Askofu Peter Kimani Ndung’u Jimbo Katoliki la Embu, Nchini Kenya
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Sherehe ya Bikira Maria Kupalizwa Mbinguni mwili na roho, tarehe 15 Agosti 2024 amemteuwa Mheshimiwa sana Padre Peter Kimani Ndung’u, kutoka Jimbo kuu la Nairobi, kuwa Askofu mpya wa Jimbo Katoliki la Embu, nchini Kenya. Hadi kuteuliwa kwake, Askofu mteule Peter Kimani Ndung’u alikuwa ni Padre mhudumu wa maisha ya kiroho kwenye magereza nchini Kenya. Itakumbukwa kwamba, Askofu mteule Peter Kimani Ndung’u alizaliwa tarehe 11 Novemba 1966 huko Githunguri, Wilayani Kiambu, Jimbo kuu la Nairobi, Kenya. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, tarehe 22 Julai 1995 akapewa Daraja ya Upadre kwa ajili ya Jimbo kuu la Nairobi, Kenya.
Katika maisha na utume wake kama Padre amewahi kuwa Paroko usu na hatimaye Paroko wa Parokia ya Rozari Takatifu huko Kamwangi tangu mwaka 1999 hadi mwaka 2001. Tangu mwaka 2001 hadi kuteuliwa kwake alikuwa ni Mhudumu wa maisha ya kiroho kwenye magereza nchini Kenya. Amejiendeleza katika masuala ya mawasiliano, saikolojia na kwamba tangu mwaka 2008 aliteuliwa kuwa ni Mwakilishi kutoka Barani Afrika kwenye Tume ya Kikatoliki Kimataifa kwa ajili ya Utume wa Shughuli za Kichungaji Magerezani, ICCPPC.