Kard.Rugambwa,Tabora:waamini waepuke udanganyifu wa kupotosha imani yao
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Mama Kanisa anaadhimisha kila ifikapo tarehe 3 Julai ya kila mwaka siku kuu ya Mtume Thomas aliyeitwa pia Pacha na alikuwa Myahudi wa karne ya 1, mmojawapo kati ya Mitume wa Yesu anayeheshimiwa kama mtakatifu, kwa namna ya pekee na Wakristo wa maeneo yaliyokuwa mashariki kwa Dola la Roma, kuanzia Iraq hadi India. Inawezekana kwamba sababu yake ni kazi za utume alizozifanya huko hadi kifodini huko Chennai mnamo mwaka 72 na kaburi lake huoneshwa katika mji huo wa Tamil Nadu.
Kwa njia hiyo katika fursa ya siku kuu hiyo, Jimbo Kuu Katoliki la Tabora nchini Tanzania, limefanya maadhimisho ya Misa Takatifu ya kupewa Pallium Takatifu kwa Askofu Mkuu, Kardinali Protase Rugambwa, mikononi mwa Balozi wa Vatican nchini Tanzania, Askofu Mkuu Angelo Accattino. Misa hiyo iliudhuriwa na Waamini kutoka Kanda ya Tabora, viongozi wa kidini na serikali. Kuhusiana na tendo la Pallium, ni mojawapo ya zile zilotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, tarehe 29 Juni 2024, katika Siku Kuu ya Watakatifu Petro na Paulo, wakati wa Maadhimisho ya Misa Takatifu yaliyofanyika katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Sherehe hizo ziliwaona maelfu ya waamini kuanzia: Makardinali, Maaskofu wakuu, maaskofu, mapadre, mashemasi, watawa kike na kiume na waamini watu wa Mungu. Na zaidi, pia Maaskofu wakuu 33 kati ya 42 waliokuwapokukabidhiwa Pallium hizo hizo na Papa.
Katika maadhimisho hayo Jimbo Kuu Tabora, katika, mahubiri yaloingozwa Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu katoliki la Tabora, Kardinali Rugambwa, ambaye kwa kujikita na masomo ya Liturujia, awali ya yote alimshukuru Askofu Eusebius Nzigilwa, wa Jimbo Katoliki la Mpanda, Tanzania kwa Tafakari ya Masifu ya jioni, siku iliyotangulia, huku akifafanua zaidi “kueleza nini maana ya Pallium na juu ya tendo hilo kwa ujumla ambalo lilifanyika katika jimbo Kuu la Tabora la kumvika Askofu Mkuu wa Jimbo kuu hilo. Kwa njia hiyo akijikita kutazama Injili kuhusu Mtume Thomas, Kardinali Rugambwa alisisitiza juu ya umuhimu wa “kuwa na imani thabiti. Kukosekana kwa imani iliyo thabiti na isiyo yumba, inatufanya tukose umoja na ushirika na hata kukosa upendo na ari ya kutumikia kama atakavyo Mungu mwenyewe. Tunadanganywa na Ulimwengu, watu na vitu vinavyotupendezea, vinavyotuleta tusifuate imani ya kweli, kadiri ya mapokea na mafundisho yetu.” Alisisitiza Kardinali.
Kwa njia hiyo Kardinali Rugambwa alitoa onyo kwa waamini wote kuepuka pepo za udanganyifu, kama vile: “wanaojiita maaskofu, maaskofu wakuu, wengine hata kujiita mapapa, na mifano mingi zaidi ya kudanyanywa na makundi yanayowafuata ni mengi sana na mengine kutafuta kuyaingiza katika imani yetu tofauti na mapokeo tuliyopata kutoka katika mitume na mafundisho ya Kanisa.” Alithibitisha. Kwa kuendelea aidha Kardinali Protase alisema: “Imani Imara ndiyo itakayotusukuma tumtaje Bwana na Mungu wetu. Kwa nini tusiwe kama Mtume Thoma, kutafuta Yesu na kutaka kuweka vidole vyetu katika madonda yake?” Ni swali la Kardinali Rugambwa.
Yafuatayo ni Mahubiri kamili ya Kardinali Rugambwa 3 Julai
Ndugu zangu wapendwa katika Kristu, Nianze tafakuri yangu hii nikimshukuru Askofu Nzigilwa ambaye kwenye masifu ya Jana Jioni alituingiza katika kuyaelewa maadhimisho haya akitueleza ni kitu gani tulichokuja kufanya hapa na kwa namna ya pekee akitoa maelezo ya kutufanya tuelewe hii Pallium niliyovishwa leo ni nini na ina maana gani ! Baba Nzigilwa asante sana. Yale mafundisho tuliyosikia jana yamewekwa kwa namna yake katika maneno ya sala tuliyosikia kutoka kwa Mwakilishi wa Baba Mtakatifu, Askofu Mkuu Angelo Accattino, aliyesali akisema kuwa, nanukuu: “Pallium hii iwe kwako ishara ya umoja na alama ya ushirika na kiti cha Kitume; iwe kifungo cha upendo na msukumo wa ujasiri, ili siku ya kuja na kufunuliwa kwake Mungu Mkuu na Mkuu wa wachungaji Yesu Kristo, uweze kupata, Pamoja na kundi ulilokabidhiwa vazi la kutokufa na la utukufu”.
Ndugu zangu tunayasikia maneno yote haya tukiwa leo tunaadhimisha Sikukuu ya Mtakatifu Toma Mtume, ambaye mimi binafsi napenda awe mfano kwangu wa mtu anayetafuta daima kuwa na imani iliyo imara, kama kweli nataka kuwa na mamlaka niliyopewa na Baba Mtakatifu ambayo yatazaa matunda ya kutufanya sote tupate vazi la kutokufa na la utukufu atakapokuja Mungu Mkuu na Mkuu wa wachungaji Yesu Kristo. Ninapojiombea mimi na kuwaomba ninyi mniombee niwe na Imani imara napenda pia kuwaombea ninyi muwe na Imani imara ambayo itatusukuma sote kwa Pamoja tumkiri kwa kutosita huyo Mungu tunayemuamini kuwa ni Bwana na Mungu wetu kwa mfano wa Mtume Toma aliyekuwa wa kwanza kuyatamka hayo. Nayasema hayo ya kuomba Imani iliyoimara nikimuomba Mtume Toma atuombee, kwani leo hii, ukosefu wa Imani iliyo imara unasababisha mpasuko mkubwa katika Kanisa letu, kuanzia kwenye Familia zetu, kwenye Jumuiya ndogondogo ambazo leo tunajivunia kuona zimetimiza miaka 50 tangu zilipoanzishwa kwenye nchi zetu za AMECEA, kwenye Kanisa letu la kitaifa na hata kwenye Kanisa la kiulimwengu.
Kukosekana kwa Imani iliyothabiti na isiyoyumba kunatufanya tulikose hilo la umoja, na ushirika ninaloombwa mimi kuwa nalo kwa ishara hiyo na alama ya Pallium na hata kukosa upendo na ari ya kutumikia kama atakavyo Mungu Mwenyewe. (Tunadanganywa na malimwengu, watu na vitu vinavyotupendekezea Imani zisizo za kweli kadili ya mapokea na mafundisho yetu !!!!!!!) Kwa nini tusiwe kama Mtume Toma tukatafuta kuziona mikononi mwake kovu za misumari, na kutia vidole vyetu katika ubavu wake ili tuweze kusadiki, katika maana kwamba tusidanganywe bure na hayo tunayokutana nayo kila siku yakituletea mafundisho ya Imani isiyo ya kweli naya kutuacha katika mashaka !!!!
Ni kweli kabisa kuwa sisi tulio viongozi lazima tuwe mstari wa mbele katika kuyaishi na kuyaonesha hayo lakini, ukweli unabaki kwamba sote kama waamini wabatizwa yatubidi tutembee Pamoja katika kuyaishi Maisha hayo yanayoongozwa na Imani na mafundisho ya kweli yaliyofunuliwa na Kristu aliye jiwe kuu la pembeni na hata Kanisa, yanayolenga kutufikisha kwenye Utukufu na uzima wa Milele, kama alivyotukumbusha leo Mtume Paulo katika Waraka wake kwa Waefeso. Napenda niseme wazi kuwa moja ya kazi anayopaswa kuifanya huyo anayevishwa Pallium kama hiyo niliyovishwa leo ni kuhakikisha kuwa katika eneo lake Imani inalindwa na nidhamu ya Kanisa vinafuatwa na kuheshimiwa.
Sisi leo katika Kanda yetu, tunaohitimisha Miaka 50 ya maadhimisho ya Jumuiya Ndogondogo ikiwa ni Pamoja na kufunga maadhimisho ya kumbukumbu tuliyokuwa nayo ya miaka 60 tangu ilipotolewa hati ya ki-liturgia, ya “Sacrosanctum Concilium” ya Mtaguso wa pili wa Vatikano, naamini kuwa tutakuwa tumeyatafakari mengi na kupendekeza pia baadhi ya vitu ambavyo inabidi tuvifanyie kazi ili vitusaidie katika kukua kwenye Imani ya kweli na hivyo kupata msukumo wa kutenda na kuishi Maisha ya kitakatifu kama atakavyo Mungu na Kanisa. Basi tualikane leo kuwa tayari kutembea Pamoja tena katika Jumuiya zetu zilizo nguzo na uwanja wa kutujenga na kutuimarisha katika Imani tunapolitafakari na kushirikishana neno la Mungu litakaloyafunua mapenzi yake kwetu, tukiyaadhimisha pia mafumbo matakatifu katika liturgia zenye kutuunganisha wote kama Kanisa mahalia tukijifunza na kusaidiana katika ngazi mbali mbali, tukimtukuza Mungu na kuutafuta utakatifu wa kutustahilisha Utukufu wake.
Nawaalika tena mniombee mimi binafsi nikue katika Imani imara ili niweze, kama ni kuwa mchungaji mwema katika kanda hii, kuyafanya yote nikiongozwa na nguvu hiyo ya ki-Mungu, ninayetaka awe ndiye yeye pekee wa kunifungulia mlango kama alivyofanya kwa Manabii na mitume na hata kwa wengine wote waliomsadiki na akawanao daima katika yote waliyofanya. Nanyi nawaombea hilo na kwa Pamoja tuyafanye Mapenzi yake daima na hivyo kuujenga Ufalme wake kokote tulipo, Amina.
Baada ya kuhitimisha Misa, Kardinali Rugambwa aidha aliwashukuru wote kuudhuria pamoja na kuwa ilikuwa siku ya kazi na hsa kuwatia moyo kuendeleza shughuli walizoanzisha katika maadhimishao ya miaka 50 ya Jumuiya ndogo ndogo, na katika kuhitimisha mwaka mzima wa Kumbukizi ya Miaka 60 ya Hati ya Sacrosantum Concilium ya Mtaguso wa Pili wa Vatican. Kwa njia hiyo kuwakumbusha zaidi ilikuwa ni mnamo tarehe 12 Januari 2015 ambapo Baba Mtakatifu Francisko alitamka kwamba, tangu wakati huo, Maaskofu wakuu watakuwa wanashiriki katika Ibada ya Misa takatifu kwa ajili ya kubariki Pallia takatifu kila mwaka ifikapo tarehe 29 Juni, Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo Mtume wa Watu lakini Pallia takatifu watavikwa na Mabalozi wa Vatican katika chi husika kadiri ya nafasi zao. Lengo kuu la mabadiliko haya ni kuwawezesha watu wa Mungu kutoka katika Makanisa mahalia kushiriki kikamilifu katika maadhimisho haya adhimu katika maisha, historia na utume wa Kanisa mahalia. Pili, ni kuendelea kuimarisha mchakato wa unafsishaji wa “dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa.” Kwa njia hiyo msikose kufuatilia tukio hilo la kupewa Palia kwa Kardinali Rugambwa katika Jimbo Kuu lake. Na ndivyo ilikuwa huko Tabora ambapo waamini waliweza kuona tukio hilo adhimu sana.