Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, Jumatatu tarehe 12 Agosti 2024 amefanya mazungumzo kwa njia ya simu na Rais Masoud Pezeshkian wa Iran. Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, Jumatatu tarehe 12 Agosti 2024 amefanya mazungumzo kwa njia ya simu na Rais Masoud Pezeshkian wa Iran.  (AFP or licensors)

Kardinali Pietro Parolin Azungumza Kwa Simu na Rais Mpya wa Iran

Kardinali Parolin Katibu mkuu wa vatican, ameonesha wasi wasi mkubwa wa Vatican kuhusu amani na utulivu huko Mashariki ya Kati. Vatican inaitaka Iran kuhakikisha kwamba, inajitahidi kufa na kupona ili kuhakikisha kuwa, vita hii haienei tena sehemu nyingine huko Mashariki ya Kati na badala yake, Mataifa yanizatiti katika majadiliano katika ukweli na uwazi; sanjari na amani ya kudumu. Vatican imempongeza Rais Masoud Pezeshkian kwa kuibuka kidedea katika uchaguzi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Dr. Masoud Pezeshkian mwenye umri wa miaka 69, aliibuka mshindi katika uchaguzi wa urais nchini Iran uliofanyika tarehe 6 Julai 2024 na akaidhinishwa rasmi na Kiongozi Mkuu wa Iran Ali Khamenei kuwa Rais wa awamu ya tisa wa Iran na kuapishwa rasmi tarehe 30 Julai 2024 katika hafla iliyofanyika kwenye Bunge mjini Tehran, ambapo maofisa wa ngazi za juu, makamanda wa kijeshi na wawakilishi kutoka nchi 88 na mashirika 10 ya kimataifa walishiriki kwenye Sherehe hii. Kufuatia kiapo chake hicho mbele ya bunge, Rais Masoud Pezeshkian ameelezea malengo ya utawala wake, akijikita katika maendeleo ya kiuchumi, maslahi mapana ya taifa na kuboresha maisha ya wananchi wa Iran. Amezungumzia malengo muhimu ya sera ya mambo ya nje ya nchi ya Iran, yenye lengo la kulinda usalama wa taifa na kuimarisha ustawi wa kiuchumi ndani ya mfumokazi wa "heshima, hekima na manufaa."

Rais mpya wa Iran ameapishwa tarehe 30 Julai 2024
Rais mpya wa Iran ameapishwa tarehe 30 Julai 2024

Rais Masoud Pezeshkian pia amelaani vitendo vya mashambulizi ya Israel huko Ukanda wa Gaza, akikosoa mashambulizi ya makombora dhidi ya raia wasiokuwa na hatia, wakiwemo wanawake na watoto, na wale wanaounga mkono vitendo hivyo. Ni katika muktadha wa ushindi huu na kuanza kushika hatamu za uongozi, Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, Jumatatu tarehe 12 Agosti 2024 amefanya mazungumzo kwa njia ya simu na Rais Masoud Pezeshkian wa Iran.  Kardinali Parolin, ametumia fursa hii kumpongeza kwa kuibuka kidedea katika kinyang’anyiro cha uchaguzi mkuu wa Iran na sasa anaanza kutekeleza dhamana na wajibu wake kama Rais mpya wa Iran. Katika mazungumzo hayo, viongozi hawa wawili wamegusia masuala msingi yanayounganisha Iran na Vatican. Kardinali Parolin, ameonesha wasi wasi mkubwa wa Vatican kuhusu amani na utulivu huko Mashariki ya Kati. Vatican inaitaka Iran kuhakikisha kwamba, inajitahidi kufa na kupona ili kuhakikisha kwamba, vita hii haienei tena sehemu nyingine huko Mashariki ya Kati na badala yake, Mataifa yanajizatiti katika majadiliano katika ukweli na uwazi; sanjari na amani ya kudumu.

Amani Iran 2024
12 August 2024, 15:14