Monsinyo Josep-Lluís Serrano Pentinat, Askofu mwandamizi mwenye haki ya kurithi Jimbo la Urgell, lililoko nchini Hispania akiwekwa wakfu tarehe 21 Septemba 2024. Monsinyo Josep-Lluís Serrano Pentinat, Askofu mwandamizi mwenye haki ya kurithi Jimbo la Urgell, lililoko nchini Hispania akiwekwa wakfu tarehe 21 Septemba 2024. 

Sifa Kuu za Askofu Mahalia: Mwinjilishaji, Mchungaji na Rafiki wa Maskini!

Yesu alimtazama Mathayo kwa upendo wa huruma na akamchagua: “miserando atque eligendo.” Askofu mkuu Edgar Peña Parra, anasema, utume wa kwanza wa Askofu ni kuwa kiongozi anayejisadaka kwa ajili ya huduma kwa watu wa Mungu, kwa kusikiliza mahitaji, kero na mahangaiko yao, ili aweze kuwa ni alama ya umoja na ushirika, tayari kutangaza na kushuhudia huruma na upendo wa Mungu usiokuwa na kikomo, kwa sababu Yesu amekuja kuwaita wadhambi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko anasema kwa ufupi sifa kuu za Askofu kuwa ni: unyenyekevu na huduma; mambo yanayofafanuliwa vyema na Mtakatifu Paulo, Mtume katika Waraka wake kwa Tito, akionesha mambo msingi yanayopaswa kufuatwa na kutekelezwa na Maaskofu, ili kukamilisha yale yanayopungua katika maisha na utume wa Kanisa; kwa kuwachagua na kuwasimika wazee wanaofaa kwa ajili ya uongozi wa Kanisa; watu wema na wenye kiasi, wapenda haki na watakatifu; watu wenye mifano bora ya kuigwa na jamii inayowazunguka. Askofu anayo dhamana ya kusali kwa ajili ya kuwaombea watu wote, kwa kutambua kwamba, kimsingi yeye ni mtu wa Mungu, aliyeteuliwa kati ya watu kwa ajili ya huduma, ili kuhakikisha kwamba, anakuza na kudumisha Ibada na Uchaji wa Mungu, mambo msingi katika kulinda na kudumisha utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.

Askofu mwandamizi Joseph Lluis Serrano Jimbo la Urgell
Askofu mwandamizi Joseph Lluis Serrano Jimbo la Urgell

Utume huu, umwezeshe Askofu kuwa ni kiongozi mkarimu, akitambua kwamba, Kristo Yesu ndiye anayewaita waja wake na kuwaweka wakfu ili kuendeleza kazi ya ukombozi! Ikumbukwe kwamba, kila Askofu, mbele ya watu watakatifu wa Mungu ni Mwinjilishaji, Mchungaji na Rafiki wa Maskini. Haya yamesemwa na Askofu mkuu Edgar Peña Parra, Katibu mkuu Msaidizi wa Vatican, Jumamosi tarehe 21 Septemba 2024 wakati alipokuwa anamweka wakfu Monsinyo Josep-Lluís Serrano Pentinat, Askofu mwandamizi mwenye haki ya kurithi Jimbo la Urgell, lililoko nchini Hispania na kama sehemu ya maadhimisho ya Sikukuu ya Mtakatifu Mathayo Mtume. Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kitume “Misericordia vultus” yaani “Uso wa huruma” anasema, Kristo Yesu ni ufunuo wa Uso wa huruma ya Mungu, muhtasari wa imani ya Kanisa ambayo imefunuliwa naye kwa njia ya: mafundisho, matendo na nafsi yake.

Askofu mwandamizi Joseph-Lluis Serrano Pentinat
Askofu mwandamizi Joseph-Lluis Serrano Pentinat

Fumbo la huruma ya Mungu ni chemchemi ya furaha, utulivu na amani ya ndani. Huruma ni ufunuo wa Fumbo la Utatu Mtakatifu, mwaliko na changamoto kwa waamini kuwa kweli ni mashuhuda na vyombo vya huruma na upendo wa Mungu. Kusamehe makosa ni kielelezo dhahiri cha upendo wenye huruma. Huruma ya Mungu ndiyo mahangaiko ya upendo wake kwa mwanadamu. Mwenyezi Mungu Anajisikia kuwajibika, kwani Mungu anataka kuwaona watoto wake wakiwa wamesheheni furaha na amani tele. Ni katika muktadha huu anasema kuitwa kwa Mathayo kumefanyika pia katika mazingira ya huruma. Akipitia kitengo cha mtoza ushuru, Yesu alimkazia Mathayo macho. Ulikuwa mtazamo uliojaa huruma, uliosamehe dhambi za yule mtu, mdhambi na mtoza ushuru ambaye Yesu alimchagua kinyume cha wasiwasi wa wanafunzi wengine, kuwa mmojawapo wa wale kumi na wawili.

Askofu mwandamizi Pentinat wakati wa Litania ya watakatifu
Askofu mwandamizi Pentinat wakati wa Litania ya watakatifu

Mtakatifu Beda Mwenyeheri, akizungumzia kifungu hiki cha Injili, ameandika kuwa Yesu alimtazama Mathayo kwa upendo wa huruma na akamchagua: “miserando atque eligendo.” Askofu mkuu Edgar Peña Parra, anasema, utume wa kwanza wa Askofu ni kuwa kiongozi anayejisadaka kwa ajili ya huduma kwa watu wa Mungu, kwa kusikiliza mahitaji, kero na mahangaiko yao, aweze kuwa ni alama ya umoja na ushirika, tayari kutangaza na kushuhudia huruma na upendo wa Mungu usiokuwa na kikomo, kwa sababu Kristo Yesu hakuja kuwaita wenye haki, bali wadhambi. Mt 9:13. Askofu mwandamizi Josep-Lluís Serrano Pentinat mwenye haki ya kurithi Jimbo la Urgell aliteuliwa na Baba Mtakatifu Francisko tarehe 12 Julai 2024 na kabla ya hapo, alikuwa akitekeleza dhamana na utume wake kwenye Sekretarieti kuu ya Vatican; utume ambao aliutekeleza kwa: Utii na unyenyekevu mkubwa na sadaka kubwa kwa Baba Mtakatifu na huduma kwa Kanisa la Kiulimwengu.

Askofu ni shuhuda wa huruma na upendo wa Mungu
Askofu ni shuhuda wa huruma na upendo wa Mungu

Lakini wajibu na dhamana kuu ni wito kutoka kwa Kristo Yesu anayewaita waje wake, ili kumfuasa, ili kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu, kwa kujivika tunu msingi za Kiinjili kama anavyokaza kusema, Mtakatifu Paulo, Mwalimu na Mtume wa Mataifa, kujitahidi kujenga Mwili wa Kristo katika: Roho mmoja, imani na ubatizo mmoja, huku wakijitahidi kuwa wakamilifu kama Kristo Yesu alivyo mkamilifu. Rej. Efe 4:1-3. 12-13.  Askofu mwandamizi Josep-Lluís Serrano Pentinat anaitwa na kutumwa kuwa ni shuhuda na chombo cha huruma na upendo wa Mungu usiokuwa na kifani. Kumbe, anaitwa Mchungaji mkuu kwa watu wa Mungu na rafiki wa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii; awe ni faraja kwa wale wanaoteseka kiroho na kimwili. Awe ni shuhuda wa haki, amani na ukweli; utume ambao ni muhimu sana kwa Askofu. Utume huu, unapaswa kupyaishwa daima kwa njia ya: Sala, Tafakari ya kina ya Neno la Mungu, Maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa kwa imani na uchaji pamoja na kujitahidi kumwilisha yote haya katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Ajitahidi kuwabeba watu wake moyoni mwake kwa njia ya sala; awe shuhuda wa imani na matumaini hasa miongoni mwa vijana wa kizazi kipya, ili aweze kuchoma na kuunguza ndani mwao tabia ya uchoyo na ubinafsi. Ajitahidi kukoleza moyo wa imani, matumaini na mapendo, kwa kujiaminisha kwa maongozi ya Roho Mtakatifu.

Kuwekwa wakfu Askofu
30 September 2024, 15:17