CEAMA” kuanzia tarehe 23 hadi tarehe 26 Agosti 2024 limeadhimisha Mkutano wake! CEAMA” kuanzia tarehe 23 hadi tarehe 26 Agosti 2024 limeadhimisha Mkutano wake!  (J.Patias)

Umuhimu wa Mawasiliano Katika Ujenzi wa Kanisa Ukanda wa Amazonia, CEAMA

Dr. Paolo Ruffini, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano katika ujumbe wake kwa njia ya video anakazia pamoja na mambo mengine: Umoja, utume na ushiriki unaosimikwa katika imani kwa Mungu mmoja; Mawasiliano yajenge umoja kwa kuzungumzana na kusikilizana ili kuimarisha nguvu ya umoja. Hii ni sehemu ya mchakato wa ujenzi wa utamaduni wa mawasiliano unaojikita katika: majadiliano, uwezo wa watu kukutana pamoja na utunzaji bora wa mazingira.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mababa wa Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia, walipendekeza kuundwa kwa Baraza litakalosaidia kumwilisha dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa Ukanda wa Amazonia, kama sehemu ya mchakato wa uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Ni katika muktadha huu, kuanzia tarehe 26 hadi 29 Juni 2020, wajumbe kutoka kwenye “Mtandao wa Kanisa Amerika ya Kusini”, (Pan-Amazon Ecclesial Network of the Latin American Church, REPAM” waliunda Baraza la Makanisa Ukanda wa Amazonia: “Conferência Eclesial da Amazônia, CEAMA.” Hili ni tukio la matumaini ya Mababa wa Sinodi wakiwa wameunganika na Baba Mtakatifu Francisko ambaye amekuwa nao bega kwa bega katika mchakato mzima wa maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia. Wajumbe wa Baraza la Makanisa Ukanda wa Amazonia wanaoesha umoja katika utofauti wao kama ulivyofafanuliwa na Mababa wa Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia. Baraza linapania pamoja na mambo mengine, kutekeleza kwa dhati maamuzi na mapendekezo yaliyotolewa na Mababa wa Sinodi kwa ajili ya Ukanda wa Amazonia. Baraza linataka kujielekeza zaidi, ili kuwa ni daraja la utekelezaji sera na mikakati ya shughuli za kichungaji; kiuchumi, kijamii na kiikolojia ndani na nje ya Ukanda wa Amazonia.

Wajumbe wa CEAMA walipokutana na kuzungumza na Papa Francisko.
Wajumbe wa CEAMA walipokutana na kuzungumza na Papa Francisko.

Ni katika muktadha huu, Baraza la Makanisa Ukanda wa Amazonia: “Conferência Eclesial da Amazônia, CEAMA” kuanzia tarehe 23 hadi tarehe 26 Agosti 2024 limeadhimisha Mkutano wake, uliokuwa unanogeshwa na kauli mbiu: "Kristo Yesu anauonesha Ukanda wa Amazonia: Umoja, utume na ushiriki." Dr. Paolo Ruffini, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano katika ujumbe wake kwa njia ya video anakazia pamoja na mambo mengine: Umoja, utume na ushiriki unaosimikwa katika imani kwa Mungu mmoja; Mawasiliano yajenge umoja kwa kuzungumzana na kusikilizana ili kuimarisha nguvu ya umoja. Hii ni sehemu ya mchakato wa ujenzi wa utamaduni wa mawasiliano unaojikita katika: majadiliano, uwezo wa watu kukutana pamoja na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, sanjari na umwilishaji wa Injili ya upendo pamoja na kutunza mila na tamaduni njema za watu asilia. Huu ni wakati wa kugundua mawasiliano yanayosimikwa katika utu na heshima ya binadamu. Dr. Paolo Ruffini anakaza kusema, maadhimisho ya Mkutano Baraza la Makanisa Ukanda wa Amazonia huko Manaus, nchini Brazil ni sehemu ya mchakato wa hija ya pamoja katika mchakato wa ujenzi wa ushirika wa Kanisa, kwa watu wa Mungu Ukanda wa Amazonia kulainisha nyoyo zao, ili waweze kujikita katika ujenzi wa ushirika kwani wote wana imani kwa Mungu mmoja.

Umuhimu wa ujenzi wa utamaduni wa mawasiliano Ukanda wa Amazonia
Umuhimu wa ujenzi wa utamaduni wa mawasiliano Ukanda wa Amazonia

Mawasiliano katika mzizi  neno wake, yanapania pamoja na mambo mengine, kuwaunganisha watu, ili kuishi kwa pamoja kama zawadi safi kutoka kwa Mungu; kwa kujenga na kudumisha utamaduni wa kuzungumzana, kusikilizana na maelewano, ili kuweza kuthaminiana. Mawasiliano ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu yanayowaunganisha watu kutoka katika kila taifa, tamaduni na jamaa, ili kuweza kuimarisha nguvu ya umoja, tayari kushiriki katika maisha na utume wa Kanisa. Ni kwa njia hii, mawasiliano ni muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa Ukanda wa Amazonia, chachu ya mageuzi yanayohitajika na walimwengu katika ulimwengu mamboleo. Ni kwa njia ya mawasiliano thabiti, Ukanda wa Amazonia utaweza kushinda kishawishi cha kupenyeza kwa mfumo wa ukoloni mamboleo katika njia za mawasiliano. Mchakato wa mawasiliano ya kijamii usaidie ujenzi wa ulimwengu ulio bora zaidi unaosimikwa katika umoja. Huu ni mwaliko wa ujenzi wa mawasiliano bora yanayosimikwa katika utu wa binadamu na haki zake msingi; malezi na majiundo endelevu ya matumizi bora ya njia za mawasiliano kwa ajili ya maisha na utume wa Kanisa; mawasiliano yanayowajibisha.

Utunzaji Bora wa Mazingira ni wajibu wa kimaadili.
Utunzaji Bora wa Mazingira ni wajibu wa kimaadili.

Jamii inadai ujenzi wa utamaduni wa mawasiliano yanayosimikwa katika majadiliano katika ukweli na uwazi; mawasiliano yanayowawezesha watu kukutana sanjari na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Huu ni wakati wa kutangaza na kushuhudia Injili ya upendo. Maendeleo makubwa ya sayansi mnemba pamoja na mifumo ya kidigitali, lakini pia kuna haja ya kulinda, kuheshimu na kuthamini mila na desturi njema pamoja na tamaduni za watu asilia. Huu ni wakati wa kuangaliana machoni, ili kujenga na kudumisha umoja tayari kuangalia na kutambua.

Dr. Paolo Ruffini

 

27 August 2024, 14:26