Tafuta

Wanachama wa Chama cha Mama Yetu wa Lourdes - San Luigi wanasema wanaendelea kumsindikiza Mheshimiwa Padre Albert Msafiri Lubuva wa Jimbo Kuu la Dodoma, nchini Tanzania kwa sala na sadaka zao. Wanachama wa Chama cha Mama Yetu wa Lourdes - San Luigi wanasema wanaendelea kumsindikiza Mheshimiwa Padre Albert Msafiri Lubuva wa Jimbo Kuu la Dodoma, nchini Tanzania kwa sala na sadaka zao. 

Padre Albert Msafiri Lubuva Azindua Jubilei ya Miaka 25 ya Upadre

Wanachama wa Chama cha Mama Yetu wa Lourdes - San Luigi wanasema wanaendelea kumsindikiza Mheshimiwa Padre Albert Msafiri Lubuva kwa sala na sadaka zao ili aweze kutekeleza vyema dhamana na utume wa kuwaongoza, kuwafundisha na kuwatakatifuza watu wa Mungu, lakini zaidi kwa kuwaimarisha katika imani, matumaini na mapendo wakati huu anapoadhimisha Jubilei ya Miaka 25 tangu alipopewa Daraja Takatifu ya Upadre tarehe 15 Agosti 1999.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mtakatifu Yohane Paulo II anasema, Daraja Takatifu ya Upadre ni fumbo ambalo linamwezesha Mwenyezi Mungu kuwateuwa baadhi ya waamini ili kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu. Wakleri wanakumbushwa daima kwamba, si wao waliomchagua Yeye, bali ni Yeye aliyewachagua wao na kuwaweka kwenda kuzaa matunda, na matunda yao yapate kukaa. Daraja Takatifu ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu “Na hapana mtu ajitwaliaye mwenyewe heshima hii, ila yeye aitwaye na Mungu, kama vile Haruni.” Ebr 5:4. Mapadre, kwa ajili ya Daraja takatifu na ya utume wanaopewa na Maaskofu, wanapokelewa kumtumikia Kristo aliye Mwalimu, Kuhani na Mfalme; nao wanashiriki huduma yake, ambayo kwayo hapa duniani, Kanisa hujengwa bila kukoma kuwa Taifa la Mungu, Mwili wa Kristo na Hekalu la Roho Mtakatifu. Presbiterorum ordins, 1. Hivyo Mapadre wanapaswa kuwa ni watumishi waaminifu wa Mafumbo ya Kanisa; wanaotolea Sadaka Takatifu ya Misa, kiini cha maisha na wito wa Kipadre.

Padre Albert  Lubuva amezindua maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 25 ya Upadre
Padre Albert Lubuva amezindua maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 25 ya Upadre

Mapadre wanaendeleza ile Sadaka ya Kristo Yesu Msalabani, “Fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu na kwamba, hili ni Fumbo la Imani.” Mapadre wakumbuke kwamba, wanashirikishwa leo ya Kristo Yesu, kama vyombo na mashuhuda wa huruma, upendo na msamaha wa Mungu kwa waja wake. Wanaitwa kuwa ni waadilifu, wema na watakatifu wa Mungu, katika kuwahudumia watu wa Mungu katika mahitaji yao msingi: kiroho na kimwili: “Cura animalum.” Utakatifu wa Mapadre unapata chimbuko lake katika maisha ya sala, tafakari ya Neno la Mungu sanjari na maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa kwa uchaji na Ibada. Padre anapaswa kuwa ni mhudumu wa Neno la Mungu, tayari kulitangaza na kulishuhudia kama sehemu ya mchakato wa uinjilishaji wa kina. Padre anapaswa kuwa ni chombo cha majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni.

Daraja Takatifu ni Fumbo na Zawadi
Daraja Takatifu ni Fumbo na Zawadi

Wanachama wa Chama cha Mama Yetu wa Lourdes - San Luigi wanasema wanaendelea kumsindikiza Mheshimiwa Padre Albert Msafiri Lubuva wa Jimbo Kuu la Dodoma, nchini Tanzania kwa sala na sadaka zao ili aweze kutekeleza vyema dhamana na utume wa kuwaongoza, kuwafundisha na kuwatakatifuza watu wa Mungu, lakini zaidi kwa kuwaimarisha katika imani, matumaini na mapendo wakati huu anapoadhimisha Jubilei ya Miaka 25 tangu alipopewa Daraja Takatifu ya Upadre tarehe 15 Agosti 1999. Wanamshukuru Padre Albert Msafiri Lubuva kwa sadaka na majitoleo yake kwa ajili ya Kristo Yesu na Kanisa lake, katika kipindi chote cha miaka ishirini na mitano ya maisha, wito na huduma ya Kipadre na kati ya miaka hiyo, takribani miaka saba amewahudumia wanachama hao wanaoishi kwenye Parokia ya Missaglia, Jimbo kuu la Milano, Italia. Tarehe 7 Julai 2024 Padre Albert Msafiri Lubuva amezindua rasmi maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 25 ya Daraja Takatifu ya Upadre. Tarehe 15 Agosti 2024 anatarajia kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu Parokiani Korogwe, Jimbo Katoliki la Tanga, Tarehe 17 Agosti 2024 ataungana na Mapadre wa Jimbo kuu la Dodoma, kumwimbia Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa Daraja Takatifu ya Padre, Ibada itakayoongozwa na Askofu mkuu Beatus Kinyaiya O.F.M.Cap. na tarehe 18 Agosti 2024 kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Paulo wa Msalaba, Padre Albert Msafiri Lubuva ataadhimisha Ibada ya Misa takatifu. Tarehe 25 Septemba 2024 Askofu Msaidizi Wilbroad Henry Kibozi wa Jimbo kuu la Dodoma, ataungana na watu wa Mungu Parokia ya Missaglia kumshukuru Mungu kwa Jubilei ya Miaka 25 ya Daraja Takatifu ya Upadre kwa ajili ya Padre Albert Msafiri Lubuva.  Uzinduzi wa maadhimisho ya Sherehe ya Jubilei ya Miaka 25 ya Daraja Takatifu ya Upadre imehudhuriwa pia na Padre Timoth Maganga Nyasulu, Paroko wa Parokia ya Mtakatifu Polycarp, Askofu na Shahidi anayeadhimisha pia Jubilei ya Miaka 25 ya Daraja takatifu ya Upadre mwaka 2024.

Mapadre ni watumishi waamini wa Mafumbo ya Kanisa
Mapadre ni watumishi waamini wa Mafumbo ya Kanisa

Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S., katika mahubiri yake alikazia umuhimu wa toba na wongofu wa kichungaji ili kuweza kukabiliana na changamoto zinazoendelea kujitokeza katika maisha na utume wa Kanisa; wongofu wa kimisionari tayari kuendelea kusoma alama za nyakati. Kwnai huu ni mwaliko wa kuziinjilisha tamaduni ili kuitamadunisha Injili ili hatimaye, mchakato wa Uinjilishaji uweze kutoa mwanga kwa changamoto mamboleo kuhusiana na Mungu, jirani pamoja na tunu msingi za kiinjili. “Ni lazima uinjilishaji huo ufike kule ambako maelezo na mielekeo mipya vinaundwa, ili kufikisha Neno la Yesu kwenye roho ndani kabisa ya miji yetu.” Evangelii gaudium, 74. Hapa kuna umuhimu wa kuziinjilisha tamaduni ili kuitamadunisha Injili. “Tazama, wakati uliokubalika ndio sasa; tazama, siku ya wokovu ndiyo sasa.” 2Kor 6:2. Baba Mtakatifu Francisko anakazia ushuhuda unaomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya waamini. Kuna umuhimu wa kujikita katika wongofu wa Kiikolojia, kwa kulinda na kutunza mazingira bora nyumba ya wote.

Baadhi ya wageni waliohudhuria kwenye uzinduzi wa Jubilei
Baadhi ya wageni waliohudhuria kwenye uzinduzi wa Jubilei

Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S., aliwataka waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kuendelea kusali ili Bwana wa mavuno apelike watenda kazi wema, watakatifu na wachamungu katika shamba lake. Wawaombee Mapadre watakaojisadaka kila siku kwa ajili ya kuadhimisha Mafumbo ya Kanisa; watakaowalisha waamini kwa Neno na Mkate wa uzima wa milele; watakaoboresha Liturujia ya Kanisa, ili waamini wengi waweze kushiriki kikamilifu na wala si kuwa ni watazamaji na wasindikizaji; Mapadre watakaojisadaka kwa ajili ya katekesi kwa watoto wadogo na wanafunzi mashuleni; watakaowasaidia vijana kukuza ndani mwao hofu ya Mungu; Mapadre watakaotangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu; Mapadre watakaochochea ari na mwamko wa toba ya ndani na utakatifu wa maisha; watakaosaidia kuimarisha imani miongoni mwa watu wa Mungu; Waamini wamwombe Mwenyezi Mungu ili awapelekee Mapadre watakaokuwa wepesi kuwashika mkono na kuwanyanyua wale walioteleza na kuanguka katika udhaifu wa maisha yao, ili waweze kujipatanisha na Mungu tayari kuambata na kufumbata kanuni maadili na utu wema. Waamini waendelee kusali na kumwomba Mwenyezi Mungu awaletee Mapadre watakaosimamia utakatifu wa maisha na tunu msingi za ndoa na familia; Mapadre watakaokuwa ni faraja kwa wagonjwa na wale waliokufani; Mapadre watakaokuwa ni vyombo vya amani na matumaini kwa wale waliovunjika na kupondeka moyo!

Jubilei Miaka 25 ya Upadre
08 July 2024, 15:44