Tafuta

Mashindano ya Olympiki iwe ni fursa ya kusitisha vita, mapigano na kinzani hizi na muda huu uwe ni kwa ajili ya ujenzi wa umoja na mshikamano wa udugu wa kibinadamu Mashindano ya Olympiki iwe ni fursa ya kusitisha vita, mapigano na kinzani hizi na muda huu uwe ni kwa ajili ya ujenzi wa umoja na mshikamano wa udugu wa kibinadamu 

Michezo ya Olimpiki ya Paris 2024: Dumisheni Tunu Msingi za Michezo

Hiki ni kipindi ambacho vita sehemu mbalimbali za dunia bado inaendelea kurindima, kuna misigano na mipasuko ya kijamii katika ngazi ya Kimataifa inayoendelea, kumbe, kipindi cha Mashindano ya Olympiki iwe ni fursa ya kusitisha vita, mapigano na kinzani hizi na muda huu uwe ni kwa ajili ya ujenzi wa umoja na mshikamano wa udugu wa kibinadamu, kwa kutumia lugha ya michezo inayoeleweka na wote. Ni wakati wa kumwilisha tunu msingi za michezo katika uhalisia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Michezo ya Olimpiki ya Paris kwa Mwaka 2024 inaanza kutimua vumbi Ijumaa tarehe 26 Julai hadi Jumapili tarehe 11 Agosti 2024 na Michezo ya Olimpiki Kwa Ajili ya Walemavu itaanza rasmi tarehe 28 Agosti hadi tarehe 8 Septemba 2024. Jiji la Paris, Ufaransa ndiye mwenyeji wa Michezo ya 33 ya Olimpiki, moja ya matukio makubwa ya michezo ulimwenguni yanayowashirikisha wanamichezo bora kutoka sehemu mbalimbali za dunia. Kipindi chote cha mashindano ya Olimpiki, kadiri ya historia vita na misigano yote ya kisiasa na kijamii ilisitishwa ili kutoa fursa kwa wananchi kufurahia michezo nchini Ugiriki. Kumbe tangu mwanzo, tunu ya amani na maridhiano kati ya watu imekuwa ni kati ya mambo yanayotiliwa mkazo wakati wa michezo ya Olimpiki. Ni katika muktadha wa umuhimu wa kujenga na kudumisha amani na utulivu, Baba Mtakatifu Francisko, Dominika tarehe 21 Julai 2024 ameitaka Jumuiya ya Kimataifa kusitisha vita na kuonesha utashi wa kutaka kujikita katika ujenzi wa amani. Michezo ya Olimpiki iwe ni fursa ya kuwakutanisha watu kutoka katika tamaduni mbalimbali, kielelezo cha ujenzi wa ulimwengu shirikishi. Ushuhuda unaotolewa na wanamichezo uwe ni mfano bora wa kuigwa na vijana wa kizazi kipya. Michezo ni wakati muafaka wa kuonja: uzuri na utakatifu wa kazi ya uumbaji kwa kukutana na watu walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Wanamichezo wa kweli ni wajumbe na mashuhuda wa Kristo Mfufuka wanapokuwa uwanjani.

Kauli mbiu: Citius, Altius, Fortius na Pamoja
Kauli mbiu: Citius, Altius, Fortius na Pamoja

Ni katika muktadha wa Michezo ya Olimpiki ya Paris kwa Mwaka 2024 Chama cha Wanamichezo wa Vatican kimewaandikia Barua ya wazi wanariadha wa Vatican kuhusu ushiriki wao katika mashindano haya. Hiki ni kipindi ambacho vita sehemu mbalimbali za dunia bado inaendelea kurindima, kuna misigano na mipasuko ya kijamii katika ngazi ya Kimataifa inayoendelea, kumbe, kipindi cha Mashindano ya Olympiki iwe ni fursa ya kusitisha vita, mapigano na kinzani hizi na muda huu uwe ni kwa ajili ya ujenzi wa umoja na mshikamano wa udugu wa kibinadamu, kwa kutumia lugha ya michezo inayoeleweka na wote. Huu ni muda muafaka kwa wanamichezo Jijini Paris kujikita katika kukuza na kumwilisha tunu msingi za michezo kama vile: shauku, ujumuishaji, udugu wa kibinadamu, moyo wa timu, uaminifu, ukombozi, sadaka na majitoleo. Katika kipindi cha mazoezi, wanamichezo wanaweza kushinda changamoto na ugumu wanaokabiliana nao, huu ndio ujasiri unaoletwa katika Michezo ya Olimpiki ya Paris kwa Mwaka 2024. Michezo hii ni marathoni ya maisha inayowashirikisha wanamichezo wengi kutoka sehemu mbalimbali za dunia na kwamba, kiini cha Michezo huu ni amani inayopaswa kumwilishwa wakati wote wa mashindano haya, ili kupandikiza mbegu ya matumaini kwa watu walioathirika kwa vita, watu wanaosiginwa utu, heshima na haki zao msingi kwa umaskini, ukosefu wa haki, kinzani na woga, tayari kujenga na kudumisha umoja na udugu wa kibinadamu kwa kusitisha vita. Mwaka 1894 Bwana Pierre de Coubertin alijitosa kuhamasisha tena michezo ya Olimpiki miongoni mwa Jumuiya ya Kimataifa kwa kuanzisha mashindano ya michezo mbalimbali, ikiongozwa na kauli mbiu iliyojulikana kwa lugha ya Kilatini kuwa ni "Citius, Altius, Fortius" yaani: Kasi, Lenga juu zaidi na kwa Nguvu."

Michezo ni shule ya upendo, mshikamano na udugu
Michezo ni shule ya upendo, mshikamano na udugu

Mashindano ya Michezo ya Olimpiki ya Tokyo, Japan 2020 yalizinduliwa mjini Tokyo nchini Japan tarehe 23 Julai 2021baada ya kuahirishwa kwa muda wa mwaka mmoja kutokana na tishio la janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 na katika kauli hii mbiu wakaongeza neno “Pamoja.” Huu ni mwaliko kwa wanamichezo kujenga na kudumisha ushirika na Baba Mtakatifu Francisko anakazia kuhusu mchakato wa ujenzi wa udugu wa kibinadamu, ili kudumisha ushirika. Anawataka wanamichezo kutekeleza ndoto zao na kwamba, hii ni fursa inayopaswa kutumiwa kikamilifu na kuendelea kuwa na moyo wa shukrani badala ya kujikita katika fedha, faida na mafanikio kwa gharama zozote zile mambo ambayo yanawafanya wanamichezo wengi kupoteza ile furaha ya michezo. Wanamichezo wahakikishe kwamba wanapata ushindi wa haki, kwani michezo ni fursa ya matumaini kwa kila mwanariadha na binadamu wote katika ujumla wao. Michezo ni mahali pa kujenga na kukuza fadhila ya amani, ili kwa pamoja waweze kushinda kombe la udugu wa kibinadamu.

Kufaulu au kushindwa kwenye michezo ni ukweli mchungu
Kufaulu au kushindwa kwenye michezo ni ukweli mchungu

Baba Mtakatifu Francisko anasema hata wanamichezo wanaweza kuwa ni watakatifu, kwani daima wanaitwa na kuhamasishwa kuendeleza mchakato wa maboresho ya maisha yao kila kukicha! Michezo inapania kujenga na kuimarisha urafiki na udugu wa kibinadamu kati ya watu; kukuza na kudumisha maelewano na amani; kuheshimiana, maridhiano na utulivu kwa kuthamini tofauti zinazojitokeza kati ya watu. Tunu msingi za michezo zinapaswa kusisitizwa miongoni mwa vijana na watoto, ili kuwasaidia kutambua kwamba, kila fursa iliyopo inaweza kutumika kwa ajili ya maboresho ya maisha ya mtu: kiroho na kimwili. Kufaulu na kushindwa katika masuala ya michezo ni ukweli usioweza kupingika. Hii iwe ni fursa ya kuweza kukabiliana na changamoto mbalimbali za maisha kwa ujasiri na moyo mkuu; kwa kuzingatia na kuheshimu sheria, kanuni, maadili na utu wema; mambo yanayopaswa kupewa kipaumbele cha kwanza katika masuala ya michezo. Lakini inasikitisha kuona kwamba, nyakati hizi, michezo inahusishwa sana na masuala ya kiuchumi, mashindano yasiyokuwa na tija, vurugu pamoja na ubaguzi kwa wale ambao hawana kiwango cha juu cha ushindi. Mashindano ya kimataifa, yamekuwa ni kichaka cha biashara na matumizi haramu ya dawa za kulevya; biashara ya binadamu na viungo vyake pamoja na umati mkubwa wa wasichana na wanawake kutumbukizwa katika utalii wa ngono pamoja na mifumo yote ya utumwa mamboleo.

Olimpiki 2024 Paris
25 July 2024, 15:34