Kumbukizi ya Miaka 55 ya SECAM: Ari na Moyo wa Kimisionari & Utume wa Walei
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Mtakatifu Paulo VI alipotembelea kwa mara ya kwanza Bara la Afrika kwa kufanya hija ya kitume nchini Uganda kuanzia tarehe 31 Julai hadi tarehe 2 Agosti 1969 kwanza kabisa: aliitaka familia ya Mungu Barani Afrika kuwa mashuhuda wa imani, matumaini na mapendo kwa Kristo na Kanisa lake; kujenga na kudumisha ari na mwamko wa kimisionari, tayari kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu Barani Afrika. Alisema, viongozi wa kisiasa Barani Afrika wanapaswa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa misingi ya haki, amani na maridhiano. Kanisa kwa kushirikiana na Serikali mbalimbali Barani Afrika zisaidie kukoleza mchakato wa maendeleo fungamani ya binadamu kwa: kusimama kidete kulinda na kutetea utu, heshima na haki msingi za binadamu, wanawake Barani Afrika wakipewa kipaumbele cha kwanza! Alilitaka Kanisa kuwekeza zaidi katika sekta ya elimu, afya, kilimo na huduma bora za maji safi na salama. Katika muktadha huu, Mtakatifu Paulo VI alikazia umuhimu wa majadiliano ya kidini na kiekumene Barani Afrika kama njia ya kukuza na kudumisha umoja, upendo na mshikamano wa kidugu. Alikazia pia umuhimu wa kukuza na kuendeleza mashirika na vyama vya kitume ili kusaidia majiundo, malezi na makuzi ya imani, tayari kuchangia katika mchakato wa kuyatakatifuza malimwengu! Mtakatifu Paulo VI, katika hija yake ya kitume, aliwataka waamini kuiga mfano bora wa Mashahidi wa Uganda walioyamimina maisha yao kama kielelezo cha ushuhuda wa imani kwa Kristo na Kanisa lake. Akawataka wawe jasiri na thabiti katika imani, matumaini na mapendo kwa Mungu na jirani. Ujasiri wa imani unawawezesha waamini kumwilisha Neno la Mungu katika maisha na vipaumbele vyao.
Waamini waendelee kuboresha imani yao kwa njia ya Sakramenti za Kanisa na Ibada mbalimbali, ambazo zitawasaidia kuwa kweli ni wafuasi wamisionari wa Kristo Yesu, kwa kuhakikisha kwamba, imani inamwilishwa katika matendo adili na matakatifu. Imani iwasaidie kuonesha upendo kwa Mungu na jirani. Mtakatifu Paulo VI, wakati alipokuwa anazungumza na Maaskofu Katoliki kutoka sehemu mbalimbali za Bara la Afrika, alikazia umoja na mshikamano katika urika wa Maaskofu katika kutekeleza dhamana na wajibu wao wa kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu. Ili kukuza na kudumisha maisha ya Kikristo Barani Afrika kwa kutambua kwamba, tangu wakati huu, waafrika wenyewe wanapaswa kuwa ni wamisionari Barani Afrika tayari kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa Mungu Barani Afrika. Dhamana hii inajikita katika ujenzi wa miundo mbinu ya Kanisa, itakayoliwezesha Kanisa kuonenana, chini ya uongozi wa Roho Mtakatifu. Kanisa kwa asili ni la kimisionari, dhamana inayopaswa kuendelezwa na kudumishwa Barani Afrika. Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katokiki Afrika na Madagascar, SECAM ni matunda ya maadhimisho ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, uliowahamasisha Maaskofu kutoka Barani Afrika kushikamana kwa hali na mali, ili kuweza kukoleza ari na moyo wa kimisionari, tayari kujikita katika mchakato wa uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. SECAM ikazinduliwa rasmi tarehe 31 Julai 1969 huko Uganda. Katika kipindi cha miaka 55 iliyopita, kumekuwepo na mafanikio makubwa na changamoto katika maisha na utume wa Kanisa Barani Afrika. SECAM inasema, mchakato wa uinjilishaji Barani Afrika unakwenda sanjari na maendeleo fungamani ya binadamu yanayogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Mababa wa SECAM wanakazia kwa namna ya pekee kabisa, umuhimu wa kumwilisha dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa, mwelekeo mpya wa utendaji wa Kanisa kama anavyokazia Baba Mtakatifu Francisko.
Kardinali Fridolin Ambongo Besungu, O.F.M. Cap. Rais wa SECAM katika maadhimisho ya Miaka 55 ya SECAM anasema, takwimu zinazonesha kwamba, Waamini wa Kanisa Katoliki wanaunda walau asilimia 18% ya Wakristo wote Barani Afrika. Kanisa Barani Afrika halina budi kujikita katika mchakato wa Uinjilishaji ndani na nje ya Bara la Afrika; sanjari na kuendelea kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Umefika wakati kwa Kanisa Barani Afrika kuwatuma wamisionari wake kwenda kuinjilisha Ulaya na Marekani, kama kielelezo cha moyo wa shukrani kwa kuwatangazia watu wa Mungu Habari Njema ya Wokovu. Ongezeko la idadi ya Mapadre wa Majimbo na Mashirika ya Kimisionari na Kitume Barani Afrika ni ishara tosha kwamba, Mapadre hawa wanaweza kutumwa kuinjilisha nje ya Bara la Afrika. Kwa hakika Kanisa Barani Afrika linazidi kukua na kukomaa na kwamba, limekuwa mstari wa mbele katika kukuza na kudumisha utu, heshima, haki msingi za binadamu; ustawi na maendeleo ya wengi. Kanisa Barani Afrika limewekeza sana kwenye sekta ya elimu, afya, ustawi na maendeleo ya watu. Ni sauti ya watu wasiokuwa na sauti, changamoto kubwa kwa Bara la Afrika ni deni kubwa la nje linalokwamisha maendeleo. Kanisa Barani Afrika kama Kanisa la Mungu linalowajibika linaendelea kujikita katika mchakato wa ujenzi wa Jumuiya Ndogondogo za Kikristo.
Jumuiya Ndogo ndogo za Kikristo zinapaswa kuimarishwa na kuendelezwa ili kujenga misingi ya umoja, udugu, upendo na mshikamano kati ya waamini kwani huu ndio mfumo na utambulisho wa Kanisa Barani Afrika, bila kusahau utume wa vijana na familia! Ushiriki mkamilifu wa waamini katika maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa, ili kuendelea kujenga na kuimarisha Fumbo la Mwili wa Kristo yaani Kanisa, umesisitizwa sana. Hii iwe ni fursa ya waamini kusikiliza na kutafakari Neno la Mungu linalopaswa kumwilishwa katika uhalisia wa maisha, kielelezo cha imani tendaji. Katekesi ya awali na endelevu ni muhimu sana katika kupyaisha uelewa wa Mafundisho tanzu ya Kanisa, ili waamini waweze kuwa tayari kuyashuhudia, kuyalinda na kuyatetea pale yanaposhambuliwa. Wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji kutoka Barani Afrika ni changamoto changamani inayohitaji kuvaliwa njuga na Kanisa Barani Afrika. Familia ya Mungu Barani Afrika imetakiwa kuwa macho dhidi ya utamaduni wa kifo unafumbatwa katika sera na mikakati ya utoaji mimba, kifo laini pamoja na shinikizo la ndoa za watu wa jinsia moja; mambo ambayo kimsingi yanasigana na kanuni maadili, utu wema na mpango wa Mungu katika maisha ya mwanadamu! Sanjari na hili, Mababa wa SECAM wanasema, haki msingi na ulinzi wa watoto wadogo ni kati ya changamoto na vipaumbele vya Kanisa Barani Afrika, kwa sasa na kwa siku za usoni. Mababa wa SECAM wanasema, Familia inakabiliwa na changamoto nyingi katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia sanjari na mabadiliko msingi katika maisha ya kijamii, kitamaduni na kiuchumi; mambo yanayochangia kushamiri kwa: Uchoyo na ubinafsi, ubabe unaofanywa na baadhi ya watu kwa kutaka kujimwambafai sanjari na anasa.
Maaskofu wanabainisha kwamba, hivi ni vishawishi ambavyo kimsingi vinasigana sana na tunu msingi za maisha ya kifamilia kadiri ya mapokeo na tamaduni njema za Kiafrika; yaani ile hali ya mtu kujitosa kisawasawa katika upendo! Maaskofu wanakazia umuhimu wa kufanya maandalizi ya kina kwa wanandoa watarajiwa, ili kuweza kukabiliana na changamoto za maisha ya ndoa na familia, jambo ambalo linahitaji mikakati makini ya kichungaji kuhusu utume wa familia. Maaskofu wanawataka waamini waliopewa dhamana katika tume ya shughuli za kichungaji kwa ajili ya familia kuhakikisha kwamba, zinatekeleza dhamana na wajibu wake bila ya kujibakiza kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Familia Barani Afrika. Barua binafsi ya Baba Mtakatifu Francisko “Motu proprio” ijulikanayo kama “Vos estis lux mundi” yaani “Ninyi ni nuru ya ulimwengu”: Sheria mpya kwa ajili ya Kanisa Katoliki dhidi ya nyanyaso za kijinsia inahusu nyanyaso za kijinsia ndani ya Kanisa. Katika barua hii, Baba Mtakatifu anabainisha sheria, kanuni na taratibu mpya zinazopaswa kutekelezwa pale kunapojitokeza shutuma za nyanyaso za kijinsia ndani ya Kanisa. Nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo ndani ya Kanisa ni kashfa ambayo imechafua maisha na utume wa Kanisa kiasi kwamba, haiwezi kamwe kufichwa, kuikataa wala kuibeza kwani ni ukweli usioweza kufumbiwa macho anasema Papa Francisko. Ukweli huu unapaswa kupokelewa na hatimaye, kumwilishwa katika mchakato wa toba na wongofu wa ndani, wema na utakatifu wa maisha; kwa kuganga na kutibu madonda ya kashfa ya nyanyaso za kijinsia, tayari kuambata upendo na huruma ya Mungu, ili kuanza upya kwa kuchuchumilia: kanuni maadili, utu wema na utakatifu wa maisha. Lengo kuu ni kuzuia kashfa ya nyanyaso za kijinsia isijitokeze tena ndani ya Kanisa.
Mababa wa SECAM wanaitaka familia ya Mungu Barani Afrika kuwa macho na biashara haramu ya binadamu na viungo vyake; kazi za suluba kwa watoto wadogo pamoja na kukazia haki msingi za watoto wadogo. Kanisa Barani Afrika halina budi kujiwekea Mwongozo wa utekelezaji wa sera na mikakati ya kuzuia nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo ndani ya Kanisa. Kardinali Berhaneyesus Demerew Souraphiel, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Ethiopia amekazia umuhimu wa familia ya Mungu Barani Afrika kusimama kidete kulinda, kutunza, kuendeleza pamoja na kushuhudia Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. Kanisa Barani Afrika liwe ni shuhuda na chombo cha haki, amani na upatanisho hasa katika nchi zile ambamo bado kuna vita, kinzani na mipasuko ya kijamii na kisiasa kama inavyojionesha nchini Sudan ya Kusini. Umoja wa Afrika uwe ni chachu ya haki, amani na upatanisho wa kweli. Viongozi waliopewa dhamana ya kuongoza, watekeleze wito huu kwa ari na moyo mkuu! Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika Magharibi, CERAO limekazia umuhimu wa kukuza na kudumisha demokrasia na utawala bora Barani Afrika kwa kuzingatia: demokrasia shirikishi, uhuru wa watu kutoa maoni yao; utawala wa Sheria sanjari na kuzingatia: utu, heshima na haki msingi za binadamu! Rushwa na ufisadi wa mali ya umma; uharibifu wa mazingira nyumba ya wote; vita, kinzani na vitendo vya kigaidi pamoja na misimamo mikali ya kidini na kiimani ni mambo yanayohitaji kupewa kipaumbele cha pekee katika maisha na utume wa Kanisa Barani Afrika. Toba na wongofu wa ndani; majadiliano ya kidini na kiekumene; ujenzi wa dhamiri nyofu pamoja na ushiriki mkamilifu wa waamini walei ni mambo muhimu katika maisha na utume wa Kanisa. Wimbi kubwa na wakimbizi na wahamiaji kutoka Barani Afrika; kuteteleka kwa tunu msingi za maisha ya ndoa na familia; maendeleo ya sayansi, teknolojia na utandawazi yanapaswa kuangaliwa kwa kina na mapana katika vipaumbele vya Kanisa Barani Afrika, katika sera na mikakati yake! Dhamana na utume wa Makatekista katika mchakato wa: kufundisha na kulea imani.
Makatekista wanapaswa kuwezeshwa kikamilifu ili waweze kufundisha kwa umakini mkubwa kuhusu: Imani, Sakramenti za Kanisa, Maisha adili pamoja na maisha ya sala, ili waamini waweze kupata neema zinazotolewa na Mama Kanisa katika maadhimisho haya. Makatekista wanao wajibu wa kuwasaidia waamini kumwilisha imani yao katika uhalisia wa maisha kwa njia ya ushuhuda unaoleta mvuto na mguso. Ni watu wanaopaswa kuwasaidia waamini kujenga na kuimarisha moyo wa sala kama njia ya kuzungumza na Mwenyezi Mungu kutoka katika undani wa maisha yao. Katika sera na vipaumbele vya Kanisa Barani Afrika, waamini walei wanapaswa kupewa kipaumbele cha pekee ili waweze kuwa ni nyenzo msingi za kuyatakatifuza malimwengu kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko! Waamini walei kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo wanashiriki katika: Ukuhani, Unabii na Ufalme wa Kristo, kumbe, ni vyombo na mashuhuda wa furaha ya Injili kwa watu wa nyakati hizi. Waamini wa Kanisa Katoliki Barani Afrika waendeleze majadiliano ya kidini na kiekumene, ili kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu. Mababa wa SECAM wanawashukuru na kuwapongeza waamini wote ambao wameendelea kusimama imara na thabiti katika imani, matumaini na mapendo, licha ya changamoto kubwa wanazokabiliana nazo katika maisha na utume wao! Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kumwilisha matunda ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican katika maisha na utume wa Kanisa, kwa kukazia umuhimu wa watu wa Mungu, kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa.
Ikumbukwe kwamba, Kanisa ni Jumuiya ya waamini wanaotembea pamoja katika: Imani, Sakramenti za Kanisa, Maisha adili na Sala. Hii ni Jumuiya inayofumbatwa katika misingi ya: imani, matumaini na mapendo kwa kuambata mshikamano na maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Hawa ndiyo wakimbizi na wahamiaji; maskini, wazee na wagonjwa ambao wanaonekana kana kwamba si mali kitu katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia! Itakumbukwa kwamba, Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katokiki Afrika na Madagascar, SECAM linaundwa na: AMECEA, yaani Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika Mashariki na Kati. IMBISA yaani Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Kusini mwa Afrika. CERAO/RECOA: yaani Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika Magharibi pamoja na CEDOI, Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Bahari ya Hindi.