Askofu Michael George Mabuga Msonganzila wa Jimbo Katoliki la Musoma, Tanzania, tarehe 29 Agosti 2024 ameadhimisha Jubilei ya Miaka 40 tangu alipopewa Daraja Takatifu ya Upadre. Askofu Michael George Mabuga Msonganzila wa Jimbo Katoliki la Musoma, Tanzania, tarehe 29 Agosti 2024 ameadhimisha Jubilei ya Miaka 40 tangu alipopewa Daraja Takatifu ya Upadre. 

Papa Francisko Ampongeza Askofu Msonganzila Kwa Miaka 40 ya Daraja ya Upadre

Askofu Michael George Mabuga Msonganzila wa Jimbo Katoliki la Musoma, Tanzania, tarehe 29 Agosti 2024 ameadhimisha Jubilei ya Miaka 40 tangu alipopewa Daraja Takatifu ya Upadre na mahubiri kutolewa na Kardinali Polycarp Pengo, Askofu mkuu mstaafu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam. Maadhimisho haya yamefanyika kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume Mjini Musoma. Baba Mtakatifu Francisko amempongeza kwa kuadhimisha Miaka 40 ya Daraja ya Upadre.

Na Daniel Benno Msangya, - Jimbo Katoliki la Musoma, Tanzania.

Askofu Michael George Mabuga Msonganzila wa Jimbo Katoliki la Musoma, Tanzania, tarehe 29 Agosti 2024 ameadhimisha Jubilei ya Miaka 40 tangu alipopewa Daraja Takatifu ya Upadre na mahubiri kutolewa na Kardinali Polycarp Pengo, Askofu mkuu mstaafu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam. Maadhimisho haya yamefanyika kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume Mjini Musoma. Naibu wa Askofu wa Jimbo la Musoma Padre Julius Ogolla alitangaza salamu za Baba Mtakatifu Francisko alizotumiwa Askofu Michael Msoganzila kwa hati maalumu ya pongezi kwa kutimiza Miaka 40 ya Upadre wake. Katika mahubiri yake Kardinali Polycarp Pengo, Askofu mkuu Mstaafu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam alirejea masomo ya Injili ya Luka akiwakumbusha waamini kutoa shukrani kama mmoja wa wakoma kumi waliopata kuponeshwa na kisha peke yake akarudi kutoa shukrani. Kardinali Pengo ambaye ametimiza miaka 40 ya uaskofu wake amesema wanadamu wanashindwa kutoa shukrani kwa Mwenyezi Mungu na kuhoji kwanini wakoma wengine tisa walishindwa kurudi kutoa shukrani? “Watu wamefanyiwa mambo mengi makubwa yaliyowaletea furaha lakini wanasahau kumrudia Mwenyezi Mungu na kutoa shukrani zao, jambo ambalo Askofu Msonganzila amelitambua na kumweka Mungu mbele kwa kutualika kushirikiana naye kutoa shukrani katika safari yake ya utumishi wa Kanisa la Mungu,” alisisitiza na kuendelea, “Mwanadamu anapata vitu vingi vya kufurahisha lakini anamweka Mungu katika viwango vya nafasi ya pili na mwisho katika maisha yake.”

Askofu Msonganzila amekoleza sana mchakato wa uinjilishaji wa kina.
Askofu Msonganzila amekoleza sana mchakato wa uinjilishaji wa kina.

Kardinali Pengo alihimiza kila mtu kujiuliza yupo kati ya wale wakoma kenda huku akitaka kutafakari ukuu wa matendo ya Mungu anayowafanyia wanadamu, “Mungu Mwenyezi amekuwa mstari wa mbele kututendea mema kwa huruma na ukarimu na kwa mambo mazuri, hatuna budi kurudi kumshukuru na kusema asante ili kulipa deni kubwa alilotushirikisha Askofu Msonganzila katika Jubilee yake ya miaka 40 tangu alipowekewa mikono kuwa ni Kasisi. Padre Julius Ogolla ambaye pia alikuwa Mwenyekiti wa Kamati Kuu ya Maandalizi ya maadhimisho hayo alisema katika Salamu zake za pongezi kuwa Askofu Michael Msonganzila alishiriki katika uundaji wa Jimbo la Bunda lililotengwa kutoka eneo la Jimbo la Musoma na Jimbo Kuu la Mwanza. Aidha Askofu Msonganzila ameimarisha taasisi, shule na huduma za kijamii za jimbo ambazo zimeongezeka na kuimarika huku akiwezesha mapadre kupata Bima ya afya, Mafrateri wakiongezeka kutoka 15 alipoingia Jimboni mwaka 2008 hadi kufikia 52 hivi sasa na zaidi waamini wakitambua umuhimu wa kuwategemeza mapadre kwa mpango wa mshikamano. “Katika kipindi hiki hata waamini wameongezeka kutoka laki mbili na nusu hadi laki tatu na nusu, jumuiya ndogo ndogo zimeongezeka na kuimarika na watawa wameongezeka ndani ya Jimbo letu,” alisema Naibu wa Askofu katika orodha ya mafanikio mengi aliyotaja.

Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania linampongeza Askofu Msonganzila
Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania linampongeza Askofu Msonganzila

Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) limempongeza Askofu Michael Msonganzila wa Jimbo Katoliki la Musoma kwa uamuzi wake wa kuunga mkono jitihada za kutetea, kulinda na kuonesha njia kwa vitendo kwa kuwapa ulinzi watoto wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi ambao wamefanyiwa ukatili kwa kulazimishwa kukeketwa kutokana na mila kandamizi za baadhi ya jamii za Mkoa wa Mara, Kaskazini Magharibi Mwa Tanzania. Akitoa Salamu za pongezi za Baraza hilo kwa kutimiza miaka 40 ya ukuhani wake, Askofu Flavian Matindi Kassala wa Jimbo Katoliki la Geita amesema, Baraza hilo linatambua mchango wa Askofu Msonganzila aliyejitolea kwa vitendo kuwasaidia mabinti wanaokumbwa na nyanyaso, ukatili na mila na desturi kandamizi zikiwemo za ukeketaji. Amesema wengine wanaishia kutetea kwa maneno lakini Askofu Msonganzila ameonesha mfano kwa kwa vitendo kwa Kanisa na Serikali kuwajengea makazi na kuwapa sehemu ya kukimbilia mabinti wanaotishiwa kufanyiwa ukatili na kwamba akishirikiana na mjane wa Hayati Rais wa Msumbiji Mama  Graca Samora Marshel na wadau wengine, waliunda taasisi maalumu ambayo imewasaidia mabinti hao na kutetea haki zao katika jamii kwa kutoa huduma muhimu za kibinadamu, ikiwemo elimu, afya na makazi kwa mabinti wenye mazingira magumu na hatarishi.

Idadi ya waamini imeongezeka maradufu Jimboni Musoma
Idadi ya waamini imeongezeka maradufu Jimboni Musoma

Askofu Flavian Matindi Kassala amesema huduma hiyo imeonesha kwamba Askofu Msonganzila ametumia karama na mapaji yake kwa kuendelea kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu kwa watu wenye shida. Akiwa Padre alikuwa mhudumu wa Sekretarieti ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, kwa kulijenga Kanisa akiwakilisha Mashirika ya Kimisionari ya Kipapa, PMS, katika Taifa la Tanzania, mbali na kuwa mlezi wa waseminaristi. Baraza hilo pia limempongeza kwa kutumiza mwaka wa 17 tangu alipotawazwa kuwa Askofu wa Jimbo la Musoma mwaka 2008 na kushirikiana na wanajimbo kujenga Kanisa la Mungu kiroho na kimwili.

Mazoezi ni muhimu ili kuimarisha afya ya roho na mwili
Mazoezi ni muhimu ili kuimarisha afya ya roho na mwili

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa mchango wa shilingi milioni 30 kwa ajili ya kusaidia shughuli za kiroho zinazotekelezwa na Jimbo Katoliki la Musoma. Fedha hizo zimewasilishwa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Deogratius Ndejembi ambaye amemwakilisha Rais Samia katika Jubilei ya Miaka 40 ya Upadre ya Askofu Michael Msonganzila wa Jimbo Katoliki la Musoma. Waziri Ndejembi amesema Serikali ya Tanzania inatambua na kuthamini mchango wa viongozi wa dini katika kujenga amani, umoja, upendo mshikamano na kuliombea taifa, hivyo itaendelea kushirikiana nao kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Watanzania. Maaskofu waliohudhuria ni pamoja na: Askofu mkuu Renatus Leonard Nkwande wa Jimbo kuu la Mwanza, Askofu mkuu Issack Massawe wa Jimbo Kuu la Arusha, Askofu Joseph Roman Mlola ALCP/OSS wa Jimbo Katoliki la Kigoma, Askofu Ludovick Minde wa Jimbo Katoliki la Moshi, Askofu Salutaris Libena wa Jimbo Katoliki la Ifakara, Askofu Simon Masondole wa Jimbo Katoliki la Bunda na Askofu Msaidizi mstaafu Methodius Kilaini wa Jimbo la Bukoba. Wengine ni wawakilishi wa majimbo, taasisi za Baraza za Maaskofu ikiwemo Seminari Kuu ya Mwenda Kulima ya Kahama, Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino Tanzania (SAUT), Hospitali ya Bugando na wakuu wa mashirika ya kitawa na kazi za kitume.

Falsafa ya Neno Asante ni kuomba tena!
Falsafa ya Neno Asante ni kuomba tena!

Katika mahojiano maalum na mwandishi wa makala haya miaka kumi iliyopita Askofu Msonganzila aliyeanza utume wake katika Jimbo la Musoma amefanikiwa kwa ushirikiano na Serikali na wadau wengine kuimarisha huduma kwa wananchi wa Mkoa wa Mara kwa kutoa elimu na malezi yanayolenga kuimarisha dhana ya kujitegemea. Mingoni mwa mafanikio hayo ni kurejesha hali ya amani ambayo ilitoweka katika baadhi ya maeneo kutokana na mapigano ya jadi baina ya koo za jamii ya Wakurya hasa Warenchoka na Wanchari katika Wilaya ya Tarime, Mkoani Mara. “Tumeendeleza jitihada za kuhakikisha wananchi wanapata amani na kudumisha amani,” alisema Askofu Msonganzila ambaye alitumia muda mfupi kutoa shukrani kwa wazazi wake: Marehemu Mathias Andrea Msonganzila na mama yake Marehemu Tecla Kayayabo Msonganzila, viongozi wa dini waliohudhuria maadhimisho hayo na wote walioshiriki katika malezi yake wakiwemo makatekista, walimu wa ngazi zote waliomfundisha akiwemo Askofu Msaidizi Mstaafu Methodius Kilaini na wengine waliomsaidia kufikia hatua hiyo wakiwemo mapadre, watawa na waamini wa Jimbo la Musoma.

Bp Mmsonganzila
31 August 2024, 15:23