Tarehe 9 Julai 2024, Sekretarieti kuu ya Sinodi za Maaskofu imechapisha “Hati ya Kutendea Kazi: Instrumentum laboris”, Tarehe 9 Julai 2024, Sekretarieti kuu ya Sinodi za Maaskofu imechapisha “Hati ya Kutendea Kazi: Instrumentum laboris”,   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Hati ya Kutendea Kazi Sinodi ya XVI ya Maaskofu 4-27 Oktoba 2024

Tarehe 9 Julai 2024, Sekretarieti kuu ya Sinodi za Maaskofu imechapisha “Hati ya Kutendea Kazi: Instrumentum laboris”, kama sehemu ya mchakato wa Maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu iliyozinduliwa kunako mwaka 2021, kama sehemu ya ujenzi wa Kanisa la Kisinodi linalowashirikisha waamini katika maisha na utume wake; Kanisa ambalo liko karibu zaidi na waamini wake; linalowawezesha waamini kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wake.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu yananogeshwa na kauli mbiu “Kwa Ajili ya Kanisa la Kisinodi: Umoja, Ushiriki na Utume.” Maadhimisho ya Awamu ya Pili ni kuanzia tarehe 4-27 Oktoba 2024. Lengo kuu la Maadhimisho haya ni kwa ajili ya Mama Kanisa kuendelea kujizatiti katika ujenzi wa utamaduni wa kuwasikiliza na kuwashirikisha waamini walei katika maisha na utume wake. Maadhimisho ya Sinodi za Maaskofu yanapania pia kujenga na kudumisha urika wa Maaskofu, tayari kumsikiliza Roho Mtakatifu, Mhimili mkuu wa mchakato wa uinjilishaji mpya unaosimikwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko. Huu ni utamaduni wa watu wa Mungu kusikilizana kwa makini! Ni kusikiliza Neno la Mungu, ili kulitafakari na hatimaye, kulimwilisha katika uhalisia na vipaumbele vya maisha ya waamini. Kusikiliza ni kujenga utamaduni wa kusali pamoja na Neno la Mungu, “Lectio Divina.” Ni wakati wa toba na wongofu wa ndani, kwa kuangalia matatizo, changamoto na fursa mbalimbali zinazojitokeza, ili hatimaye, kuhamasisha umoja na ushiriki wa watu wa Mungu kutoka katika ngazi mbalimbali za maisha, kama ilivyokuwa kwa Wafuasi wa Emau. Wafuasi hawa baada ya kukutana, kuzungumza na kutembea na Yesu Kristo Mfufuka, walirejea wakiwa wamesheheni furaha, imani na matumaini kedekede, tayari kutangaza na kushuhudia imani yao kwa Kristo Mfufuka aliyewafufua kutoka katika makaburi yao ya kutoamini na kujikatia tamaa.

Awamu ya Pili ya Sinodi 4-27 Oktoba 2024
Awamu ya Pili ya Sinodi 4-27 Oktoba 2024

Tarehe 9 Julai 2024, Sekretarieti kuu ya Sinodi za Maaskofu imechapisha “Hati ya Kutendea Kazi: Instrumentum laboris”, kama sehemu ya mwendelezo wa mchakato wa Maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu iliyozinduliwa kunako mwaka 2021, kama sehemu ya ujenzi wa Kanisa la Kisinodi linalowashirikisha waamini katika maisha na utume wake; Kanisa ambalo liko karibu zaidi na waamini wake; Kanisa linalowawezesha waamini wake kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wake; kwa kuthamini mchango wa wanawake katika maisha na utume wa Kanisa; daima likijielekeza katika ukweli na uwazi. Hati ya Kutendea Kazi, Instrumentum laboris imegawanyika katika sehemu kuu tano: Utangulizi; Dhamana na Utume wa Wanawake katika Kanisa: hapa kuna haja ya kujikita katika wongofu kwa kuwa na mwelekeo mpya utakaowawezesha waamini kukamilishana katika utekelezaji wa majukumu yao katika Kanisa; wote wakiishi na kutenda kama ndugu wamoja katika Kristo kama sehemu ya ushiriki wao wa utume wa pamoja! Hapa kuna haja ya kuondokana na mfumo dume, ambao umeathiri sana maisha na utume wa Kanisa, kwa kuhakikisha kwamba, wanawake wanapewa nafasi katika maisha na utume wa Kanisa; kwa kutambua na kuthamini maisha, karama na mapaji yao katika kuwajibika. Kuhusu Mashemasi wanawake ndani ya Kanisa Katoliki, bado upembuzi yakinifu kitaalimungu unaendelea na kwamba, Mashemasi wanawake, haitakuwa ni mada ya majadiliano wakati wa maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu mwezi Oktoba. Lakini, wanahitaji majiundo makini yatakayowawezesha hata kutangaza na kushuhudia Neno la Mungu hata wakati wa Maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu.

Wanawake washirikishwe zaidi katika vikao vya maamuzi
Wanawake washirikishwe zaidi katika vikao vya maamuzi

Sehemu ya Kwanza: Mahusiano na Mwenyezi Mungu, Kati ya Wakristo na Makanisa. Karam ana utume mbalimbali unaotekelezwa na Mama Kanisa unapaswa kujikita katika kutafuta na kuambata: haki, amani na matumaini. Vijana wa kizazi kipya wanataka kuona Kanisa linalosimikwa katika mahusiano yatakayosaidia kujenga na kudumisha utamaduni wa kusikiliza pamoja na kuwasindikiza vijana katika maisha yao; lakini waamini wanataka kuona Kanisa ambalo watajisikia wako huru, bila vitisho au maamuzi mbele. Sehemu ya Pili: Safari ya Majiundo na Mang’amuzi ya Kijumuiya yanayohitaji muda mrefu, kwa kuhakikisha kwamba, Kanisa linakita mizizi yake katika maisha ya watu. Kumbe, kuna haja ya Kanisa kujikita katika malezi na majiundo sanjari na kufanya mang’amuzi ya kijumuiya, ili kuliwezesha Kanisa kufanya maamuzi muafaka kwa kugawa nyajibu na kuhakikisha kwamba, kuna ushiriki wa waamini wote. Kumbe, kuna umuhimu wa kuendelea kujifunza katika shule ya Kisinodi inayowashirikisha waamini wote: wenye nguvu na dhaifu; vijana kwa wazee, kwani kila kundi linayo mambo ya kushirikisha; kwa kupokea na kutoa kwa wengine. Hati hii inakazia pamoja na mambo mengine, uwajibikaji; ukweli na uwazi kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya Kanisa zima. Hii ni sehemu muhimu sana inayopania kujenga uaminifu miongoni mwa watu wateule wa Mungu, ili kuwawezesha kutembea bega kwa bega, kwa kuwajibika kwa ajili ya utume wa pamoja. Hili ni Kanisa linalotafuta kujikita katika ukweli na uwazi pamoja na kutoa marejesho ya maisha na utume wake, hasa baada ya Kanisa kujikuta linatumbukia katika kashfa ya nyanyaso za kijinsia na kwamba, wakleri sasa wanawajibika kutoa marejesho ya maisha na utume wa Kanisa katika maeneo yao.

Kwa ajili ya Kanisa la Kisinodi: Umoja, Ushiriki na Utume
Kwa ajili ya Kanisa la Kisinodi: Umoja, Ushiriki na Utume

Hati ya Kutendea Kazi inasema, kuna haja ya kuwa na miundo mbinu itakatosaidia kufanya upembezi yakinifu katika ngazi zote za maisha na utume wa Kanisa si tu kwa kujikita katika kashfa za kijinsia ndani ya Kanisa, Matumizi ya fedha za Kanisa; lakini upembuzi utakaoliwezesha Kanisa kubaini changamoto za shughuli za kichungaji, mbinu za uinjilishaji mpya; jinsi ambavyo Kanisa linapaswa kusimama kidete kulinda na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu. Kumbe, kuna haja ya kuchapisha kila mwaka mapato na matumizi ya rasilimali za Kanisa; maisha na utume wa Kanisa mahalia; Ulinzi wa watoto wadogo; uhamasishaji wa ushiriki wa wanawake katika maisha na utume wa Kanisa katika masuala ya uongozi na kwenye vikao vyenye kufanya maamuzi. Sehemu ya Tatu: Hizi ni sehemu za Majadiliano ya Kiekumene na Kidini: Huu ni mwaliko kwa waamini kujenga na kudumisha mahusiano na mafungamano ya urafiki wa kijamii na waamini wa Makanisa na dini nyingine duniani, kwa kuvunjilia mbali maamuzi mbele na badala yake, kutambua na kuthamini tofauti msingi zinazoliwezesha Kanisa kuishi na watu wote katika msingi wa amani na maridhiano. Lengo ni kuendeleza mchakato wa majadiliano ya kiekumene, kidini na kitamaduni. Kwa Wakristo hii ni hija ya kutafuta umoja wa Wakristo. Hitimisho la Hati ya Kutendea Kazi: Instrumentum laboris: Hati hii inapaswa kuangaliwa kama chombo cha huduma kwa Kanisa, fursa ya pekee katika kuganga na kuponya madonda ya nyakati hizi. Hati hii inahitimishwa kwa mwaliko wa kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuendeleza hija ya matumaini mintarafu maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025 ya Ukristo!

Hati ya Sinodi

 

09 July 2024, 14:37