Kuelekea Jubilei ya Wamisionari wa kidijitali na washawishi wa Kikatoliki 2025!
Vatican News
Katika muda wa chini ya mwaka mmoja tu, Roma inaandaa hafla ya Jubilei inayokusanya hata wamisionari wa kidijitali na washawishi wa Kikatoliki kutoka ulimwenguni kote. Tarehe 28 na 29 Julai 2025, kabla ya Jubilei ya Vijana, kwa wale waliojitolea kueneza Injili kupitia mitandao ya kijamii watakutana kwa ajili ya Jubilei yao wenyewe. Huu utakuwa ni muunganiko wa watu wengi waliokutana kwa mara ya kwanza katika Siku ya Vijana Ulimwenguni(WYD) huko Lisbon mnamo kiangazi cha 2023. Wakati wa tukio hilo, hata hivyo Kardinali José Tolentino de Mendonça, Mwenyekiti wa Baraza Kipapa la Utamaduni na Elimu, aliwaeleza vijana washawishi katika mahubiri yake kwamba: “Leo, Kanisa linawahitaji ninyi, wapenzi wa ushawishi wa kidigitali, kuleta matumaini katika nafasi hizi mpya za kijamii. Hiyo ni mitandao ya vyombo vya habari na mitandao ya kijamii.”
Sehemu ya maisha ya umisionari wa Kanisa
Papa Francisko vile vile aliwahimiza wamisionari wa kidijitali kujiona kama jumuiya, yaani: “sehemu ya maisha ya kimisionari ya Kanisa, ambayo haijawahi kuogopa kujitosa katika upeo na mipaka mipya. Kwa ubunifu na ujasiri, tangazeni Huruma ya Mungu.”Kwa hiyo Jubilee hii inalenga kukuza hisia ya jumuiya na ushirika miongoni mwa wamisionari wa kidijitali. Itakuwa nafasi kwa jumuiya hii ya wamisionari, iliyounganishwa na utume wa pamoja, kukusanyika na kupita katika Mlango Mtakatifu katika mwaka wa Jubilei.
Mkutano wa kwanza wa Wamisionari wa Kidijitali huko Aparecida
Ni katika fursa hiyo ambapo tarehe 13 Julai 2024 huko Aparecida umetayarishwa kufanyika Mkutano wa kwanza wa Kitaifa wa Wamisionari wa Kidijitali nchini Brazili. Tukio hili limehamasishwa na Tume ya Maaskofu ya Mawasiliano ya Kijamii(Cepac)ya Baraza la Maaskofu wa Brazili(CNBB), kwa ushirikiano na Tume ya Maaskofu ya Vijana, Mtakatifu Carona, Igrejeiros, Madhabahu ya Roho ya Branding, Pascom Brasil, na Vijana wa Kidijitali. Mkutano huo, unaoongozwa na mada: “Tupeni Nyavu”utaoongozwa na Injili ya Luka, ambao utafunguliwa saa 3.00 asubuhi hadi saa 12.00 jioni.
Kukumbatia Sinodi katika ulimwengu wa kidijitali
Askofu Amilton Manoel da Silva wa Guarapuava, mjumbe wa Cepac CNBB, alisisitiza umuhimu wa kutembea pamoja akisema:“tunaishi wakati maalum katika Kanisa, na Papa Francisko anatuhimiza kuishi sinodi, tuungane na kuutafuta umoja katika Kristo Yesu, tukikuza ushirika kati yetu.” Alibainisha pia kwamba mazingira ya kisasa ya kidijitali yanatoa fursa ya pekee ya kueneza neno la Mungu na kujenga Ufalme, na kuwahimiza watu kuvuka hali ya kutoridhika na kutojali na kugundua upya maajabu ya Yesu Kristo na Injili.
Washawishi wa Kikatoliki na mazungumzo katika Roho
Mkutano huo utawashirikisha Monsinyo Lucio Adrian Ruiz, Katibu wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano, pamoja na maaskofu wengine wa Cepac na Tume ya Vijana. Watajihusisha katika mijadala ili kuimarisha kujitolea kwa uinjilishaji wa kidijitali. Tume ya Mawasiliano ya Kijamii ya CNBB imealika idadi ndogo ya wamisionari wa kidijitali kwenye mkutano huu wa kwanza lakini inapanga kupanua mikusanyiko ya siku zijazo ili kuongeza ushiriki na juhudi za utume wa kimisioanti katika jukwaa la kidijitali. Tukio hilo litajumuisha mazungumzo, kusikiliza, ushiriki, na meza za mduara kwa kutumia mbinu ya Mazungumzo katika Roho, ambayo inasisitiza utambuzi na sinodi. Pia kutakuwa na nyakati za mafunzo ya kiroho, sala, na adhimisho la Ekaristi, kutoa fursa ya kuimarisha imani na ushirika kati ya washiriki.