Tafuta

Papa Paulo VI: Kumbukizi ya Miaka 60 tangu alipoandika Waraka wa Kitume, "Ecclesiam Suam" Yaani "Kanisa la Kristo." Papa Paulo VI: Kumbukizi ya Miaka 60 tangu alipoandika Waraka wa Kitume, "Ecclesiam Suam" Yaani "Kanisa la Kristo."  (Vatican Media) Tahariri

Mtakatifu Paulo VI: Miaka 60 ya Waraka wa "Ecclesiam Suam": Majadiliano

Dr. Andrea Tornielli, Mhariri Mkuu wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano katika Tahariri yake kuhusu, Kumbukizi ya Miaka 60 tangu Mtakatifu Paulo VI alipochapisha Waraka wake wa Kichungaji "Ecclesiam Suam" "Kanisa la Bwana" anakazia kuhusu mchakato wa majadiliano katika ukweli na uwazi; katika upendo, uvumilivu na ukarimu. Ujumbe huu bado ni muhimu sana katika ulimwengu mamboleo; ni majadiliano katika ukombozi, utume wa Kristo Yesu wa Uinjilishaji!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mtakatifu Paulo VI mara tu baada ya kuchaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki tarehe 21 Juni 1963, kunako tarehe 10 Agosti 1964, Papa Paulo VI akachapisha Waraka wake wa kwanza wa Kitume unaojulikana kama "Ecclesiam suam" "Kanisa la Bwana" Waraka unaonesha dira na mwelekeo wa Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya Tatu ya Ukristo, kwa kuzingatia changamoto zilizotolewa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican yaani: Majadiliano ya kidini na kiekumene na kitamaduni, ili kukuza na kudumisha: haki, amani, ustawi na maendeleo ya watu; kujenga na kudumisha umoja wa Kanisa kwa ajili ya huduma kwa walimwengu. Mama Kanisa anapaswa kutambua asili, maisha na utume wake, kwa kujikita katika mchakato wa kujenga na kudumisha amani duniani.Mama Kanisa ana amana na utajiri mkubwa katika maisha na utume wake; amana na utajiri unaobubujika kutoka katika: Maandiko Matakatifu, Mafundisho tanzu ya Kanisa; Mamlaka fundishi ya Kanisa yaani “Magisterium,” Mababa wa Kanisa bila kusahau mchango wa wasomi. Yote haya yanapania pamoja na mambo mengine kusaidia mchakato wa kujikita katika ukombozi. Kristo Yesu anaendelea kulipyaisha Kanisa lake sanjari na kuyatakatifuza malimwengu mimntarafu Mafundisho ya Mtaguso mkuu wa pili wa Vatican kwa kuonesha utii kwa Kristo Yesu na Kanisa lake; kwa kujikita katika utii kwa Kristo Yesu. Majadiliano yasaidie kukoleza safari ya ukombozi.

Majadiliano katika ukweli na uwazi ni chanzo cha amani ya kudumu.
Majadiliano katika ukweli na uwazi ni chanzo cha amani ya kudumu.

Ni katika muktadha huu, Papa Paulo VI akafanya hija ya kitume Nchi Takatifu ili kukutana na kusali na Patriaki Anathegoras, mwanzo wa mchakato wa majadiliano ya kiekumene kati ya Makanisa. Mtakatifu Paulo VI katika Waraka huu analitaka Kanisa kutambua dhamana na wajibu wake; kuanza mchakato wa kujipyaisha kwa kujielekeza katika majadiliano ya kidini na kiekumene, ili dunia iweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi. Papa Paulo VI anapenda kuwaambia watu wa Mataifa kwamba, Kanisa limebarikiwa kuwa na amana ambayo watu wanaitafuta katika historia ya maisha yao. Ni Waraka unaojikita katika fadhila ya mapendo kwa Mungu na jirani. Ni kutokana na mwelekeo huu, Kanisa halina budi kuwashirikisha watu upendo unaobubujika kutoka kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Watu watambue kwamba, Kristo Yesu ndiye ile hazina iliyofichika machoni pa wengi, lakini ni muhimu sana katika maisha ya watu. Tafakari ya kina iliyofanywa na Mtakatifu Paulo VI, ilihitimishwa tarehe 11 Julai 1964. Kuanzia tarehe 6 Agosti 1964 alianza utume wake mjini Vatican, wakati Mama Kanisa alipokuwa anaadhimisha Sikukuu ya Kung'ara kwa Bwana, kielelezo cha ufunuo wa Mungu na utukufu wa Kristo Yesu, ili kuwaimarisha Mitume wake waweze kukabiliana barabara na Kashfa ya Msalaba. Miaka kumi na minne baadaye, Papa Paulo VI tarehe 6 Agosti 1978, akiwa Ikulu Ndogo ya Castel Gandolfo, akafariki dunia, huku akiwa anasali, ile sala kuu, yaani Sala ya Baba Yetu.

Majadiliano ya kiekumene ni muhimu katika maisha na utume wa Kanisa
Majadiliano ya kiekumene ni muhimu katika maisha na utume wa Kanisa

Dr. Andrea Tornielli, Mhariri Mkuu wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano katika Tahariri yake kuhusu, Kumbukizi ya Miaka 60 tangu Mtakatifu Paulo VI alipochapisha Waraka wake wa Kichungaji "Ecclesiam suam" "Kanisa la Bwana" anakazia kuhusu mchakato wa majadiliano katika ukweli na uwazi; katika upendo, uvumilivu na ukarimu. Ujumbe huu bado ni muhimu sana katika ulimwengu mamboleo; ni majadiliano katika ukombozi, utume wa Kristo Yesu unaofumbatwa katika upendo; watu wakiwa huru, kuupokea au kuukataa na wala hakuna sababu ya kujiundia maadui. Majadiliano ni mchakato wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu; mchakato unaofumbatwa katika toba na wongofu wa ndani kwa kutambua kwamba, hii ni neema ya Mungu kwa ajili ya wokovu wa walimwengu; upendo kwa Mungu na jirani. Ikumbukwe kwamba, wokovu ni kwa ajili ya wote. Mchakato wa majadiliano unafumbatwa katika ukweli na upendo. Waamini wanapaswa kujizatiti kikamilifu kwa kutambua kwamba, wanaitwa na kutumwa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Mama Kanisa anapenda kuimarisha majadiliano katika ukweli na uwazi, katika ulimwengu anamoishi na kutenda, tayari kujielekeza katika toba na wongofu wa ndani anasema, Mtakatifu Paulo VI. Mtakatifu Paulo VI katika Waraka wake wa Kitume "Ecclesiam suam" "Kanisa la Bwana" anakaza kusema, Kristo Yesu ndiye Muasisi wa Kanisa lake na wala hii si kazi ya mikono ya wanadamu wala ujasiri wa kibinadamu. Ubora na ufanisi wa Kanisa hautegemei “matangazo ya biashara” au kampeni au uwezo wake wa kujaza viwanja kwa mikutano mikubwa. Kanisa linajengwa na kuimarishwa kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko unaofanywa na “maskini wengi wa Kristo Yesu.” Hawa ni wadhambi waliosamehewa dhambi zao; watu waliokutana na Kristo Yesu katika hija ya maisha yao, akawapatia dira na mwongozo wa matumaini. Kanisa linataka kuwasaidia watu kukutana na Uso wa Kristo Yesu, kielelezo cha ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake.

Majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni ni muhimu sana
Majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni ni muhimu sana

Askofu mkuu Roberto Repole, wa Jimbo kuu la Torino, lililoko Kaskazini mwa Italia, katika mahojiano maalum na vyombo vya mawasiliano ya jamii vinavyomilikiwa na kuendeshwa na Vatican anasema, Waraka wa Kitume wa Papa Paulo VI "Ecclesiam suam" "Kanisa la Bwana" uliandikwa katika vuguvugu la maadhimisho ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican na hasa katika Waraka wake “Lumen gentium” yaani “Mwanga wa Mataifa: Juu ya Fumbo la Kanisa na Waraka wa “Gaudium et spes” yaani “Kanisa na Ulimwengu: Nyaraka hizi ni kielelezo cha mpango wa wokovu wa Mungu kwa binadamu. Kanisa linapaswa kutambuliwa kuwa limeasisiwa na Kristo Yesu na kwamba, hili ni Fumbo linalowaunganisha wabatizwa wote kushikamana katika mchakato wa ujenzi wa Kanisa la Kisinodi. Udhaifu na mapungufu ya waamini yanaweza kurekebishwa kwa kujikita katika toba na wongofu wa ndani. Huu ni wongofu wa kimisionari na kichungaji ili kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Majadiliano yasaidie kutangaza Injili ya Kristo na kutoa huduma kwa walimwengu pamoja na kukuza na kudumisha mawasiliano na watu wote wa Mungu. Mtakatifu Paulo wa VI alikazia ujenzi wa utamaduni wa kuheshimu utawala wa sheria, haki msingi za binadamu, utu na heshima ya binadamu pamoja na uhuru wa kweli. Hizi ni tunu msingi zinazopaswa kufanyiwa kazi hata katika ulimwengu mamboleo sanjari na kwamba, maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia yawe ni kwa ajili ya huduma kwa binadamu.

Majadiliano ya kidini ni sehemu ya vinasaba vya maisha ya Kanisa
Majadiliano ya kidini ni sehemu ya vinasaba vya maisha ya Kanisa

 

Tunu msingi za maisha ya kiroho zinasimikwa katika upendo kwa Mungu na jirani na kwamba, Kanisa ni mahali pa kukutana na Mungu na kwamba, lina amana na utajiri mkubwa ambao ikiwa kama utatumiwa na waamini, hawatakuwa na sababu ya kutangatanga katika maisha ya kiroho! Baba Mtakatifu Francisko anakazia uekumene wa upendo unaojikita katika udugu na urafiki; msamaha na upatanisho miongoni mwa Wakristo. Pili ni uekumene wa ukweli unaofumbata na kuambata majadiliano ya kitaalimungu kwa kushirikishana mang’amuzi na vipaumbele vya maisha na utume wa Makanisa kwa ajili ya ujenzi wa Ufalme wa Mungu. Tatu, Uekumene hauna budi kusimikwa katika umoja wa Wakristo unaoshuhudiwa katika sala ya pamoja; kwa kufanya kazi kwa ushirikiano; kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha misingi ya haki, amani, utu na heshima ya binadamu; kwa kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote. Wakristo watambue kwamba, umoja ni zawadi ya Roho Mtakatifu kwa Kanisa la Kristo! Nne, Baba Mtakatifu anazungumzia uekumene wa damu unaoshuhudiwa na damu ya Wakristo wanaoendelea kuteseka na kunyanyaswa sehemu mbalimbali za dunia! Askofu mkuu Roberto Repole, wa Jimbo kuu la Torino, anasema, majadiliano ya kidini na kiekumene yanasaidia kujenga na kuimarisha misingi ya haki, amani, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi; umoja na amani kwa watu wote wa Mungu.

Ecclesiam Suam

 

 

02 August 2024, 15:40