Tafuta

Maadhimisho ya Kongamano la 53 la Ekaristi Takatifu Kimataifa “53rd International Eucharistic Congress” (IEC) Jimbo kuu la Quito lililoko nchini Ecuador . Maadhimisho ya Kongamano la 53 la Ekaristi Takatifu Kimataifa “53rd International Eucharistic Congress” (IEC) Jimbo kuu la Quito lililoko nchini Ecuador . 

Kongamano la 53 la Ekaristi Takatifu Kimataifa Quito: Hati ya Kutendea Kazi!

Hati ya Kutendea Kazi ya Maadhimisho ya Kongamano la 53 la Ekaristi Takatifu Kimataifa inazungumzia kuhusu: Ubinadamu uliojeruhiwa; Ubinadamu ulioinuliwa juu na Kristo Yesu; Udugu katika kuponya ulimwengu, ili waamini wote wawe wamoja. “Tunakuomba, uyaangalie matoleo ya Kanisa, na kwa kumtambua Yeye aliye Kafara ambaye ulitaka kutulizwa kwa sababu ya kifo chake utujalie sisi tunaotiwa nguvu kwa Mwili na Damu ya Mwanao, na kujazwa Roho wake... Umoja."

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Maadhimisho ya Kongamano la 53 la Ekaristi Takatifu Kimataifa “53rd International Eucharistic Congress” (IEC) Jimbo kuu la Quito lililoko nchini Ecuador yanaanza kutimua vumbi kuanzia tarehe 8 hadi tarehe 15 Septemba 2024 kwa kunogeshwa na kauli mbiu “Udugu wa kuponya Ulimwengu: “Nanyi nyote ni ndugu.” Mt 23: 8. Ujumbe wa udugu wa kibinadamu unagusa masuala mbalimbali ya kijamii, ndiyo maana Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kukimbilia Moyo Mtakatifu wa Yesu ili apate kuwaganga na kuwaponya. Maadhimisho haya yanakwenda sanjari na maadhimisho ya miaka 150 tangu Ecuador ilipowekwa chini ya ulinzi na mambolezi ya Moyo Mtakatifu wa Yesu, kisima cha huruma na upendo wa Mungu tarehe 25 Machi 1874. Hii ikawa ni nchi ya kwanza kabisa duniani kujiweka chini ya ulinzi na maombezi ya Moyo Mtakatifu wa Yesu. Kwa sasa Kanisa nchini Ecuador linataka kupyaisha Ibada kwa Moyo Mtakatifu wa Yesu katika maisha na utume wake, ili kuganga na kuponya nyoyo za watu waliojeruhiwa kwa matukio mbalimbali katika maisha yao. Hati ya Kutendea Kazi ya Maadhimisho ya Kongamano la 53 la Ekaristi Takatifu Kimataifa inazungumzia kuhusu: Ubinadamu uliojeruhiwa; Ubinadamu ulioinuliwa juu na Kristo Yesu; Udugu katika kuponya ulimwengu, ili waamini wote wawe wamoja. “Tunakuomba, uyaangalie matoleo ya Kanisa, na kwa kumtambua Yeye aliye Kafara ambaye ulitaka kutulizwa kwa sababu ya kifo chake utujalie sisi tunaotiwa nguvu kwa Mwili na Damu ya Mwanao, na kujazwa Roho wake Mtakatifu, tupate kuwa mwili mmoja na roho moja katika Kristo Yesu.” Rej. Sala ya Ekaristi III.

Hati ya Kutendea Kazi ya Kongamano la 53 la Ekaristi Takatifu Kimataifa
Hati ya Kutendea Kazi ya Kongamano la 53 la Ekaristi Takatifu Kimataifa

Hii ni ndoto ya ujenzi wa udugu wa kibinadamu na Zaburi ya udugu inayokita mizizi yake katika kumtukuza na kumshukuru Mungu; Kuomba; Kujizatiti na katika uzoefu. Hii ni changamoto kwa waamini kuhakikisha kwamba, uzoefu na mang’amuzi ya Kiekaristi yanamwilishwa katika uhalisia na vipaumbele vya maisha yao, tayari kutangaza na kushuhudia huruma na upendo wa Mungu unaobubujika kutoka katika Fumbo la Ekaristi Takatifu, tayari kujikita katika mchakato wa upatanisho. Kongamano la Ekaristi Takatifu ni muda muafaka wa kumwilisha zawadi ya Mungu kwa kutambuana wote kuwa ni ndugu wamoja, wanaofumbatwa katika upendo unaobubujika kutoka katika Moyo Mtakatifu wa Yesu. Huu ni mwaliko wa kujenga na kudumisha udugu wa kibinadamu na udugu na kazi ya uumbaji. Ni udugu uliojeruhiwa kiasi cha kwenda kinyume kabisa na mpango wa kazi ya uumbaji na huo ukawa ni mwanzo wa mateso na mahangaiko ya binadamu! Yuko wapi ndugu yako Abeli? Mwa 4:9. Huu ndio uadui unaoendelea kumwandama mwanadamu hata katika ulimwengu mamboleo, kinyume kabisa cha Mwenyezi Mungu asili na kilele cha maisha ya mwanadamu na kwamba, wote ni watoto wa Mwenyezi Mungu. Pili ni dhambi ambalo ni kosa dhidi ya akili, ukweli na dhamiri sahihi. Ni kushindwa kuwa na mapendo kweli kwa Mungu na jirani kwa sababu ya mapendo potofu ya mambo fulani. Hujeruhi tabia ya mtu na kuharibu mshikamano wa kibinadamu. Dhambi ni tamko, tendo, au tamaa kinyume cha sheria ya milele.

Kongamano la Ekaristi Takatifu: Kiini na hitimisho la maisha na utume wa Kanisa
Kongamano la Ekaristi Takatifu: Kiini na hitimisho la maisha na utume wa Kanisa

Dhambi ni kumkosea Mungu na ni kinyume cha utii wa Kristo Yesu unaoleta wokovu. Hata Mama Kanisa amejeruhiwa pia kutokana na dhambi za watoto wake. Kumbe, huu ni mwaliko wa kujipatanisha na Mungu, jirani na kazi ya uumbaji, kama alivyofanya Mtakatifu Oscar Arnulfo Romero, Shuhuda aliyesadaka maisha yake kwa ajili ya Kristo Yesu na Kanisa lake. Imeandikwa usiuwe! Huu ni udugu wa kibinadamu uliopyaishwa na Kristo Yesu na hivyo kuiwezesha jumuiya ya waamini kuadhimisha Fumbo la Ekaristi Takatifu, chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa unaobubujika kutoka katika Moyo Mtakatifu wa Yesu. Hili ni adhimisho la Meza ya Neno la Mungu na Ekaristi Takatifu sadaka inayojenga na kuimarisha udugu wa kibinadamu unaosimikwa katika: Liturujia na Sala; kwa kushiriki mateso ya Kristo Yesu. Rej. Sacrosanctum concilium, 12. Udugu wa kibinadamu unawaambata na kuwakumbatia maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii; hawa ni wale ambao Kristo Yesu katika maisha na utume wake, aliwapatia kipaumbele cha kwanza. Mt 25: 31-42. Kwa Kanisa Amerika ya Kusini, linapaswa kukisikiliza kilio cha watu asilia kama wa “Indios.” Kanisa linapaswa kuwa ni sauti ya kinabii, kwa wale wasiokuwa na sauti. Udugu wa kibinadamu usaidie kuponya majeraha ya walimwengu kama sehemu ya maadhimisho ya Fumbo la Pasaka, huku waamini wakijibidisha kuwa ni vyombo na mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu. Rej. Lk 9: 13. Mama Kanisa anakazia mchakato wa upatanisho na haki kwa kukiri kwamba, hata leo hii kuna vitendo vinavyosigana na udugu wa kibinadamu, mwaliko wa kujenga na kudumisha udugu wa kibinadamu kama anavyofundisha Kristo Yesu, Mwanakondoo wa Mungu aondoaye dhambi za ulimwengu.

Mashuhuda wa imani ni nguzo imara wa ujenzi wa Kanisa.
Mashuhuda wa imani ni nguzo imara wa ujenzi wa Kanisa.

Huu ni mwaliko wa kujenga na kudumisha utamaduni wa kusikiliza; kwa kujikita katika ujenzi wa udugu wa kibinadamu; katika umoja, unyenyekevu na upendo; udugu unaowafumbata na kuwaambata watu wote; tayari kuwa ni “Mkate unaomegwa kwa ajili ya jirani zao.” Ekaristi Takatifu inawawezesha waamini kuwa ni vyombo na mashuhuda wa udugu wa kibinamu, tayari kujikita katika ulinzi na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Huu ni mwaliko kwa waamini kugeuka na kuwa ni “Ekaristi” kadiri ya maisha na wito wa kila mwamini. Na huu ndio mwendelezo wa maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu nje ya kuta za Kanisa. Huu ni mwaliko kwa waamini wanaoshiriki Ekaristi Takatifu kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Kristo Yesu katika medani mbalimbali za maisha. Maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu yajenge na kuimarisha mchakato wa udugu wa kibinadamu. Kongamano la Ekaristi Takatifu iwe ni fursa ya kuimarisha: Imani katika Fumbo la Ekaristi Takatifu linaloadhimishwa na kumwilishwa katika uhalisia wa maisha na vipaumbele vya waamini. Ni mahali pa kutangaza na kushuhudia furaha na uchungu wa maisha; matumaini na ujenzi wa Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu inayopendwa na watu wa Mungu Amerika ya Kusini. Madhabahu ni mlango wazi wa uinjilishaji mpya unaokita mizizi yake katika moyo wa: Ukarimu kwa mahujaji; maisha ya sala, lakini zaidi kwa kuwasaidia waamini kujifunza kusali: Sala ya Kanisa sanjari na maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa, hususan Sakramenti ya Ekaristi Takatifu na Upatanisho, Mahakama ya huruma ya Mungu! Baba Mtakatifu Francisko anasema, Madhabahu yawe ni mahali pa sala na ukimya, ili kutoa nafasi kwa mahujaji kuzungumza na Mwenyezi Mungu kutoka katika undani wa maisha yao! Madhabahu ni mahali pa kuonjeshana upendo na ukarimu, ili kila hujaji anapofika mahali hapa aweze kujisikia kuwa yuko nyumbani anakaribishwa, kuthaminiwa na kupendwa. Kumbe, Madhabahu ya Bikira Maria Amerika ya Kusini ni mahali muafaka pa uinjilishaji wa kina, kwa waamini kujiaminisha chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria Mama wa Mungu na Kanisa. Maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu ni ufunguo wa umoja na ushirika kwa Kanisa la mbinguni na Kanisa linalosafiri hapa duniani.

Kongamano la Ekaristi 2024 Ecuador
07 September 2024, 13:06