Kardinali Baltazar ni mwakilishi wa Papa kwa Kongamano la 53 la Ekaristi Kimataifa,Quito
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Katika kuelekea kwenye Kongamano la 53 la Ekaristi Takatifu Kimataifa, litakalofanyika huko Quito nchini Ecuador kuanzia tarehe 8-15 Septemba 2024, Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi tarehe 24 Agosti 2024, amemteua Mwakilishi wake katika tukio hilo, Kardinali Baltazar Enrique Porras Cardozo, Askofu mkuu Mstaafu wa Caracas. Tukio hilo litafanyika “katika fursa ya miaka 150° tangu kuwekwa wakfu kwa Nchi hiyo kwa Moyo Mtakatifu wa Yesu, ambapo muungano huo wa kikanisa utaonesha matunda ya Ekaristi kwa ajili ya uinjilishaji na upyaishwaji wa imani katika bara la Amerika ya Kusini.”
Kongamano kuanzaia 8 hadi 15 Septemba
Kwa njia hiyo Kamati ya Kongamano la 53 la Ekaristi Takatifu Kimataifa (IEC2024) lililopangwa kufanyika kuanzia tarehe 8 hadi 15 Septemba 2024 linaingia katika awamu ya mwisho sasa ya utendaji. Quito kwa mara nyingine tena itakuwa kitovu cha usikivu wa ulimwengu kwa kusherehekea katika ukumbi wa statio Orbis utakaowaleta pamoja wawakilishi wa Kanisa la kiulimwengu kuzunguka meza ya Ekaristi.
Ishara ya Kongamo la Ekaristi ni Kitabu kikubwa cha Injili
Kamati mahalia ya Ecuador katika fursa hiyo ilichagua kama ishara yake, Kitabu kikubwa cha Injili chenye jalada kubwa la fedha ambalo kwenye bamba la mbele lina picha ya Moyo Mtakatifu wa Yesu. Picha hiyo inawakilisha mchoro ambao Mtakatifu Paulo VI, alitoa zawadi kwa Jimbo Kuu la Quito, wakati wa kuadhimisha miaka 100 ya kuwekwa wakfu kwa nchi hiyo kwa Moyo Mtakatifu wa Yesu. Kwenye jalada la nyuma kumechorwa makabila ya Ecuador yanayowakilishwa pamoja na karama za Roho Mtakatifu.
Baraka kwa Kitabu na kutia sahihi
Na ikumbukwe ilikuwa Siku ya Jumatano tarehe 24 Mei 2024, wajumbe kutoka Ecuador walifika jijini Roma kuwasilisha maendeleo ya Kongamamo la 53 la Ekaristi Kimataifa kwa Kamati ya Kipapa ya Makongamano kimataifa ambapo walishiriki Katekesi iliyofanyika katika Uwanja wa Mtakatifu Petro. Mwisho wa katekesi hiyo wajumbe, wakiongozwa na Askofu Mkuu Alfredo José Espinoza Mateus, wa Jimbo kuu la Quito na Mkuu wa Kanisa la Ecuador, waliwasilisha kitabu kikubwa cha Injili kwa Papa. Baba Mtakatifu Francisko wakati huo alikibariki na kukitia sahihi kwa mkono wake mwenyewe, huku akiandika maneno ya kutia moyo kwa ajili ya maandalizi hayo. Wakati huohuo alituma hata baraka zake kwa Ecuador, akihakikishia maombi yake kwa ajili ya amani katika nchi hiyo ya Amerika Kusini. Katika mahojiano yake na vyombo vya habari vya Vatican, Askofu mkuu Espinoza alibainisha kwamba “Kongamano la Ekaristi Takatifu litakaloadhimishwa hapo mnamo Septemba 2024 – katika kumbukumbu ya miaka 150 tangu nchi hiyo ilipojitolea kwa Moyo Mtakatifu ni baraka kwa Ecuador.”
Kauli mbiu: “Udugu wa Kuponya Ulimwengu”
Askofu Mkuu huyo vile vile aliongeza kuwa, kaulimbiu ya inayoongoza Kongamano hilo: “Udugu wa Kuponya Ulimwengu. Ninyi Nyote ni Ndugu” ni changamoto kubwa kwa nchi hiyo ya Amerika Kusini ambayo inabidi ikabiliane na hali ngumu ya kijamii ambapo ghasia huongezeka na mapambano dhidi ya mauzo ya dawa za kulevya."