Tafuta

2024.08.29 Madhabahu ya Mama Yetu wa Huruma huko Pellevoisin,Ufaransa. 2024.08.29 Madhabahu ya Mama Yetu wa Huruma huko Pellevoisin,Ufaransa. 

Mama Yetu wa huruma huko Pellevoisin:ibada inayofanya mema

Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa,limeridhia Askofu Mkuu wa Bourges kutoa amri ya “nihil obstat”inayohusiana na ibada iliyounganishwa na Madhabahu ya Maria katika manispaa ndogo ya Ufaransa,ambapo mnamo 1876 mjakazi maskini,Estelle Faguette,alitokewa na maonesho mbalimbali ya Bikira Maria.

Vatican News

Kardinali Victor Manuel Fernández amendika katika barua iliyotumwa kwa Askofu mkuu Jérôme Daniel Beau  wa Bourges nchini Ufaransa na kuidhinishwa na Papa Francisko mnamo Alhamisi tarehe 22 Agosti 2024, ambayo inatoa idhini ya kuendelea na agizo lililopendekezwa la "nihil obstat" (hakuna kizuizi hivyo niidhini) inayohusiana na “Mama Yetu wa Huruma,” anayeheshimiwa katika Madhabahu ya Pellevoisin, mji mdogo katikati mwa Ufaransa, ambapo mnamo 1876 mjakazi maskini, Estelle Faguette, aliripotiwa kuwa na matokeo mbalimbali ya Bikira Maria. Katika barua ya Mkuu wa Baraza, Kardinali Fernandez anaandika kuwa: “Ingawa si mazoezi ya sasa ya Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa, kujieleza yenyewe juu ya tabia isiyo ya kawaida au asili ya kimungu ya matukio ya juu ya asili na ujumbe unaodaiwa, maneno ambayo Estelle aliwasilisha kama yanatoka kwa Bikira Maria yana thamani fulani ambayo hutuwezesha kuona kitendo cha Roho Mtakatifu katikati ya uzoefu huu wa kiroho.”

Ibada inayopendekezwa

Mkuu wa Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa anasema: “sio tu kwamba hakuna pingamizi za mafundisho, maadili au zingine kwa tukio hili la kiroho ambalo waamini wanaweza kutoa kibali chao kwa busara (Kanuni, kifungu cha 22). , 1), lakini kwamba katika kesi hii ibada, ambayo tayari inastawi, inapendekezwa hasa kwa wale ambao kwa hiari wanataka kushikamana nayo, kwani kuna njia ya usahili wa kiroho, uaminifu, upendo ambao utafanya wema mkubwa na ambao utafanya hakika liwe zuri Kanisa zima.”

Barua ya Estelle kwa Bikira

Estelle alizaliwa mnamo tarehe 12 Septemba 1843 katika familia maskini sana. Ili kuweza kujikimu yeye mwenyewe na wazazi wake, kwanza alifanya kazi kama mwoshaji na kisha kama mfanyakazi wa nyumbani. Aliugua sana na maisha yake yalikuwa hatarini. Kwa wakati huo aliamua kuandika barua ya dhati kwa Maria ili apate nafuu na aendelee kusaidia wazazi wake maskini. Kardinali anaandika kuwa “ Maneno yake yanashangaza kwa urahisi, uwazi na unyenyekevu. Estelle alisimulia mateso yaliyosababishwa na ugonjwa wake. Hakujivunia roho ya Kikristo ya kujiuzulu. Badala yake, alielezea upinzani wake wa ndani kwa ugonjwa ambao ulivuruga mpango wake wa maisha. Lakini mwishowe daima alitegemea mapenzi ya Mungu. Alitaka tu kumsaidia baba na mama yake kwa nguvu zote alizobaki nazo, yaani Kujitolea huku kwa ukarimu kwa wengine, maisha haya ambayo alitumiwa kutunza wengine, ndio yaligusa moyo wa Mama zaidi ambaye anajua kutambua kila mtu uzuri unaojificha nyuma ya maneno yetu.”

Uponyaji wa kimiujiza

Mwanamke huyo kijana alisema kwamba mnamo Februari 1876, akiwa na umri wa miaka 32, kuwa maonesho ya kwanza yalianza siku ya tano, kama alivyoahidi Maria, alipona kabisa. Estelle alikuwa wazi sana juu ya kile kilichotokea kwa sababu Bikira alimpatia uponyaji wake kutoka kwa Mwanawe. Kila kitu kinahusishwa na Kristo, ni Kristo ambaye alisikiliza maombezi ya mama yake. Uponyaji - anasisitiza Kardinali Fernandez - uliothibitishwa kuwa wa kimuujiza na Askofu Mkuu wa Bourges, tarehe 8 Septemba 1893, kwa idhini ya Ofisi Takatifu ya wakati huo.

Baadhi ya ujumbe kutoka kwa Maria

Katika jumbe zake, Maria alimwonesha Estelle ukaribu wake wote na huruma kwa maneno ya kutia moyo kwamba “Usiogope chochote, wewe ni binti yangu, Ikiwa unataka kuwa katika huduma yangu, kuwa rahisi, jasiri, nitafanya kuwa karibu nawe bila kuonekana […] Huna cha kuogopa. Ninachagua wadogo na wanyonge kwa ajili ya utukufu wangu.” Na kisha  alitoa ushauri wa kuwa na amani: “kuwa mtulivu, binti yangu, kuwa na subira, utakuwa na mateso fulani, lakini niko hapa. Ningependa uwe na utulivu zaidi [...] Unahitaji kupumzika.” Mwaliko pia ulielekezwa kwa Kanisa kwamba: “Kanisani hakuna utulivu ninaoutamani.”

Uwepo wa kimya

Kardinali vile vile amesema kuwa “Mara nyingi hata zaidi ya maneno machache ya Maria, kinachoshangaza ni uwepo wake wa kimya, kimya hicho cha muda mrefu ambapo macho ya Mama huponya nafsi. Estelle aliandika: “Mungu wangu, jinsi gani alivyokuwa mzuri! Alikaa kimya kwa muda mrefu bila kusema chochote [...] Baada ya ukimya huu, alinitazama; Sijui nilihisi nini; jinsi nilivyokuwa na furaha!. Hakuniambia chochote. Kisha akanitazama kwa wema mkubwa na akaenda zake. Kila mara alinitazama akitabasamu. Uzuri gani na utamu gani!. Ni wema ulioje machoni pake na huruma iliyoje!”

Skapulari yenye sura ya Moyo wa Kristo

Katika maandishi ya Kardinali anaendelea kuwa: “Uzoefu wa Pellevoisin ni wa Maria, lakini wakati huo huo ni wa Kikristo. Hivyo ombi kuu ambalo Bikira alimweleza  Estelle ni kwamba, aeneze skapulari yenye sura ya Moyo wa Kristo, na ujumbe mkuu wa Maria ni mwaliko wa kuugeukia Moyo huo wa upendo wa Bwana. Akimwonesha Estelle skapulari ya Moyo Mtakatifu wa Kristo, Maria alisema: “Hazina za Mwanangu zimekuwa wazi kwa muda mrefu [...] Ninapenda ibada hii.” Estelle alikaribisha ombi hili la kueneza ibada kwa Moyo wa Bwana.”

Kardinali Fernandez  alibanisha kuwa: “Moyo wa Kristo kamwe haujali, unajiruhusu kuguswa na sala zetu za dhati na za upendo, hasa ikiwa ni Mama anayegusa Moyo wake.” Maisha ya Estelle yalipitia katika unyenyekevu kati ya majaribu mengi, shutuma na kashfa. Mnamo 1925 alijiunga katika Shirika la Tatu la Wadominikani na alifarikia huko Pellevoisin mnamo tarehe 23 Agosti 1929 akiwa na umri karibu miaka 86. Kardinali Fernandez alikumbusha kwamba, Mapapa mbalimbali waliidhinisha ishara za ibada zinazohusishwa na “Mama yetu wa Huruma” ambaye pia anajulikana kwa jina la Mama Mwenye Huruma”, na mnamo mwaka 1892, Papa Leo XIII alitoa msamaha kwa mahujaji waliofika huko Pellevoisin na mwaka 1900 alitambua Skapulari ya Moyo Mtakatifu.

Misa ya Ibada ya Maria wa Huruma tarehe 9 Septemba

Kunako mwaka wa 1915, Papa Benedikto  XV kwa kupokea Skapula, alithibitishwa kuwa "Pellevoisin ilichaguliwa na Bikira Matakatifu kama mahali maalum  pa kueneza neema zake.” Kunako mwaka 1922 walilidhia kufanya ibada  ya misa kwa Bikira tarehe 9 Septemba kwa ajili ya Parokia ya Pellevoisin.  Kwa mujibu wa Kardinali Fernández amethibitisha kwamba “Katika miaka hii yote matunda mengi mazuri ya imani na mapendo yamechanua kwa wale ambao wameishi ibada hii.”

Maria wa Huruma huko Pellevoisin,Ufaransa
30 August 2024, 10:30