Mkutano Rimini:Ask.Mkuu Paglia:uongofu wa kiroho ili kujenga amani
Na Massimiliano Menichetti naAndrea De Angelis - Rimini
Amani inayojengwa kwa kuchukua mateso ya wengine moyoni, ambayo huzaliwa kutokana na uongofu wa kiroho kwa ugunduzi mpya wa Injili ndizo mada katika kitovu cha mahojiano na Askofu Mkuu Vincenzo Paglia, Rais wa Chuo cha Kipapa cha Maisha, katika studio za Radio Vatican - Vatican News, kwenye Mkutano wa Urafiki kati ya Watu huko Rimini utakaohitimishwa tarehe 25 Agosti 2024. Askofu Mkuu Paglia alifanya hotuba yake saa 9.00, alasiri katika meza ya mduara na mada ya Njia za Amani pamoja na Makamu wa Rais wa Baraza la Mawaziri na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa nchini Italia, Bwana Antonio Tajani. Kwa njia hiyo yafuatayo ni mahojiano na mwandishi wa habari wa Radio Vatican mara baada ya mkutano huo.
Kwa wengi, kwa neno amani linaonekana kama neno la mbali, lakini umesema mara kadhaa kwamba tusikate tamaa katika kuijenga, ukielekeza kwenye Hati za kitume mbili za Papa: Laudato si' na Fratelli tutti...
Hasa, kwa sababu kile kinachokosekana ulimwenguni leo hii, sio tu nchini Italia na Ulaya, ni maono. Kila nchi na hata kila mtu huwa anageuziwa kivyake, yaani dunia imekuwa ya utandawazi, uchumi umevamia sayari, lakini kila mtu anageuzwa kujitafutia na kutetea maslahi yake au njia za mtu binafsi. Papa Francisko anatupatia maono, tunaishi katika nyumba moja, ya sayari katika Laudato si' ; sisi ni familia moja ya watu wengi na huu ni udugu wa ulimwengu wote, na ndiyo maana kuwa na imani ya kuwa na Baba mmoja wa watoto hawa wote ni muhimu kwa amani. Tunatetemeka kwa kile ambacho Papa Francisko anakiita vita ya tatu ya dunia vilivyo megeka vipande vipande, lakini kiukweli tayari tunaipasua dunia vipande vipande, na tayari tunaisambaratisha kwa majanga yasiyofikirika: kiukweli kuna vita 59 vinavyoendelea, lakini kuna viwili ambavyo vinazungumzwa kila siku. Sasa chanzo chake ni nini? Ninaamini kuna haja ya uongofu wa kiroho, ili kuelewa kwamba tuna wajibu wa kila mtu. Huu ni unabii wa kiinjili ambao Papa Francisko anashikilia sana, lakini wengi wetu tunauweka chini ya pishi.
Baba Mtakatifu Francisko anazungumzia utandawazi wa kutojali, unaojumuisha pia kuchochea migogoro na vita. Je, hii inajengwaje kweli?
Watu wengi wanapigana vita lakini sote tunaweza kufanya amani ili pasiwepo anayeweza kusema sijali au ninaweza kufanya nini na vita vya Ukraine. Unaweza kuhuzunishwa na kile kinachotokea, kashfa, lakini unaweza kuombea, kushirikiana na wengi ambao wamejitolea kukuza amani au hata mshikamano. Kuna mambo mengi tunaweza kufanya. Kwa bahati mbaya, kinachoendelea ni kile ambacho rafiki mpendwa, Giuseppe De Rita, aliita dini mpya, yaani ubinafsi: ibada ya ubinafsi ambayo juu ya madhabahu yake hata upendo wa kupendeza hutolewa sadaka. Ni lazima tuhame kutoka katika ubinafsi huu wa uharibifu hadi kwenye udugu wetu. Haya ndiyo mapinduzi makubwa ambayo Papa Francisko anayazungumza na ningetumaini kwamba Makanisa yote, si yale ya Kikatoliki pekee yake, bali yote yakaungana pamoja. Kuna msemo mzuri wa Athenagoras, mhusika mkuu wa kukumbatiana na Papa Paulo VI, uliosema kuwa: “Makanisa dada, ndugu wa watu,” ikiwa makanisa yanagawanyika, watu watakuwaje? Hilo ndilo swali kubwa.
Pia kuna kitendawili: ubinafsi mwingi lakini pia hauna nguvu mbele ya uovu. Ni wapi pa kuteka ili tusijisikie wanyonge?
Kutoka katika Injili, ambayo inatuambia wazi kwamba kila kitu kinawezekana. Kugundua tena Neno la Mungu kama chanzo cha nguvu ya kihistoria na isiyo ya kufikirika. Sisi Wakristo tuna jukumu la kubadili ukweli: hivi ndivyo Yesu alivyofanya, aliwapatia wanafunzi uwezo wa kufanya vivyo hivyo na tunapaswa kuendelea katika barabara hiyo. Kwa usahihi mkuu, hebu tuanze tena kusoma Injili kila siku, tukiikaribisha kiukweli na kwamba mvutano wa ndani utakuwa ukweli wa kihistoria wa mabadiliko.
Hapa Rimini kuna ukweli mwingi tofauti, wakiwemo watu wasio Wakatoliki wanaokuja kuunda madaraja ya maarifa na mikutano: je, huu ndio ufunguo?
Ndiyo kabisa, Papa Paulo VI alikuwa ameianzisha katika Waraka wa Kitume wa kwanza wa “Ecclesiam suam, alioandika kwamba: “Mkristo kwa asili yake ni wa ulimwengu wote, katika Kanisa, katika uhusiano wake na Wakristo, na dini nyingine na hata na wale wasioamini.” Ndiyo maana Papa Francisko anazidi kusisitiza kwamba utetezi wa utambulisho unahitaji uwazi, na utetezi wa utambulisho ni kuwa ndugu wa wote: Francis wa Assisi, Charles de Foucauld ni baadhi ya mifano. Ningependa sisi sote Wakristo tupate mvutano huu ambao ni wa Mungu.
Ni nini muhimu katika kujenga amani?
Kupendana na kupenda.
Tafakari ya jinsi ilivyo muhimu kujenga amani katika familia binafsi, katika nyumba: kuwa mafundi wa amani lazima tuwe kitu kimoja katika nyumba...
Ndio kabisa, kwa sababu vita huanzia nyumbani, na baadaye huwa kubwa. Kwa maana hii, amani maana yake ni kupenda na kupendwa: tutunzane na pia tutashinda vita.