Papa amemteua Padre Ronzani(OSA)kuwa Mwenyekiti wa Pango Hifadhi la Nyakara za Kitume Vatican
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko Ijumaa tarehe 5 Julai 2024, amemteu Mwenyekiti wa Pango Hifadhi la Nyakara za Kitume Vatican, Padre Rocco Ronzani,(O.S.A.,) ambaye hadi uteuzi huo alikuwa ni Profesa wa Mafunzo ya Mababa wa Kanisa katika Taasisi ya Kipapa ya Baba wa Kanisa Augustinianum, Roma.
Padre Ronzani wa Shirika la Mtakatifu Agostino (O.S.A) alizaliwa Roma mnamo tarehe 21 Februari 1978. Alijiunga na Shirika la Waagostiniani mnamo mwaka 1997 na kufunga nadhiri za daima mnamo tarehe 1 Novemba 2002. Mnamo tarehe 27 Juni 2004 alipewa daraja la Upadre. Na kunako mwaka 2010 alipata Shahada ya Udaktari katika Taalimungu na Sayansi za Mababa wa Kanisa katika Tasisi ya Kipapa ya Baba wa Kanisa Augustinianum, Roma, mahali ambapo anafundisha hadi sasa.
Jukumu jingine ambalo analo ni Mshauri wa Baraza la Kipapa la Kuwatangaza Watakatifu, lakini pia ni Mkurugenzi wa Pango hifadhi la Kihistoria la Kanda ya Waagostiniani Nchini Italia na Mkufunzi katika Kitengo cha Taalimungu katika Chuo Kikuu cha Kipapa cha Laterano Roma.