Mama Kanisa katika huruma yake kuu, ametenga rasmi mwezi Julai kwa ajili ya kukuza na kudumisha Ibada kwa Damu Azizi ya Kristo Yesu, Mto wa rehema. Mama Kanisa katika huruma yake kuu, ametenga rasmi mwezi Julai kwa ajili ya kukuza na kudumisha Ibada kwa Damu Azizi ya Kristo Yesu, Mto wa rehema. 

Jubilei ya Wamisionari, Watawa Na Walei wa Utume wa Damu Ni Julai Mosi 2025

Padre Emanuele Lupi, C.PP.S katika Waraka wake kwa Wamisionari wa Mashirika ya Damu Azizi ya Yesu pamoja na wanachama wa Utume wa waamini walei, Damu Azizi ya Yesu, anapenda kuchukua fursa hii kuwaalika Wamisionari, Watawa na Waamini walei kujiandaa katika Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo kwa kukutana mjini Roma, tarehe Mosi Julai 2025, tayari kutangaza na kushuhudia nguvu na upendo wa Damu Azizi ya Yesu, chemchemi ya neema na haki.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Tamko la Maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025 ya Ukristo linanogeshwa na kauli mbiu “Spes non confundit" yaani “Tumaini halitahayarishi.” Rum 5:5 na kwamba, kiini cha maadhimisho haya ni matumaini yatakayowawezesha watu waaminifu wa Mungu kutoka sehemu mbalimbali za dunia kufanya hija ya maisha ya kiroho mjini Roma sanjari na maadhimisho haya kufanyika kwenye Makanisa mahalia, ili kukutana na Kristo Yesu aliye hai na ambaye pia ni Mlango wa uzima. Rej, Yn 10:7.9. Mama Kanisa anaitwa na kutumwa kutangaza na kushuhudia Injili ya matumaini dhidi ya hofu na mashaka; ukosefu wa imani na furaha ya kweli. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025 itakuwa ni fursa ya kupyaisha tena matumaini kwa kuongozwa na Neno la Mungu. Katika Tamko hili, Baba Mtakatifu anakazia kuhusu Matumaini katika Neno la Mungu ili kuamini, kutumaini, kupenda na kuvumilia kwa kutambua kwamba, wao ni mahujaji wa matumaini.

Sherehe ya Jubilei ya Damu Azizi ya Yesu tarehe Mosi Julai 2025
Sherehe ya Jubilei ya Damu Azizi ya Yesu tarehe Mosi Julai 2025

Alama za matumaini zinazomwilishwa katika amani, kwa kujikita katika Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo, maboresho ya magereza; huduma kwa wagonjwa, vijana, wahamiaji na wakimbizi, wazee na maskini. Wito wa matumaini kwa kujikita katika matumizi bora ya rasilimali za dunia; msamaha wa madeni ya nje kwa nchi zinazoendelea duniani. Hii pia ni Jubilei ya Miaka 1, 700 tangu Mtaguso wa Nicea ulipoadhimishwa kunako mwaka 325. Nanga ya matumaini katika maisha ya uzima wa milele yanayopata chimbuko lake kutoka katika mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kwa wafu; Ushuhuda wa wafiadini na waungama imani; hukumu ya Mungu na mwaliko kwa waamini kujitakasa; Rehema na Sakramenti ya Upatanisho; Wamisionari wa huruma ya Mungu. Bikira Maria ni shuhuda wa hali ya juu kabisa wa matumaini, Nyota ya Bahari na kwamba, hija ya maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025 ya Ukristo iwasaidie waamini kujikita katika Maandiko Matakatifu.

Mwezi Julai ni kwa ajili ya Ibada ya Damu Azizi ya Yesu
Mwezi Julai ni kwa ajili ya Ibada ya Damu Azizi ya Yesu

Mama Kanisa katika huruma yake kuu, ametenga rasmi mwezi Julai kwa ajili ya kukuza na kudumisha Ibada kwa Damu Azizi ya Kristo Yesu, Mto wa rehema, shule ya utakatifu, haki, upendo, upatanisho na msamaha wa kweli. Damu Azizi ya Kristo ni chemchemi ya huruma ya Mungu kwa binadamu. Hii ni Ibada ambayo inaenezwa kwa namna ya pekee kabisa na Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu, C.PP.S., Shirika la Masista Waabuduo Damu Azizi ya Yesu, ASC, Mashirika ya Kitawa pamoja na waamini walei walioko kwenye utume wa Damu Azizi ya Yesu, sehemu mbalimbali za dunia. Fumbo la upendo wa Kristo Yesu limekuwa ni kivutio kikubwa cha waamini na waanzilishi wa Mashirika ya Kitawa kama vile Mtakatifu Gaspari del Bufalo na Mtakatifu Maria de Mathias, kiasi kwamba, fumbo hili la upendo na huruma ya Mungu limekuwa ni msingi wa maisha na utume wa Mashirika haya. Damu Azizi ya Kristo ni chemchemi ya wokovu wa ulimwengu na kwamba, ni alama ya juu kabisa inayoshuhudia upendo na sadaka ya maisha kwa ajili ya wengine. Sadaka hii inajirudia tena na tena katika maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa, kiasi cha Kristo Yesu kuwakirimia waamini Mwili na Damu yake Azizi; Damu ya Agano Jipya na la milele, iliyomwagika kwa ajili ya maondoleo ya dhambi, maisha na uzima wa milele. Baba Mtakatifu Francisko anawataka waamini kujitambua kama watu waliotiwa muhuri ili kushiriki katika utume wa Kristo Yesu, ili waweze kuwa ni mwanga na baraka inayofufua na kupyaisha; mwanga unaoponya na kumweka mtu huru; tayari kujisadaka kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu.

Padre Emanuele Lupi, Mkuu wa Shirika la C.PP.S na Wanashirika wake
Padre Emanuele Lupi, Mkuu wa Shirika la C.PP.S na Wanashirika wake

Ni katika muktadha huu, Mheshimiwa Padre Emanuele Lupi, Mkuu wa Shirika la Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu Ulimwenguni, katika waraka wake kwa Wamisionari wa Mashirika ya Damu Azizi ya Yesu pamoja na wanachama wa Utume wa waamini walei, Damu Azizi ya Yesu, anapenda kuchukua fursa hii kuwaalika Wamisionari, Watawa na Waamini walei kujiandaa kikamilifu katika Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo kwa kukutana mjini Roma, tarehe Mosi Julai 2025, tayari kutangaza na kushuhudia nguvu na upendo wa Damu Azizi ya Kristo, chemchemi ya neema na Muumba wa mema yote. Maadhimisho haya yananogeshwa na kauli mbiu: “Jubilei ya Damu Azizi ya Kristo, maisha na matumaini ya ulimwengu.” Huu ni mwaliko kwa waamini kujikita katika uchaji na tafakari ya kina juu ya Damu Azizi ya Kristo Yesu “bei ya fidia yetu, dhamana ya wokovu na uzima wa milele” kama alivyosema Mtakatifu Yohane XXIII, katika Waraka wake wa “Inde a primis ya Mwaka 1960. Damu iliyomwagika ni ishara na onesho la maisha yanayoyotolewa kwa njia ya umwagaji damu kama ushuhuda wa upendo mkuu, tendo la unyenyekevu wa Kimungu kuelekea hali yetu ya kibinadamu. Mwenyezi Mungu alichagua ishara ya damu, kwa sababu hakuna ishara nyingine iliyo fasaha sana kuonesha uhusika kamili watu. Rej. Mtakatifu Yohane Paulo II, 1 Julia 2000.

Ibada kwa Damu Azizi ya Yesu ni chemchemi ya huruma ya Mungu
Ibada kwa Damu Azizi ya Yesu ni chemchemi ya huruma ya Mungu

Tukio hili litatanguliwa na Mkesha wa Sherehe ya Jubilei utakaoadhimishwa tarehe 30 Juni 2025 kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Paulo, Nje ya Kuta za Roma, kuanzia saa 10: 00 hadi 11:30 kwa Saa za Ulaya. Tarehe Mosi Julai, 2025 Baba Mtakatifu Francisko ataongoza Ibada ya Misa Takatifu na waamini watapitia Lango kuu la Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican kuanzia saa 3:30 na Ibada ya Misa Takatifu itaanza rasmi Saa 4: 00. Kwa saa za Ulaya. Tarehe 2 Julai 2025 itakuwa ni siku maalum kwa Wamisionari, watawa na waamini walei wa Utume wa Damu Azizi ya Yesu kufahamiana pamoja na kutembelea maeneo ya kihistoria mjini Roma. Gharama ya ushiriki kwa kila hujaji inatarajiwa kuwa ni Euro 1,600. Baba Mtakatifu Francisko ametangaza kwamba, Mwaka 2024 uwe ni mwaka wa Sala kama sehemu ya maandalizi ya Jubilei ya Mwaka 2025 ya Ukristo. Mwaka huu unapania pamoja na mambo mengine: Kugundua na kupyaisha umuhimu wa maisha ya sala katika maisha ya mtu binafsi, ndani ya Kanisa na katika Ulimwengu katika ujumla wake. Maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025 ya Ukristo, yatazinduliwa rasmi kwa kufungua Lango kuu la Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican tarehe 24 Desemba 2024.

Damu Azizi ya Yesu ni chemchemi ya wokovu wa walimwengu
Damu Azizi ya Yesu ni chemchemi ya wokovu wa walimwengu

Mwaka wa Sala Kuelelea Maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025 unapania pamoja na mambo mengine anasema Baba Mtakatifu Francisko: Kupyaisha matumaini baada ya watu wengi kukata na kujikatia tamaa ya maisha kutokana na hali ngumu ya maisha, vita na mipasuko ya kijamii bila kusahau athari za mabadiliko ya tabianchi. Huu ni mkakati wa shughuli za kichungaji unaopania kuwarejeshea tena watu wa Mungu matumaini. Huu ni mwaliko kwa kila jimbo, baada ya kusoma alama za nyakati kwa watu wake, liandae katekesi kuanzia wakati huu, hadi wakati wa ufunguzi wa Maadhimisho ya Jubilei ya mwaka 2025 hapo tarehe 24 Desemba 2024. Katekesi hii ilenge kuwasaidia waamini kujiandaa kikamilifu kuingia katika lango la Jubilei, ambalo ni Kristo Yesu, Mwanakondoo Mungu. Padre Emanuele Lupi, Mkuu wa Shirika la Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu Ulimwenguni anasema kama sehemu ya maandalizi ya Maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025 ya Ukristo, kuanzia tarehe Mosi Desemba 2024 hadi tarehe Mosi, Julai 2025, yatakuwa ni maandalizi ya maisha ya kiroho, miezi saba kama ishara ya Matoleo Saba ya Umwagaji Damu Azizi ya Kristo Yesu, mwaliko wa kutafakari juu ya Fumbo la Damu Azizi ya Kristo Yesu. Kwa mawasiliano zaidi unaweza kuwasiliana kwa njia ya barua pepe kwa Katibu wa Jubilei ya Damu Azizi ya Yesu kwa anuani ifuatayo: prezgiub25@gmail.com.

Ifuatayo ni orodha ya wajumbe wa Tume ya Maandalizi ya Jubilei:

Padre Giovani Francilia, Mmisionari wa Damu Azizi, gfrancilia@yahoo.itMratibu

Sr Ana Marija Antolović, Masista Waabuduo Damu ya Kristo, sljeme2005@gmail.comMratibu

Sr Ljubica Radovac, Masista Waabuduo Damu ya Kristo, ASC, prezgiub25@gmail.comKatibu

Padre Federico Maria Rossi, Mmisionari wa Damu Azizi, C.PP.S., federicomaria.rossi@gmail.com

Sr M. Gaspara Sannikova, Watumishi wa Damu Takatifu (SAS), sr.kaspra@gmail.com

Sr Rita Farioli, Shirika la Masista wa Damu Azizi, ASC., 11due57@gmail.com

Sr Terry Walter, Masista wa Damu Azizi, Dayton-Ohio, ASC., twalter@cppsadmin.org

Vicky Otto, Shirika la Roho ya Damu Azizi, votto@pbspiritualityinstitute.org

Sr Maksymiliana Nowakowska, Mmisionari wa Damu ya Kristo,  msc.sekretariat@gmail.com

Jubilei ya Damu Azizi ya Yesu
01 July 2024, 15:33