Misingi ya Diplomasia ya Vatican: Amani, Utu, Heshima na Haki Msingi za Binadamu
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Damu ya mashuhuda wa imani, ni amana na utajiri mkubwa wa Kanisa na kwamba, damu yao ni mbegu ya Ukristo mpya! Kumbe, Wakristo wanahamasishwa kuishi kwa furaha; kwa kutangaza na kushuhudia imani yao kama anavyokazia Baba Mtakatifu Francisko, daima wakionesha upendo na msamaha; kwa kuendelea kuwa ni wajenzi wa umoja, na mshikamano wa kitaifa; kwa kuheshimiana na kuthaminiana. Kwa njia hii, wataweza kuwa kweli ni wajenzi wa haki, amani na upatanisho, kwa kutambua kwamba, Kanisa ni Sakramenti ya umoja na wokovu kwa watu wote. Kumbe, waamini wanahamasishwa kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa Kanisa. Mashuhuda wa imani kwa njia ya mahubiri na maisha yao adili na matakatifu wamepandikiza mbegu ya Ukristo nchini Italia, Slovenia, Austria, Croatia, Ujerumani hadi Hungaria. Askofu mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu mkuu wa Mambo ya Nchi za Nje, Ushirikiano na Mashirika ya Kimataifa anasema, Kumbukizi ya Sherehe ya Mashuhuda wa imani ni mwaliko kwa waamini kuendelea kujikita katika ujenzi wa jamii inayosimikwa katika utu, heshima na haki msingi za binadamu na maridhiano kati ya watu wa Mataifa, ili hatimaye kuenzi amani duniani. "Aquileia Magistra Pacis," Kwa hakika Aguileia ni mji wa amani, ulioko njia panda, unataka kuwarithisha wananchi wake tunu msingi za maisha ya kiroho na kwamba, Diplomasia ya Vatican na Kanisa katika ujumla wake, kimsingi inakazia kwa namna ya pekee kabisa: huduma makini ya maendeleo endelevu ya binadamu; kusimama kidete kulinda na kudumisha: utu, heshima na haki msingi za binadamu; amani na maridhiano kati ya watu; huduma makini kwa wakimbizi na wahamiaji duniani; elimu, afya, biashara, mawasiliano, ushirikiano na mshikamano wa Jumuiya ya Kimataifa pamoja na haki miliki ya kiakili. Lengo ni kusaidia kukoleza ujenzi wa amani duniani, na maridhiano ya watu.
Jimbo kuu la Gorizia na Friuli Venezia Giulia tarehe 12 Julai 2024 zimeadhimisha Sherehe ya Mashuhuda wa Imani Kijimbo. Mashuhuda wa imani walichangia sana ustawi, maendeleo na mafao ya Kanisa; wakawaimarisha watu kwa imani, ushirika, liturujia, nidhamu pamoja na elimu ya usanifu wa majengo. Jambo la msingi kwa waamini ni kujiaminisha kwa Roho Mtakatifu na kwamba, kiini cha ujumbe wa Habari Njema ya Wokovu ni kwamba, “Kristo Yesu, alitwaa mwili akakaa kwetu, akateswa, akafa na kufufuka kwa wafu na ameketi kuume kwa Baba kwa utukufu.” Hiki ndicho Kiini cha Fundisho la Imani yaani “Kerygma.” Amana na utajiri huu ukajimwilisha katika tasaufi na sanaa, kiasi cha kuwajengea sanaa na utamaduni wa majadiliano; tunu msingi za maisha ya kijamii, kiroho na kiliturujia zilizowawezesha waamini kukabiliana na majanga mbalimbali katika maisha yao. Ni katika utajiri huu, mji wa Nova Gorica na Gorizia imechaguliwa kuwa ni miji ya Kitamaduni Barani Ulaya kwa Mwaka 2025, alama ya matumaini kama anavyosema Baba Mtakatifu Francisko kama sehemu ya Maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025 ya Ukristo. Diplomasia ya Vatican inatoa kipaumbele cha pekee kwa uhuru wa kidini, utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu, bila kusahau utunzaji bora wa mazingira. Kutambua na kuheshimu haki msingi za binadamu ni hatua muhimu sana ya maendeleo fungamani kwani mizizi ya haki za binadamu inafumbatwa katika hadhi, heshima na utu wa binadamu. Huu ni mwaliko kwa Jumuiya ya Kimataifa kuheshimu Sheria za Kimataifa ili kujenga amani inayojikita katika msingi wa majadiliano na upatanisho na kwamba, hii ni diplomasia ya huruma ya Mungu, inayovunjilia mbali chuki, hasira na uhasama kati ya watu wa Mataifa. Kumbe, kuna haja ya kukuza na kudumisha: ushirikiano na mshikamano unaosimikwa kwenye: Kanuni ya auni, udugu wa kibinadamu, ili kudumisha haki na amani na kwamba, hizi ni tunu msingi za maisha ya kimadili na kijamii.
Askofu mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu mkuu wa Mambo ya Nchi za Nje, Ushirikiano na Mashirika ya Kimataifa anasema Vatican imeendelea kujipambanua kwa ajili ya kutafuta na kudumisha amani huko: Ukraine, Palestina, Israeli, Azerbaigan, Myanmar, Ethiopia, Sudan na Yemen. Mtakatifu Yohane XXIII katika Wosia wake wa Kitume, “Pacem in terris” yaani “Amani Duniani” anasema amani ya kweli inasimikwa katika: ukweli, haki, upendo na uhuru. Kumbe, kuna haja ya kukuza na kudumisha utamaduni wa kuheshimu: utu, heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu sanjari na haki msingi za binadamu na kwamba, kila mtu anapaswa kuwajibika, ili kujenga na kuimarisha mafungamano ya kijamii na mahusiano pamoja na Mwenyezi Mungu. Kumbe, jambo la msingi ni kujenga mshikamano wa dhati, utawala wa sheria na demokrasia sanjari na uhuru wa kidini. Hija za Kitume zinazotekelezwa na Baba Mtakatifu Francisko sehemu mbalimbali za dunia zinalenga pamoja na mambo mengine: ni kujenga madaraja ya kuwakutanisha watu, ili kuimarisha udugu wa kibinadamu; kwa kukazia heshima na haki msingi za kibinadamu licha ya tofauti zao msingi za: Makabila, dini na tamaduni. Kamwe tofauti hizi zisiwe ni chanzo cha vita, kinzani na mipasuko ya kijamii. Diplomasia ya Vatican inajikita katika Mafundisho Jamii ya Kanisa. Mafundisho Jamii ya Kanisa yanapata chimbuko lake mintarafu kanuni na muundo wa elimu fahamu, taalimungu, hususan taalimungu maadili ambayo ni dira na mwongozo wa maisha ya watu. Yanachota amana na utajiri wake kutoka katika Maandiko Matakatifu na Mapokeo ya Kanisa na imani thabiti ambayo inamwilisha Neno la Mungu katika matendo, kielelezo cha imani tendaji. Mambo msingi katika mchakato wa kudumisha haki msingi za binadamu: Amani katika ukweli, haki, upendo na uhuru.
Hizi ni tunu ambazo ni urithi mkubwa kwa binadamu wote kwani zinabubujika kutoka katika asili ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu hivyo zinapaswa kulindwa, kutetewa na kuheshimiwa na wote; kwa kuzingatia kwamba, haki inakwenda sanjari na wajibu; hakuna haki pasi na wajibu. Hii ni haki ya kuishi, kupata huduma bora ya makazi, afya, elimu, kuabudu, uhuru wa dhamiri, uhuru wa kuchagua mfumo wa maisha; haki za kiuchumi na kisiasa pamoja na uhuru wa kwenda unakotaka kwa kuzingatia sheria na kanuni zilizopo. Kanisa Katoliki lina amana na utajiri mkubwa wa Mafundisho Jamii ya Kanisa yanayopata chimbuko lake katika Waraka wa Kichungaji wa Baba Mtakatifu Leo XIII; Mambo Mapya; Rerum Novarum. Askofu mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu mkuu wa Mambo ya Nchi za Nje, Ushirikiano na Mashirika ya Kimataifa, amehitimisha hotuba yake kwa kukazia amani, maridhiano kati ya watu wa Mataifa; Ujenzi wa mshikamano na udugu wa kibinadamu, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi na kwa ajili ya mtu mmoja mmoja. Tofauti msingi kati ya watu wa Mataifa ni amana na utajiri wa kulindwa na kudumishwa: Waamini wawe ni vyombo na wajenzi wa matumaini.