazo kwamba sisi sote ni mahujaji katika maisha haya na kwamba uinjilishaji unafanyika katika muktadha wa hija hii ya pamoja.  “Tunatembea kwenye njia zilizopitwa na vizazi vilivyopita. Kwa hiyo tuache tuunde njia mpya na watu wa kizazi chetu. Nyayo zetu leo ​​ni urithi wetu kwa mahujaji wa siku zijazo.”

Bila matumaini hakuna hija

Hija inazungumza juu ya matumaini. Bila matumaini hakuna Hija, lakini ni harakati zisizo na lengo. Kila Mkristo ameitwa kushiriki katika utume wa kueneza Injili, si kama mtaalamu aliyezoezwa, bali kama mtu anayeshiriki habari njema kwa kawaida. Uinjilishaji lazima uwe upanuzi wa uzoefu wa kibinafsi wa mabadiliko. Kardinali Tagle alipenda kukumbusha kuwa Baba Mtakatifu Francisko anasema, Wakristo wote wamealikwa kushiriki kikamilifu katika uinjilishaji. Zaidi ya hayo, mazungumzo ya kawaida yanaweza kueleweka kama mkutano wa wamisionari. Kushiriki habari njema ya Injili hakuhitaji mafunzo ya hali ya juu, bali nia ya kueleza yale ambayo umepitia na uzoefu. Kadhali alitaka kufanya tafakari tofauti juu ya utamadunisho wa Injili, akikumbuka kwamba “neema hutangulia utamaduni, na zawadi ya Mungu inakuwa mwili katika utamaduni wa wale wanaoipokea (EG 115). Kila utamaduni una uwezo wa kuimarisha uinjilishaji ikiwa uko wazi kwa mabadiliko na ushirika na tamaduni zingine.”

Tamaduni ambazo Kanisa lazima iingilie kati 

Zaidi ya hayo katika hitimisho la hotuba ya Kardinali Tagle aliwasilisha mifano kadhaa ya tamaduni ambazo Kanisa lazima iingiliane kati: “Kwanza kabisa, tamaduni za watu wa kiasili katika sehemu mbalimbali za dunia. Hisia zao za jumuiya na maelewano na uumbaji ni muhimu ili kutakasa utamaduni mkuu wa ubinafsi, utumiaji ovyo na upotevu. Pili, “kutoka katika Sinodi ya Vijana ya mnamo 2018, tunakutana na tamaduni za vijana wa siku hizi ambazo Kanisa linapaswa kutembea nao na kujifunza kutoka kwao. Tamaduni za vijana zinaonesha mabadiliko ya tamaduni za familia katika enzi yetu ya kisasa. Tatu, tunawezaje kupuuza utamaduni unaotokana na mapinduzi ya kidijitali, mtandao ukiwa kila mahali, vihisi vinavyozidi kuwa vidogo na vyenye nguvu zaidi, Akili mnemba na kujifunza kwa mashine? ... Tunapoingia katika utamaduni wa akili mnemba, uinjilishaji unaweza kuchukua namna ya kuamsha aina nyingine za akili. Nne, ninatoa msisitizo kwaajili ya kuwa na utamaduni wa watu wenye ulemavu na uwezo tofauti. Kuwasiliana nao kunahitaji kujifunza lugha mpya na kukuza hisia. Tano, kuna hija ya ajabu inayoitwa uhamiaji wa kulazimishwa, mada iliyo karibu sana na moyo wa Papa Francisko:” Kardinali Tagle alisisitiza.

Mkutano Mkuu wa CXVII wa Baraza la Maaskofu nchini Colombia Julai 2024
Mkutano Mkuu wa CXVII wa Baraza la Maaskofu nchini Colombia Julai 2024

Kanisa kiukweli ni la watu watakatifu wenye nyuso nyingi

Katika hotuba yake Kardinali Tagle hakokosa kutoa mifano hai ya historia ambapo katika mkutano huo alisimumulia  mwanamke mmoja Mfilipino ambaye anafanya kazi kama yaya katika familia moja ya Kiitaliano kwa kuwapeleka watoto wao katika shule nzuri nchini Ufilipino. Kardinali alisema: “Mwanamke huyo aliniambia: ‘Ninapowatunza wale watoto wawili wazuri wa Italia ninawahisi kana kwamba ni watoto wangu. Ninawapa upendo uleule nilio nao kwa watoto wangu.' Kwa kuongeza alisema" Watoto wawili wa Kiitaliano na wale waliobaki Ufilipino wamebahatika kuwa na mama mmoja mmisionari ndani yake. Kanisa, kiukweli ni la watu watakatifu wenye nyuso nyingi.” Katika maandalizi ya Kongamano la XIII la Kitaifa la Kimisionari, makongamano manne ya awali yalifanyika mnamo mwaka 2022 yaliyoandaliwa na Tume ya Maaskofu ya Utume wa Baraza la Maaskofu wa Colombia (CEC), Mashirika ya Kimisionari ya Kipapa (PMS) na Baraza la Kitaifa la Wamisionari (CONAMI).

Hotuba ya Kardinali Tagle nchini Colombia
11 July 2024, 15:38