Askofu Wallace Ng’ang’a Gachihi Jimbo Katoliki la Kijeshi Nchini Kenya
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko katika Maadhimisho ya Sherehe ya Bikira Maria Kupalizwa mbinguni mwili na roho, tarehe 15 Agosti 2024 amemteuwa Askofu Msaidizi Wallace Ng’ang’a Gachihi wa Jimbo kuu la Nairobi kuwa Askofu wa Jimbo la Kijeshi nchini Kenya. Itakumbukwa kwamba, Askofu Wallace Ng’ang’a Gachihi wa Jimbo la Kijeshi nchini Kenya, alizaliwa tarehe 26 Machi 1973 huko Gatundu, Wilaya ya Kiambu, Jimbo kuu la Nairobi. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, tarehe 21 Mei 2005 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre kwa ajili ya Jimbo kuu la Nairobi. Baada ya kupewa Daraja Takatifu amelitumikia Kanisa kama Paroko-usu na hatimaye kama Paroko kuanzia mwaka 2006 hadi mwaka 2009.
Kuanzia Mwaka 2009 hadi mwaka 2011 akatumwa na Jimbo kuu la Nairobi kwenda kuongeza ujuzi na maarifa katika Taalimungu ya shughuli za kichungaji na hatimaye, akajipatia Shahada ya Uzamivu toka Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Afrika Mashariki na Kati, CUEA. Baada ya masomo yake, akapangiwa kuwa Paroko-usu katika Parokia ya Malkia wa Mbingu “Regina Coeli” kuanzia mwaka 2009 hadi 2015, Paroko wa Parokia ya Kristo Yesu Mfalme, “Christ the King”, Embakasi tangu mwaka 2015 hadi mwaka 2024. Amekuwa Mratibu wa shughuli za kichungaji Jimbo kuu la Nairobi kuanzia mwaka 2011 hadi mwaka 2024 na alikuwa ni Mjumbe katika Baraza kuu la Washauri wa Jimbo kuu la Nairobi. Tarehe 13 Februari 2024, Baba Mtakatifu Francisko akamteuwa kuwa Askofu Msaidizi wa Jimbo kuu la Nairobi, na kuwekwa wakfu tarehe 6 Aprili 2024. Na tarehe 15 Agosti 2024 Baba Mtakatifu Francisko amemteuwa tena kuwa Askofu wa Jimbo la Kijeshi nchini Kenya.