Sera na Mikakati ya Chuo Kikuu cha Kikatoliki Cha Sacro Cuore Kwa Miaka Mitano
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Ibada kwa Moyo Mtakatifu wa Yesu inapata chimbuko lake pale juu Msalabani, askari alipomchoma Kristo Yesu kwa mkuki ubavuni, mara ikatoka damu na maji, alama za Sakramenti za Kanisa. Kunako mwaka 1673 Mtakatifu Margherita Maria Alacoque akatokewa na Kristo Yesu na kumpatia dhamana ya kutangaza na kueneza Ibada kwa Moyo Mtakatifu wa Yesu. Hiki ni kielelezo cha ndani kabisa cha upendo na huruma ya Mungu kwa binadamu, lakini zaidi kwa wadhambi wanaothubutu kutubu na kumwongokea Mungu, tayari kuambata utakatifu wa maisha na kutembea katika mwanga wa Kristo Mfufuka! Baba Mtakatifu Francisko anawaalika kwa mara nyingine tena Mapadre na waamini walei kujichotea utajiri wa maisha ya kiroho unaofumbatwa katika Waraka wa Kitume wa Papa Pio XII, “Haurietis acqua” wa Mwaka 1956 kuhusu “Moyo Mtakatifu wa Yesu kiini cha huruma ya Mungu.” Ni katika muktadha huu, Chuo Kikuu Cha Kikatoliki cha Moyo Mtakatifu wa Yesu “Università Cattolica del Sacro Cuore” Jimbo kuu la Milano, kilianzishwa ili kujibu hitaji la mahali pa malezi na majiundo makini ya vijana wa kizazi kipya nchini Italia.
Changamoto hii ikavaliwa njuga na Padre Agostino Gemelli na wasaidizi wake wa karibu akina: Armida Barelli na Giuseppe Toniolo. Na matokeo yake katika kipindi cha uhai wake wa takribani miaka 100 iliyopita, Chuo hiki kimeendelea kukua na kupanuka na hatimaye, kuwa ni jukwaa la malezi na majiundo makini ya kielimu kitaifa na kimataifa! Ni kati ya vyuo vikuu vya kikatoliki maarufu sana Barani Ulaya. Kuna zaidi ya wanafunzi 43, 302 wanaopata elimu bora inayokidhi viwango vya soko la ajira Barani Ulaya. Ni Chuo kikuu ambacho kimewekeza sana katika tafiti makini, ili kuendelea kusoma alama za nyakati. Haya ni matokeo ya sadaka kubwa ya akili, sadaka na ukarimu inayotekelezwa na wadau wa Jumuiya ya Chuo Kikuu, bila kusahau kwamba, wanafunzi wana imani na wanathamini sana mchango huu. Kumbe, kuna haja ya kukazia ari na mwamko wa kimisionari, tayari kutoka na kuanza kufanya tafiti za ukweli, ustawi na maendeleo ya wengi. Chuo Kikuu kiwe ni mfano bora wa kuigwa katika ukarimu, huduma makini kwa wanafunzi, kwa kutafuta na kuambata mafao ya wengi, sanjari na kupambana na changamoto mamboleo kuhusu: utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji duniani; mifumo mbalimbali ya ubaguzi, ukosefu wa haki, amani, maridhiano sanjari na kupambana kufa na kupona na umaskini wa hali na mali sehemu mbalimbali za dunia.
Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu tarehe 12 Agosti 2024 amekutana na kuzungumza na Profesa Elena Beccalli, Gambera wa Chuo Kikuu Cha Kikatoliki cha Moyo Mtakatifu wa Yesu “Università Cattolica del Sacro Cuore” Jimbo kuu la Milano, ambaye tangu tarehe Mosi, Julai 2024 ameshikilia hatamu za uongozi Chuoni hapo. Profesa Beccalli amemshukuru na kumpongeza Baba Mtakatifu Francisko kwa uwepo wake wa karibu kwa vyuo vikuu vya Kikatoliki nchini Italia, ambavyo vimeendelea kutoa huduma kwa Kanisa nchini Italia na Kanisa la Kiulimwengu. Hiki ni Chuo kikuu cha Kikatoliki kinachoendelea kujipyaisha kwa kusoma alama za nyakati; kwa kujisadaka kwa ajili ya vijana wa kizazi kipya, na kuendelea kutoa elimu makini kwa vijana, ili waweze kukabiliana kikamilifu na changamoto mamboleo zinazoendelea kuibuka kila kukicha katika Ulimwengu mamboleo unaojipambanua kwa maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia. Hiki ni Chuo kikuu kinachoendelea kufanya upembuzi yakinifu kuhusu maana ya kuwa ni Chuo Kikuu cha Kikatoliki katika mwanga wa kutafuta na kuambata Ukweli. Profesa Elena Beccalli, Gambera wa Chuo Kikuu Cha Kikatoliki cha Moyo Mtakatifu wa Yesu “Università Cattolica del Sacro Cuore” ametumia fursa hii, kumwelezea Baba Mtakatifu Francisko miradi mbalimbali inayotekelezwa katika Kipindi cha Miaka mitano kuanzia sasa katika vitivo vyake vilivyoko: Milano, Brescia, Piacenza, Cremona na Roma. Lengo ni kuendelea kuchangia mawazo katika masuala mtambuka yanayovuka mipaka katika mtazamo wa Kimataifa.