Tafuta

2024.08.22 Madhabahu ya Mama Yetu wa Chandavila, La Codosera, nchini Hispania. 2024.08.22 Madhabahu ya Mama Yetu wa Chandavila, La Codosera, nchini Hispania. 

Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa:Kutoa idhini ya Bikira wa Huzuni wa Chandavila

Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa limetoa idhini yake kuwa 'hakuna kizuizi kilichopendekezwa na Askofu Mkuu wa Mérida-Badajoz kuhusu ibada inayohusishwa na Madhabahu ya Chandavila,nchini Hispania.'Mama Maria alionekana kwa vijana wawili kama Mama Yetu wa Huzuni,katika mji wa Chandavila huko Extremadura karibu na mpaka na Ureno 1945.

Vatican News

Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa “kwa hiari linatoa idhini yake” kwa Askofu Mkuu wa Mérida-Badajoz, Askofu Mkuu José Rodríguez Carballo, kuendelea na tamko la "nihil obstat" yaani 'hakuna kizuizi' lililopendekezwa, ili “madhabahu ya Chandavila, mrithi wa historia tele ya usahihi, maneno machache na ibada nyingi, iweze kuendelea kuwatolea huduma waamini wanaotaka kulikaribia, mahali pa amani ya ndani, faraja na uwongofu”. Hiki ndicho alichoandika Kardinali Victor Manuel Fernández, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa katika barua, iliyoidhinishwa na Papa Francisko  tarehe 22 Agosti 2024, akijibu barua kutoka kwa Askofu wa Hispania ya tarehe 28 Julai 2024 kuhusu matukio hayo, yaliyoanzia mnamo 1945. Hili ni tukio la vijana wawili ambao Maria alionekana kwao, kama Mama Yetu wa Huzuni, katika mji wa Chandavila, huko Extremadura nchini Hispania, karibu na mpaka na Ureno. Kulingana na Kanuni zilizochapishwa mnamo tarehe 17 Mei 2024 na Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa lilibainisha kuwa "kwa idhini, hata kama hakuna uhakika unaooneshwa juu ya uhalisi usio wa kawaida wa jambo hilo, ishara nyingi za utendaji wa Roho Mtakatifu zinatambulika” ambapo “askofu wa jimbo anahimizwa kuthamini thamani ya kichungaji na pia kuendeleza uenezaji wa pendekezo hili la kiroho, pia kwa njia ya hija inayowezekana ya mahali patakatifu”, huku waamini walioidhinishwa kutoa ushirikiano wao “kwa njia ya busara.”

Matukio ya Marcelina na Afra

Ibada kwa Bikira wa Huzuni huko Chandavila ilizaliwa kuelekea mwisho wa Vita vya Pili vya Kidunia na uzoefu wa kiroho ambao wasichana wawili, Marcelina Barroso Expósito wa miaka kumi na Afra Brígido Blanco wa miaka kumi na saba, walikuwa nao tofauti katika hili eneo kuanzia Mei 1945. Kardinali Fernández anaandika kuwa “Marcelina anasema kwamba, mwanzoni, aliona umbo la giza angani, ambalo wakati mwingine lilizidi kuwa nyepesi, kana kwamba ni Bikira wa Huzuni, na vazi jeusi lililojaa nyota, kwenye mti wa chestnut(castagno.) Lakini uzoefu wa kina wa msichana huyu, zaidi ya maono, ulikuwa ni wa kuhisi kumbatio na busu ambalo Bikira alimpatia kwenye paji la uso. Uhakikisho huu wa ukaribu wa upendo wa Mama Yetu labda ndiyo ujumbe mzuri zaidi,” alibainisha Kardinali. “Ingawa, kadiri siku zilivyopita, yeye na Afra walimtambua mtu huyo kuwa ni Bikira wa Huzuni, kinachodhihirika zaidi ni uwepo wa Bikira unaotia faraja, na uaminifu. Wakati Bikira anaomba Marcelina kutembea kwa magoti kupitia njia yenye maganda makavu ya miti ya matunda ya chestnut, miiba na mawe makali, havikumfanya na kumsababishia mateso. Kinyume chake, alimwomba uaminifu katika kukabiliana na changamoto hiyo kwamba “Usiogope, hakuna kitakachokupata.”

Upole wa Maria

Mwaliko huu kutoka kwa Mama Yetu wa kuamini upendo wake ulimpatia msichana huyo maskini na anayeteseka matumaini na uzoefu wa kuhisi kuhamasishwa katika hadhi yake. Je! vazi hilo sahihi lililotengenezwa kwa matete na nyasi ambalo Mama Yetu alilinda magoti ya msichana mdogo si udhihirisho mzuri wa huruma ya Maria? Wakati huo huo ilikuwa ni uzoefu wa uzuri, kwa sababu Bikira alionekana kuzungukwa na makundi ya nyota yenye kung'aa, kama yale ambayo yangeweza kupendezwa usiku katika anga safi la vijiji vidogo vya Extremadura.”

Maisha ya busara katika huduma ya wagonjwa, wazee na yatima

Baada ya maono hayo yanayodaiwa, wasichana hao wawili waliishi“maisha ya busara na sio ya kujionesha kabisa wakijitolea kwa kazi za upendo, wakiwatunza wagonjwa, wazee na mayatima na hivyo kuwapelekea wale waliopata faraja tamu ya upendo wa Bikira ambao walikuwa wamefanya uzoefu.

Vipengele vingi vinavyoonesha tendo la Roho

Kardinali Fernández, alimwandikia Askofu Mkuu Rodríguez Carballo  kuwa "Kwa sababu hiyo zote hakuna kitu ambacho kinaweza kupingwa kwa ibada hii nzuri, ambayo inatoa usahihi uleule tunaoweza kuuona kwa Maria wa Nazareti, Mama yetu. Kuna mambo mengi chanya ambayo yanaonesha utendaji wa Roho Mtakatifu kwa mahujaji wengi wanakwenda, Hispania na Ureno, katika uwongofu, uponyaji na ishara nyingine za thamani zinazotokea mahali hapa.” Hatimaye, Kardinali Fernandes anakumbusha juu ya Jubilei ya 2020 katika kumbukumbu ya miaka 75 ya uzoefu wa kiroho uliofanyika huko Chandavila, mwaka wa Jubilei iliyotambuliwa na Askofu wa Mérida-Badajoz “kama baraka ya Jimbo.”

Madhabahu ya Mama Maria Huzuni huko Chandavile

 

23 August 2024, 11:35